Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Marundo ya Mchanga Yenye Kustaajabisha Huko Poland

Marundo ya Mchanga Yenye Kustaajabisha Huko Poland

Marundo ya Mchanga Yenye Kustaajabisha Huko Poland

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Poland

PICHA zinazoonyesha sehemu za mashambani huko Poland kwa kawaida huonyesha mashamba na misitu iliyonyunyiziwa maji vizuri. Lakini je, ulijua kwamba nchini Poland pia kuna maeneo ya kustaajabisha yenye marundo mengi ya mchanga mweupe ambao huonekana hata kutoka angani? Eneo hilo kavu lenye ukubwa wa kilometa 18 katika Pwani ya Bahari ya Baltiki ni mojawapo ya mandhari zenye kupendeza zaidi katika Mbuga ya Kitaifa ya Słowiński.

Kichapo fulani cha serikali kinasema kwamba eneo hilo lina “bahari, maziwa, mito, marundo ya mchanga, misitu, udongo, na mashamba yenye nyasi ambayo hufanya lipendeze sana. . . . Ni katika eneo hilo tu ambapo marundo ya mchanga yanapakana na maziwa na misitu.” Kwa kweli marundo ya mchanga, yanayoitwa mchanga mweupe au vilima vyeupe, na maziwa yasiyo na kina kirefu hufanya eneo hilo kuwa la kipekee barani Ulaya.

Marundo hayo makubwa ya mchanga mweupe na manjano ndiyo makubwa zaidi barani Ulaya na yako kwenye eneo kame la ekari 1,200 hivi. Kwa kufaa, nembo ya Mbuga ya Kitaifa ya Słowiński ni korongo mweupe anayepaa juu ya marundo ya manjano na maji ya buluu.

Pia kuna marundo mengi zaidi ya kijivu mbugani lakini hayapendezi sana. Yamekuwapo kwa muda mrefu kuliko marundo meupe, hivyo nyasi na miti imekua na kufanyiza udongo, na vilevile kuimarisha mchanga na kuulinda usipeperushwe. Rundo moja la kijivu ni refu zaidi kuliko mengine katika mbuga hiyo, nalo linaitwa Czołpino na lina urefu wa meta 55 hivi.

Wageni wanapoyaona marundo ya mchanga hasa marundo mengi meupe yanayosonga, kwa kawaida wao huuliza, “Mchanga huu wote ulitoka wapi? Na kwa nini ulijikusanya katika eneo hilo dogo la Pwani ya Baltiki?”

Jinsi Mchanga Ulivyofanyizwa

Ingawa watafiti hawawezi kujibu maswali hayo kikamilifu, uthibitisho unaonyesha kwamba wanadamu walihusika. Wanasayansi wamefikia mkataa huo kwa kuchunguza chavua zilizo kwenye matabaka mbalimbali ya udongo katika mbuga hiyo. Uchunguzi wao umefunua kwamba eneo ambalo leo lina marundo ya mchanga lilikuwa na miti mingi, hasa mialoni. Basi miti hiyo ilienda wapi?

Inaaminiwa kwamba kabla ya Wakati wetu wa Kawaida, misitu mikubwa ya pwani iliteketezwa na mioto iliyowashwa na makabila yaliyoishi katika eneo hilo. Kitabu Słowiński National Park kinasema hivi: “Mchanga ambao ulikuwa umeshikiliwa na misitu, ulianza kupeperushwa kwa mara ya kwanza.” Hata hivyo, kulingana na uchunguzi wa chavua, miti ilimea tena, kwanza aina fulani ya mifune kisha misonobari.

