Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sukari Ni Muhimu kwa Uhai

Sukari Ni Muhimu kwa Uhai

Sukari Ni Muhimu kwa Uhai

HUENDA wewe hutumia sukari kufanya vyakula na vinywaji viwe vitamu, kama vile keki na kahawa. Lakini je, ulijua kwamba sukari inaweza kuleta maendeleo makubwa katika biolojia kama ilivyokuwa wakati chembe za DNA zilipovumbuliwa?

Gazeti New Scientist linasema kwamba katika miaka ya majuzi, wanasayansi wamechunguza jinsi chembe za mwili hutumia sukari rahisi kama glukosi kujenga molekyuli “zilizo tata na kubwa kuliko chembe za DNA na za protini. Sukari hutumiwa katika karibu taratibu zote za uhai, kama kutambua viini, kugandisha damu, na kuwezesha shahawa kupenya yai.” Vilevile inasemekana kwamba mtu huugua magonjwa mengi mwili wake unaposhindwa kutumia sukari, kama vile ugonjwa wa kuharibika misuli na baridi-yabisi. Ripoti hiyo inasema kwamba “sasa ndio wanabiolojia wanaanza kuelewa jinsi sukari hizo zinavyofanya kazi mwilini, na wanapofanya hivyo inawabidi kufikiria tena maoni ambayo yamekuwapo kuhusu utata wa uhai.”

Wanasayansi wametunga neno “glycome” ili kuonyesha utata wa sukari mbalimbali ambazo viumbe hutengeneza, kama neno “genome” linavyoonyesha chembe zote za urithi. Hata hivyo, Ajit Varki, mkurugenzi wa Kituo cha Uchunguzi na Elimu ya Sukari katika Chuo Kikuu cha California, San Diego, huko Marekani, anasema kwamba “huenda sukari ni tata mara elfu kadhaa kuliko chembe za urithi.” Kwa nini sukari hizo ni tata sana?

Ndani ya chembe, sukari rahisi yaani, monosakaridi, huungana na kufanyiza polisakaridi. Sukari hiyo nayo huungana na molekyuli zenye chembe zaidi ya 200 za sukari rahisi. Gazeti New Scientist linasema kwamba kwa kuwa sukari zinazofanyizwa huwa za miraba mitatu, “molekyuli ya sukari yenye chembe sita tu za sukari rahisi inaweza kuwa na maumbo bilioni 12 tofauti-tofauti.”

Varki alisema hivi kuhusu ugumu unaowakabili watafiti katika elimu hiyo mpya ya sukari: “Ni kana kwamba ndipo tu tumevumbua bara la Amerika Kaskazini. Sasa itatubidi tuwatume wavumbuzi kwenye bara hilo wachunguze ukubwa wake.”

Ni wazi kwamba utata wa chembe hai unaonyesha jinsi ilivyobuniwa kwa ustadi wa hali ya juu sana. Jambo hilo linawafanya wengi wawe na heshima na kicho. Je, unahisi hivyo? —Ufunuo 4:11.