Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Ncha za Mabawa ya Ndege Wanaopaa Angani

Ncha za Mabawa ya Ndege Wanaopaa Angani

NDEGE inapopaa angani hufanya hewa izunguke haraka sana kwenye ncha za mabawa yake. Mizunguko hiyo ya hewa, hupunguza kasi ya ndege na kusababisha itumie mafuta mengi. Ndege zingine zilizo karibu zinaweza kuathiriwa na mizunguko hiyo ya hewa. Hivyo basi, ndege zinazotumia njia moja ya kurukia, zinahitaji kupeana muda wa kutosha kabla ya kupaa ili kuruhusu mizunguko hiyo ya hewa iishe.

Wahandisi wa ndege wamegundua njia ya kupunguza matatizo hayo. Ni njia gani hiyo? Ni kutengeneza ncha za mabawa kwa kuiga ncha za mabawa ya ndege wanaopaa angani kama vile korongo, tai, na aina fulani ya mwewe.

Fikiria hili: Ndege hao wanapopaa angani, manyoya yaliyo kwenye ncha za mabawa yao huinuka na kuwa wima. Kitendo hicho cha kusawazisha mabawa yake humwezesha ndege apae vizuri. Wahandisi wametengeneza mabawa ya ndege kwa kuiga muundo huo. Wakitumia bomba kubwa linalopuliziwa upepo kufanya uchunguzi, waligundua kwamba ncha za mabawa zinapoundwa vizuri na kufuata mkondo wa upepo, hufanya ndege isitumie mafuta mengi na hivyo kusafiri kwa kasi zaidi. Kufikia sasa wamefaulu kuboresha utendaji kazi wa ndege kwa asilimia 10 au zaidi. Kwa nini imekuwa hivyo? Kitabu Encyclopedia of Flight kinaeleza hivi: Ncha za mabawa ya ndege zinaongeza kasi yake na pia “hupunguza uvutano unaozuia ndege isiende kwa kasi.”

Hivyo basi, ncha za mabawa ya ndege huifanya ndege isafiri mbali zaidi, ibebe mizigo mizito zaidi, bila kulazimika kuwa na mabawa marefu. Jambo hilo hufanya ndege itumie mafuta kidogo na pia nafasi ndogo ya kuegesha. Kwa mfano, kulingana na ripoti ya shirika la NASA, mwaka wa 2010 pekee, kampuni za ndege “ziliokoa lita milioni 7,600 za mafuta ya ndege ulimwenguni pote” na hilo lilisaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na ndege.

Una maoni gani? Je, ncha zinazoinuka za mabawa ya ndege anayepaa angani zilijitokeza zenyewe? Au zilibuniwa?