Katika Zama za Kati, mchanga ulianza kusonga tena kwa sababu zisizojulikana. Katika karne ya 16 hata karibu ufunike mji wa kale wa Łeba. Wakazi wa mji huo walijenga mji mwingine mbali na eneo hilo hatari, lakini jitihada zao zilifanya hali ziwe mbaya hata zaidi. Kitabu Słowiński National Park kinasema hivi: “Walihitaji kukata miti mingi ili wajenge mji na bandari na inaonekana hakuna mtu aliyetambua kwamba kukata miti hiyo kungetokeza madhara.” Kitabu hicho kinasema kwamba ukataji huo “ulifanya mchanga usonge isivyo kawaida.” Mchanga ulisonga umbali wa meta 3 mpaka 10 kila mwaka, na kufunika kijiji, mashamba, na hata misitu.

Mchanga Ulitoka Wapi?

Ingawa wanadamu walikata miti na hivyo kubadili mazingira, hawakuleta mchanga huo. Basi mchanga ulitoka wapi? Je, bado mchanga zaidi unajikusanya? Majibu ya maswali hayo yanaweza kutusaidia kujua jinsi mbuga hiyo itakavyokuwa wakati ujao.

Watafiti wanaamini kwamba mito ilihamisha sehemu ya mchanga huo kutoka nchi kavu hadi baharini. Huenda pia ulifanyizwa na mawimbi yanayomomonyoa miamba ya pwani. Kwa mfano, kwenye pwani moja katika Bahari ya Baltiki, mawimbi hugonga miamba ya pwani kwa njia fulani na kuyamomonyoa polepole, hivyo kufanyiza mchanga. Hatimaye mchanga huo hujikusanya kwenye sakafu ya bahari.

Mikondo na mawimbi ya bahari hubeba baadhi ya mchanga huo kutoka sakafu ya bahari mpaka pwani ya mbuga hiyo, ambapo hufanyiza marundo yaliyopangwa sambamba na ufuo. Baadaye jua hukausha mchanga huo na upepo huupeperusha katika nchi kavu. Kisha mchanga huo hujikusanya na kuongezeka na kufanyiza marundo meupe.

Maziwa “Jangwani”

Licha ya kuwa na mchanga mwingi, Mbuga ya Kitaifa ya Słowiński si jangwa lisilo na uhai. Badala yake, ina mimea, wanyama na maji mengi. Ama kweli, marundo ya mchanga na fuo huwa asilimia 5 hivi ya eneo la mbuga, huku mito, maziwa, na vijito vikifanyiza karibu asilimia 55.

Ziwa kubwa kabisa ni Ziwa Łebsko, ambalo lina ukubwa wa kilometa 71 za mraba na kina cha meta 6 hivi. Mto Łeba ndio mto mkubwa zaidi unaotiririka kwenye ziwa hilo. Ziwa la pili kwa ukubwa ni Ziwa Gardno, na Mto Łupawa huingia ndani ya ziwa hilo. Kwa sababu mchanga husongasonga, fuo za maziwa hayo mawili hubadilika daima.

Hifadhi ya Mimea na Wanyama

Zaidi ya sehemu tatu kuu za mbuga hiyo, yaani, marundo ya mchanga, nyika, na msitu wa misonobari, kuna maziwa, mito, na vijito. Katika mazingira hayo kuna karibu aina 900 za mimea yenye utomvu kutia ndani okidi. Mojawapo ya mimea inayoweza kustahimili na inayofaidi mazingira ni nyasi iitwayo European beach au marram. Kwa kawaida, nyasi hiyo ndiyo huwa ya kwanza kumea kwenye mchanga huo. Mashina yake yanayokua chini ya ardhi huenea kwa meta 13 na hutoa machipukizi mengi. Kwa njia hiyo nyasi hiyo huimarisha marundo ya mchanga, hivyo kuruhusu mimea mingine iote na kukua.

