Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wamegundua Nini Huko Yezreeli?

Wamegundua Nini Huko Yezreeli?

Wamegundua Nini Huko Yezreeli?

KWA karne nyingi, eneo la mji wa kale wa Yezreeli limekuwa ukiwa. Wakati fulani mji huo ulikuwa mashuhuri katika historia ya Biblia. Sasa, ukiwa umeondolewa utukufu wake wa awali na kufunikwa chini ya udongo, umebaki kuwa kilima, au tuta. Katika miaka ya majuzi, waakiolojia wameanza kuchunguza magofu ya Yezreeli. Magofu hayo yafunua nini kuhusu masimulizi ya Biblia?

Yezreeli Katika Biblia

Yezreeli, uliokuwa sehemu ya mashariki ya Bonde la Yezreeli, ulikuwa katika mojawapo ya sehemu zenye rutuba zaidi za nchi ya Israeli ya kale. Ng’ambo ya bonde upande wa kaskazini pana mlima wa More ambapo Wamidiani walipiga kambi wakijitayarisha kushambulia Mwamuzi Gideoni na vikosi vya wanajeshi wake. Kitambo kidogo upande wa mashariki pana kisima cha Harodi, chini ya Mlima Gilboa. Hapo ndipo Yehova alipopunguza jeshi la Gideoni kutoka maelfu hadi kuwa watu 300 tu ili kuonyesha uwezo wake wa kukomboa watu wake pasipo kutumia jeshi kubwa. (Waamuzi 7:1-25; Zekaria 4:6) Kwenye Mlima Gilboa ulio karibu na hapo, Sauli, mfalme wa kwanza wa Israeli, alishindwa na Wafilisti katika pigano lenye kutazamisha, ambapo Yonathani na wana wengine wawili wa Sauli waliuawa na Sauli mwenyewe akajiua.—1 Samweli 31:1-5.

Mitajo ya Biblia inayohusu mji wa kale wa Yezreeli ina matukio yanayotofautiana sana. Mitajo hiyo husema kuhusu watawala wa Israeli walivyotumia mamlaka vibaya na uasi wao, na kuhusu uaminifu na bidii ya watumishi wa Yehova. Yezreeli ndipo mahali Mfalme Ahabu—mtawala wa ufalme wa kaskazini wa Israeli wa makabila kumi mwishoni mwa karne ya kumi K.W.K.—alipojenga makao yake ya kifalme, ingawa mji mkuu rasmi ulikuwa Samaria. (1 Wafalme 21:1) Yezreeli ndipo mahali Yezebeli, mke wa Ahabu wa kutoka nchi ya kigeni, alipotishia kumwua Eliya nabii wa Yehova. Mke huyo alikasirika kwa sababu Eliya alikuwa amewaua manabii wa Baali pasipo woga, baada ya mtihani wa kumtambua Mungu wa kweli ambao Eliya aliufanya kwenye Mlima Karmeli.—1 Wafalme 18:36–19:2.

Kisha uhalifu fulani ukatendwa hapo Yezreeli. Nabothi Myezreeli aliuawa kimakusudi. Mfalme Ahabu alikuwa amelitamani shamba la mizabibu la Nabothi. Mfalme huyo alipotaka shamba hilo kwa nguvu, Nabothi aliitikia kwa uaminifu-mshikamanifu hivi: “BWANA anizuize, nisikupe uriti wa baba zangu.” Jibu hilo lenye msimamo imara lilimkasirisha sana Ahabu. Malkia Yezebeli alipoona moyo mzito wa mfalme, alipanga mahakama isiyo halali, akamshtaki Nabothi kuwa amekufuru. Nabothi asiye na hatia alipatikana na hatia na kupigwa kwa mawe hadi akafa, kisha mfalme akatwaa shamba lake la mizabibu.—1 Wafalme 21:1-16, linganisha Zaire Swahili Bible.

