Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Magonjwa Yanayosababishwa na Maziwa

Magonjwa Yanayosababishwa na Maziwa

Magonjwa Yanayosababishwa na Maziwa

SAA moja hivi imepita tangu ulipomaliza kula aiskrimu au jibini unayopenda sana. Tumbo lako limefura, linasokota, na lina gesi. Unameza dawa ambazo wewe hubeba kwa ukawaida. Sasa umeanza kujiuliza: ‘Kwa nini tumbo langu hunisokota kila wakati?’

Ikiwa unahisi kichefuchefu, tumbo linasokota, linafura, lina gesi, au unaharisha baada ya kunywa maziwa au kula vyakula vinavyotengenezwa na maziwa, huenda una ugonjwa unaosababishwa na maziwa (lactose intolerance). Ugonjwa huo huwapata watu fulani wanapotumia maziwa na bidhaa za maziwa. Ripoti ya Taasisi ya Kitaifa ya Magonjwa ya Kisukari, Tumbo, na Figo inasema kwamba “kati ya Wamarekani milioni 30 na 50 wana magonjwa yanayosababishwa na maziwa.” Kulingana na kitabu The Sensitive Gut, kilichochapishwa na Shule ya Kitiba ya Harvard, imekadiriwa kwamba “karibu asilimia 70 ya watu ulimwenguni huathiriwa na maziwa.” Hayo ni magonjwa ya aina gani?

Laktosi ni sukari inayopatikana katika maziwa. Utumbo mdogo hutoa kimeng’enya kinachoitwa lactase, ambacho huvunja laktosi ili iwe glukosi na galactose. Sasa damu inaweza kuitumia sukari hiyo. Lakini ikiwa hakuna kimeng’enya cha kutosha, laktosi huingia katika utumbo mkubwa bila kuvunjwa kisha huanza kuchacha na kutokeza asidi na gesi.

Dalili zilizotajwa awali huwapata watu wenye magonjwa yanayosababishwa na maziwa. Kimeng’enya cha lactase hutengenezwa kwa wingi mtu anapokuwa mtoto wa miaka miwili, kisha baada ya hapo huanza kupungua. Hivyo, huenda watu wengi wakaathiriwa na maziwa bila kujua.

Je, Ni Mzio?

Watu wengi hufikiri kwamba wana mzio wa maziwa wanapougua magonjwa yanayosababishwa na maziwa. Je, hiyo ni kweli? Wataalamu fulani wa mizio wanasema kwamba kwa ujumla, mizio ya chakula si mingi, na ni asilimia 1 mpaka 2 ambao huathiriwa. Watoto wengi zaidi huathiriwa ingawa hawazidi asilimia 8. Dalili za mizio na za magonjwa ya maziwa zinaweza kufanana, lakini kuna tofauti chache.

Mzio hutokea wakati mwili unapokuwa ukijikinga na kitu kibaya ambacho umekula au kunywa. Mwili hutokeza kemikali inayoitwa histamine. Dalili nyingine za mzio zinaweza kuwa kufura mdomo au ulimi, vipele, au pumu. Dalili hizo hazitokei mtu anapougua ugonjwa unaosababishwa na maziwa kwa sababu kinga ya mwili haihusiki. Badala yake mtu huwa mgonjwa kwa sababu tumbo hushindwa kusaga chakula vizuri.

Unawezaje kujua tofauti? Kitabu The Sensitive Gut kinajibu hivi: “Mizio halisi . . . hutokea dakika chache baada ya kula chakula kisichofaa. Dalili zikionekana zaidi ya saa moja baadaye, yaelekea huo ni ugonjwa unaosababishwa na maziwa.”

Jinsi Watoto Wanavyoathiriwa

Mtoto mchanga akiathiriwa na maziwa, yeye pamoja na wazazi wake wanaweza kutatizika sana. Mtoto akianza kuharisha, anaweza kuishiwa na maji mwilini. Huenda ikafaa wazazi wampeleke kwa daktari. Iwapo itagunduliwa kwamba anaathiriwa na maziwa, madaktari fulani hupendekeza apewe vyakula vingine badala ya maziwa. Wengi wamepata nafuu baada ya kufuata mapendekezo hayo.