Mbuga ya Kitaifa ya Słowiński huwa na ndege wengi kwa kuwa wao hupitia eneo hilo wanapohama. Karibu aina 260 za ndege, ambao ni asilimia 70 hivi ya aina za ndege wanaopatikana nchini Poland, huishi katika mbuga hiyo au hutua kwa muda wanapohama. Ndege wanaoishi majini hutia ndani shakwe mwenye kichwa cheusi, membe, kibisi, na bata wanaotambuliwa kwa urahisi kwa sababu ya manyoya yao yaliyo kichwani. Pia kuna bundi, aina mbalimbali za tai, na kunguru. Ukitembea polepole na ukiwa makini, unaweza pia kuona baadhi ya wanyama wa mbuga hiyo kama vile mbawala mwekundu, paa mdogo mwenye pembe fupi, nguruwe-mwitu, sungura, na wanyama wengine wanaofanana na mbweha.

Mahali Pazuri pa Kutembea

Watalii wanaruhusiwa tu kutembea. Hivyo, mbuga hiyo ina njia za kutembelea za kilometa 140 ambazo zinaelekeza kwenye sehemu mbalimbali za mbuga, kama vile misitu; marundo ya kijivu ya mchanga, mashamba, nyika, na mabwawa; maziwa yenye majukwaa na minara ya kutazama mandhari; marundo meupe ya mchanga, marundo yaliyo karibu na maji; na fuo kubwa zenye mchanga mweupe.

Watu wanaotembelea maeneo hayo wakati wa kupukutika kwa majani au wa baridi kali wanaweza kuona marundo yakipeperushwa na upepo kama mawimbi ya bahari. Watu husema kwamba yanatoa moshi. Chembe nyingi sana za mchanga pia hugongana na kutoa sauti zinapopeperushwa kwa kasi.

Watu 800,000 hutembelea mbuga hiyo kila mwaka ili kutazama mandhari zake nyingi zenye kupendeza sana. Basi, si ajabu kwamba wageni wengi wasiopenda hekaheka za jijini, huja kutafuta utulivu kwenye misitu iliyojitenga, sauti ya mawimbi matulivu ya bahari, na mlio wa shakwe mpweke.

[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 19]

Mbuga ya Kitaifa ya Słowiński

Mbuga hiyo iko katika pwani ya kati ya Poland katikati ya miji ya Łeba na Rowy. Inaitwa kwa jina la kabila la Kashubi la Słowińcy, ambao ni Waslavi walioishi katika eneo hilo kabla tu ya Vita vya Pili vya Ulimwengu kumalizika. Mbuga hiyo ilifunguliwa mwaka wa 1967 na katika mwaka wa 1977 ikaorodheshwa kuwa Hifadhi ya Maumbile ya Ulimwengu. Ina ukubwa wa ekari 45,985 na zaidi ya nusu yake ina maji. Sehemu nyingine ya mbuga hiyo ni misitu (asilimia 25), fuo na marundo ya mchanga (asilimia 5), mabwawa na nyika (asilimia 8), na mashamba na sehemu za malisho (asilimia 8).

[Ramani]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BAHARI YA BALTIKI

URUSI

POLAND

MBUGA YA KITAIFA YA SŁOWIŃSKI

UJERUMANI

JAMHURI YA CHEKI

SLOVAKIA

[Picha katika ukurasa wa 16]

Inasemekana kwamba marundo ya mchanga hutoa moshi wakati pepo kali za majira ya baridi kali zinapopeperusha mchanga

[Picha katika ukurasa wa 17]

Membe

[Hisani]

Photo by Chukchi Imuruk, National Park Service ▸

[Picha katika ukurasa wa 17]

Marundo ya mchanga wakati wa kiangazi

[Picha katika ukurasa wa 17]

Marundo ya mchanga wakati wa baridi kali

[Picha katika ukurasa wa 18]

Ziwa Łebsko

[Picha katika ukurasa wa 18]

Nyasi ya “European beach”

[Picha katika ukurasa wa 18]

Paa mdogo

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mchanga uliofanyizwa kwa njia ya pekee

[Picha katika ukurasa wa 18]

Aina ya bata