Kwa sababu ya kitendo hicho kiovu, Eliya alitabiri hivi: “Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli.” Kisha nabii huyo akasema hivi tena: “Mtu wa nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla . . . Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa BWANA ambaye Yezebeli mkewe alimchochea.” Hata hivyo, kwa sababu Ahabu alijinyenyekeza Eliya alipotangaza hukumu ya Yehova, Yehova alisema kwamba adhabu hiyo haingetekelezwa Ahabu akiwa hai. (1 Wafalme 21:23-29) Masimulizi ya Biblia yaendelea kusema kuwa katika siku za Elisha, mwandamizi wa Eliya, Yehu alitiwa mafuta awe mfalme wa Israeli. Aliposonga kuingia Yezreeli, Yehu aliamuru kwamba Yezebeli atupwe nje ya dirisha la jumba lake la kifalme, na farasi wakamkanyaga-kanyaga. Baadaye, ikapatikana kwamba mbwa walimla na kusaza tu fuvu lake la kichwa, miguu yake, na vitanga vya mikono yake. (2 Wafalme 9:30-37) Tukio la mwisho la Kibiblia linalohusiana moja kwa moja na Yezreeli ni kuuawa kwa wana 70 wa Ahabu. Yehu alivikusanya vichwa vyao kwa machungu makubwa mawili penye lango la mji wa Yezreeli, kisha akawaua wakuu wengine na makuhani waliohusika katika utawala wa uasi wa Ahabu.—2 Wafalme 10:6-11.

Waakiolojia Wamegundua Nini?

Mwaka wa 1990, mradi wa pamoja wa kuchimbua eneo la Yezreeli ulianzishwa. Taasisi ya Akiolojia ya Chuo Kikuu cha Tel Aviv (iliyowakilishwa na David Ussishkin) na Shule ya Akiolojia ya Uingereza katika Yerusalemu (iliyowakilishwa na John Woodhead) zilishiriki katika mradi huo. Kwa misimu saba (kila msimu ukiwa majuma sita) katika miaka ya 1990-1996, kati ya wajitoleaji 80 na 100 walifanya kazi katika eneo hilo.

Mbinu ya kisasa ya akiolojia ni kuchunguza uthibitisho katika eneo fulani kwa kutegemea ustahili wake tu, pasipo kutegemea mawazo na dhana zilizokwisha amuliwa. Basi, kwa mwakiolojia anayechunguza nchi za Biblia, masimulizi ya Kimaandiko siyo mamlaka ya mwisho juu ya habari hiyo. Vyanzo vingine vyote na uthibitisho unaoonekana lazima vichunguzwe na kuchanganuliwa kwa makini. Hata hivyo, kama John Woodhead aelezavyo, hakuna uthibitisho wowote wa kale ulioandikwa kuhusu Yezreeli mbali na sura chache katika Biblia. Kwa hiyo, masimulizi na miaka na matukio ya Biblia sharti yawe sehemu ya uchunguzi wowote ule. Jitihada za waakiolojia zimefunua nini?

Ngome na vyombo vya udongo vilipofukuliwa, ikawa wazi tangu mwanzoni kwamba magofu hayo ni ya wakati uitwao Enzi ya Chuma, yakiyaweka barabara katika kipindi cha wakati cha Yezreeli katika Biblia. Lakini uchimbuaji ulipoendelea, kulitokea mambo kadhaa ya kushangaza. La kwanza lilikuwa ukubwa wa eneo hilo na ngome zake kubwa mno. Waakiolojia hao walikuwa wakitarajia kupata eneo lenye ngome kama zile za Samaria ya kale, mji mkuu wa ufalme wa Israeli. Hata hivyo, walipozidi kuchimba, ikawa wazi kwamba Yezreeli ulikuwa mkubwa zaidi. Jumla ya eneo ndani ya ngome za mji huo, ambao kuta zake zilikuwa zenye kipimo cha meta 300 kwa 150, lilikuwa lenye ukubwa zaidi ya mara tatu ya mji mwingine wowote wa kipindi hicho uliogunduliwa katika Israeli. Ulizungukwa na handaki lisilo na maji, lenye kina cha meta 11 chini ya ngome hizo. Kwa mujibu wa Profesa Ussishkin, handaki hilo lilikuwa kitu kisicho na kifani katika nyakati za Biblia. “Hakuna kitu kingine chochote kama hicho katika Israeli hadi kipindi cha Krusedi,” akasema.

