Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Waliokoka Furiko!

Waliokoka Furiko!

Waliokoka Furiko!

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Uswisi

MNAMO Oktoba 2000, mafuriko yalitukia katika sehemu mbalimbali ulimwenguni. Milimani kulikuwa na mafuriko yaliyosababisha maporomoko ya matope, ambayo yalibeba kila aina ya takataka, hata miti!

Msiba huo ulitokea katika jimbo la Valais, kusini mwa Uswisi. Sehemu hiyo imepakana na Mto Rhône, unaoelekea magharibi kwenye Ziwa Geneva ukitokea kwenye barafu ya Rhône kwenye Milima ya Kati ya Alps—umbali wa kilometa 170 hivi. Maji yote yaliyo milimani humiminika kwenye mto huo kupitia kwenye vijito. Kwa kawaida, maji hayo hutiririka kwa utaratibu. Lakini msiba hutokea mvua inaponyesha kupita kiasi.

Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa huko Gondo, kwenye mpaka wa Italia. Maporomoko ya matope na mawe yaliharibu sehemu kubwa ya kijiji hicho kilicho mlimani chenye wakazi 150. Muda si muda kukawa na mafuriko katika sehemu nyingine za Valais. Barabara na reli zilifungwa na nyumba zilijaa matope na mawe. Katika sehemu fulani, kulikuwa na marundo ya matope yaliyojikusanya kufikia urefu wa meta 4. Mwanamke mmoja alitazama jinsi poromoko la matope lenye urefu wa meta 30 lilivyosomba miamba mikubwa na miti katika kijiji chao!

Markus na mke wake, Tabitha, walikuwa wanaishi mjini Mörel msiba huo ulipotokea. “Tuliamshwa na sauti kubwa na tetemeko baada tu ya saa 12 asubuhi,” Markus anakumbuka. “Nilishtuka sana nilipotoka nje na tochi na kuona kilichokuwa kimetokea. Nyumba na madaraja yalikuwa yameharibiwa na marundo ya miamba, na gari moja liligonga nyumba ya jirani yetu. Chini kidogo, jirani yetu na mke wake walizuiliwa nyumbani mwao. Niliwasaidia wapite dirishani. Niliporudi nyumbani, mimi na Tabitha tulikuwa na wakati mchache tu wa kukusanya vitu vyetu.”

Kwa kuwa Markus na Tabitha ni Mashahidi wa Yehova, walipata usalama kwa waamini wenzao ambao walikuwa mbali na eneo la msiba. Markus anasema: “Ingawa hatukuumia, msiba huo ulimfadhaisha Tabitha kwa siku nyingi.” Ni nini kilichomsaidia kuvumilia hali hiyo ngumu? Tabitha anasema: “Ni ushirika na msaada wa akina ndugu na dada zetu wa kiroho, na jinsi majirani wetu walivyotushughulikia.”

Markus na Tabitha walikumbuka andiko la Methali 18:24 linalosema kwamba kuna “rafiki anayeshikamana na mtu kwa ukaribu zaidi kuliko ndugu.” Marafiki kama hao ni wenye thamani sana wakati wa msiba!

[Ramani katika ukurasa wa 20]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Eneo lililoathiriwa

Gondo

[Picha katika ukurasa wa 20]

Markus na Tabitha

[Picha katika ukurasa wa 20]

Mise à disposition par www.crealp.ch