Lakini ikiwa ana mzio, kuna sababu ya kuhangaika. Madaktari wengine huwapa dawa ya kuzuia histamine. Hata hivyo, ikiwa anashindwa kupumua, daktari atahitaji kufanya mengi zaidi ili kuzuia hali hiyo. Katika visa vichache, ugonjwa fulani hatari unaoitwa anaphylaxis hutokea.

Mtoto akianza kutapika, huenda ana ugonjwa mwingine unaoitwa galactosemia ambao hutokea mara chache. Kama ilivyotajwa mapema, lactase hutokeza sukari ya galactose, ambayo pia huhitaji kubadilishwa iwe glukosi. Sukari ya galactose ikirundamana mwilini, inaweza kuharibu ini, figo, kupungukiwa na akili, kupata ugonjwa wa hypoglycemia, na hata mtoto wa jicho (cataract). Hivyo ni muhimu kuacha kabisa kumpa mtoto maziwa au bidhaa za maziwa mapema.

Magonjwa Hayo Ni Hatari Kadiri Gani?

Tumbo la msichana mmoja lilikuwa na gesi nyingi na kufura. Hali yake ilipozidi kuwa mbaya, alienda hospitalini. Baada ya kufanyiwa uchunguzi mwingi, alipatikana na ugonjwa wa kufura tumbo. * Alipewa dawa za kuutibu. Hata hivyo, kwa kuwa hakuacha kutumia bidhaa za maziwa, dalili hazikutoweka. Baada ya kujifanyia uchunguzi mwenyewe, aligundua kwamba ugonjwa wake ulisababishwa na chakula, hivyo pole kwa pole akaacha kutumia vyakula fulani. Hatimaye aliacha kutumia bidhaa za maziwa kabisa, na ugonjwa wake ukaanza kwisha! Kabla ya mwaka mmoja kwisha, na baada ya kufanyiwa uchunguzi zaidi, daktari alimwambia kwamba hana ugonjwa wa kufura tumbo. Ugonjwa wake ulisababishwa na maziwa. Hebu wazia jinsi alivyofurahi!

Kwa sasa hakuna matibabu yanayoweza kumsaidia mgonjwa atokeze kimeng’enya cha lactase. Hata hivyo, kwa kawaida magonjwa yanayosababishwa na maziwa hayasababishi kifo. Basi unaweza kufanya nini ili ukabiliane na magonjwa hayo?

Wengine wamejaribu kula bidhaa za maziwa na kuona kiasi ambacho wanaweza kutumia bila kuathiriwa. Ukiwa mwangalifu kuona kiasi ambacho hakiwezi kukuathiri, unaweza kujua kiasi ambacho kinaweza kusagwa na tumbo lako.

Wengine wameamua kutotumia bidhaa za maziwa hata kidogo. Wengine wamefanya utafiti wao au kumuuliza mtaalamu wa chakula kuhusu njia nyingine za kupata kalisi wanayohitaji. Mboga na aina fulani za samaki na njugu zina kalisi nyingi.

Wale wanaotaka kuendelea kutumia bidhaa za maziwa wanaweza kununua dawa ambazo zina lactase ili kusaidia matumbo kuvunja-vunja laktosi. Dawa hizo zinaweza kumsaidia mtu asiathiriwe na maziwa.

Si rahisi kutunza afya siku hizi. Lakini kwa msaada wa utafiti wa kitiba na kinga ya mwili wetu, tunaweza kuvumilia mpaka wakati ambapo “hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa.’”—Isaya 33:24; Zaburi 139:14.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 15 Kuna aina mbili za magonjwa ya kufura tumbo—ugonjwa wa Crohn na ugonjwa wa kufura utumbo mkubwa. Magonjwa hayo hatari yanaweza kumfanya mtu akatwe sehemu ya utumbo inayougua na yakizidi yanaweza kuua.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]

VYAKULA HIVI HUENDA VIKAWA NA LAKTOSI:

▪ Mkate na bidhaa za mkate

▪ Keki na biskuti

▪ Chokoleti na peremende

▪ Unga wa viazi

▪ Majarini

▪ Dawa nyingi ambazo watu huandikiwa na daktari

▪ Dawa za dukani

▪ Unga na vitu vingine vinavyotumiwa kupika chapati za maji na biskuti

▪ Chakula cha nafaka kinachotumiwa kwa kiamsha-kinywa

▪ Viungo vya saladi

▪ Nyama zilizotengenezwa viwandani

▪ Michuzi mbalimbali