Jambo jingine lisilotarajiwa ni kukosekana kwa majengo mengi katikati ya mji. Udongo mwingi wa rangi nyekundu ulioletwa ndani wakati wa ujenzi wa mji huo ulitumiwa kujenga eneo lililoinuliwa—mfano wa jukwaa lililoinuliwa—katikati ya eneo lililozungukwa. Kichapo kiitwacho Second Preliminary Report kuhusu uchimbuaji huo katika Tel Jezreel chaeleza kuwa jukwaa hilo maarufu laweza kuwa uthibitisho kwamba Yezreeli ulitumiwa kwa makusudi mengine mbali na kuwa makao ya kifalme. Ilisema hivi: “Tungependa kuonyesha kwamba yawezekana Yezreeli ulikuwa kituo kikuu cha kijeshi cha jeshi la kifalme la Israeli wakati wa wafalme wa uzao wa Omri . . . ambapo askari wa magari vita na askari wa farasi wa kifalme waliishi na kuzoezewa.” Kwa kutegemea ukubwa wa jukwaa hilo lililoinuliwa, na vilevile ukubwa wa eneo lenyewe lililozungushwa, Woodhead adokeza kwamba huenda hilo lilikuwa kama uwanja wa gwaride wa kuonyesha nguvu za kijeshi za jeshi kubwa zaidi katika Mashariki ya Kati wakati huo.

Magofu yaliyofukuliwa ya lango la mji huo ni jambo lenye kuwavutia waakiolojia kwa njia maalumu. Magofu hayo yaonyesha kiingilio cha lango lenye angalau vyumba vinne. Ingawa hivyo, kwa kuwa mawe mengi kwenye eneo hilo yamechukuliwa kwa karne nyingi, ugunduzi huo si kamili. Woodhead aonelea kwamba magofu hayo hudokeza lango lenye vyumba sita lenye ukubwa unaofanana na malango yaliyogunduliwa huko Megido, Hazori, na Gezeri. *

Ugunduzi wa kiakiolojia waonyesha kuwa mji huo uliokuwa mahali pazuri sana, kijeshi na kijiografia, ulidumu kwa kipindi kifupi mno. Woodhead asisitiza kuwa Yezreeli, mji mkubwa wenye ngome, ulidumu kwa muda mfupi tu—ulitumiwa kwa miongo michache tu ya miaka. Eneo hilo ni tofauti kabisa na maeneo mengine muhimu ya Kibiblia katika Israeli, kama vile Megido, Hazori, na mji mkuu Samaria, ambayo yalijengwa upya mara nyingi, yakapanuliwa, na kukaliwa katika vipindi mbalimbali. Kwa nini eneo hilo lenye kufaa lilikoma kutumiwa haraka hivyo? Woodhead adokeza kuwa Ahabu na nasaba yake ya wafalme karibu asababishe kuanguka kwa uchumi kwa sababu ya kutumia kiholela rasilimali za taifa hilo. Hilo lilionekana wazi katika ukubwa wenye kupita kiasi na nguvu za Yezreeli. Labda utawala huo mpya wa Yehu haukutaka kuhusianishwa na aliyofanya Ahabu na kwa hiyo ukahama mji huo.

Uthibitisho wote uliofukuliwa hadi sasa wathibitisha kuwa eneo la Yezreeli lilikuwa kituo muhimu cha Israeli katika kipindi cha Enzi ya Chuma. Ukubwa na ngome zake zapatana na maelezo ya Biblia yanayoonyesha kuwa mji huo ulikuwa makao mashuhuri ya kifalme kwa Ahabu na Yezebeli. Ishara zinazoonyesha kwamba mji huo ulikaliwa kwa muda mfupi zaafikiana na masimulizi ya Biblia kuuhusu: Ulipata kuwa mashuhuri haraka wakati wa utawala wa Ahabu kisha, kwa amri ya Yehova, yaonekana ukaharibiwa kwa aibu Yehu ‘alipowapiga wote waliosalia wa nyumba ya Ahabu katika Yezreeli, na hao wakuu wake wote, na rafiki zake, na makuhani wake, hata hakumwachia aliyesalia hata mmoja.’—2 Wafalme 10:11.

Miaka na Matukio Katika Yezreeli

“Ni vigumu sana katika akiolojia kupata msingi sahihi wa kupima tarehe,” akiri John Woodhead. Basi waakiolojia wachunguzapo matokeo ya uchimbuaji wa miaka saba, wao hulinganisha ugunduzi huo na ugunduzi katika maeneo mengine ya kiakiolojia. Hayo yamesababisha uchanganuzi mpya na mjadala. Kwa nini? Kwa sababu tangu uchimbuaji wa mwakiolojia Mwisraeli Yigael Yadin huko Megido miaka ya 1960 na mapema miaka ya 1970, waakiolojia wengi walifikiri kuwa imethibitishwa kwamba amegundua ngome na malango ya mji ambazo ni za tangu wakati wa Mfalme Solomoni. Sasa, ngome, vyombo vya udongo, na malango yaliyogunduliwa huko Yezreeli zinasababisha watu fulani kutilia shaka maamuzi hayo.

Kwa kielelezo, vyombo vya udongo vilivyopatikana huko Yezreeli vyafanana na vile vilivyoko Megido ambavyo Yadin alivihusianisha na utawala wa Solomoni. Muundo wa malango na vipimo vya maeneo hayo mawili vyafanana, au vyalingana. Woodhead asema hivi: “Uthibitisho wote huweka eneo la Yezreeli katika kipindi cha Solomoni au hupunguza tarehe ya vitu hivyo katika maeneo yale mengine [Megido na Hazori] hadi kipindi cha Ahabu.” Kwa kuwa Biblia yahusianisha waziwazi eneo la Yezreeli na kipindi cha Ahabu, Woodhead aonelea kuwa ni jambo la busara zaidi kukubali kwamba vyombo hivyo huonyesha kipindi cha utawala wa Ahabu. David Ussishkin akubaliana naye: “Biblia yasema kuwa Solomoni alijenga Megido—haisemi kuwa alijenga malango hayo hususa.”

Je, Historia ya Yezreeli Yaweza Kujulikana?

Je, ugunduzi huo wa kiakiolojia na mjadala unaofuatia hutilia shaka masimulizi ya Biblia kuhusu Yezreeli au Solomoni? Kwa kweli, mabishano ya kiakiolojia hayaathiri sana masimulizi ya Biblia. Akiolojia huchunguza historia kwa msingi unaotofautiana na masimulizi ya Biblia. Hiyo hutokeza maswali tofauti na hukazia mambo tofauti. Mwanafunzi wa Biblia na mwakiolojia waweza kulinganishwa na wasafiri walio kwenye njia zinazokaribia kuwa sambamba. Msafiri mmoja aendesha gari barabarani, na mwingine atembea kwenye kijia cha kando. Mambo wanayokazia fikira na malengo yao ni tofauti. Ingawa hivyo, mara nyingi maoni yao hukamilishana badala ya kupingana. Kulinganisha maoni ya wasafiri hao wawili huleta taswira zenye kuvutia.

Biblia ina rekodi iliyoandikwa juu ya matukio na watu wa kale; akiolojia hujaribu kupata habari kuhusu matukio na watu hao kwa kuchunguza mabaki yoyote yale juu ya vitu hivyo ambavyo vingali udongoni. Hata hivyo, mara nyingi mabaki hayo si kamili nayo yaweza kufasiriwa kwa njia mbalimbali. Kwa hiyo, katika kitabu chake cha Archaeology of the Land of the Bible—10,000−586 B.C.E., Amihai Mazar aeleza hivi: “Kazi ya akiolojia . . . hasa ni sanaa na vilevile mchanganyiko wa mazoezi na ustadi wa kitaalamu. Hakuna mbinu yoyote maalumu iwezayo kuhakikisha mafanikio, na ni lazima wakurugenzi wawe wenye kubadilikana na wabunifu. Tabia, kipawa, na maarifa ya kawaida ya mwakiolojia ni muhimu kama vile mazoezi na rasilimali alizo nazo.”

Akiolojia imethibitisha kuwepo kwa kituo muhimu cha kifalme na kijeshi huko Yezreeli, kituo kilichodumu kwa muda mfupi sana katika kipindi cha kihistoria kinacholingana na utawala wa Ahabu—kama vile Biblia inavyosimulia. Maswali mengine mengi yanayotatanisha ambayo huenda waakiolojia watayachunguza kwa miaka kadhaa ijayo yamezushwa. Ingawa hivyo, Neno la Mungu, Biblia, laendelea kusema waziwazi, likituandalia masimulizi kamili kwa njia ambayo waakiolojia hawawezi kumudu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Ona makala ya “Lile Fumbo la Malango” katika Mnara wa Mlinzi la Agosti 15, 1988.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Uchimbuaji wa kiakiolojia katika Yezreeli

[Picha katika ukurasa wa 28]

Sanamu ya Wakanaani iliyopatikana huko Yezreeli