Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Visababishi na Hatari za Jongo

Visababishi na Hatari za Jongo

Visababishi na Hatari za Jongo

JONGO ni moja kati ya aina za yabisi-kavu ambazo huwaathiri watu wengi na inaweza kusababisha maumivu makali. “Jongo hutokezwa wakati ambapo mwili unashindwa kuvunja-vunja asidi ya yurea,” kinasema kitabu Arthritis. Zaidi ya hayo, jongo “ni ugonjwa ambao chanzo chake kinatambuliwa waziwazi​—kuwepo kwa chembechembe za asidi ya yurea kwenye umajimaji unaofunika vifundo . . . , na hasa kwenye kidole kikubwa cha mguu.

Asidi ya yurea ni takataka zinazopatikana kwenye damu, nazo hutokezwa wakati ambapo vitu vinavyoitwa purini vinapovunjwa-vunjwa. Kwa kawaida, asidi ya yurea huongezeka sana inaposhindwa kutoka kwa njia ya mkojo, na kwa sababu hiyo chembechembe zenye umbo kama la sindano zinaweza kurundamana kwenye kifundo cha kidole kikubwa cha mguu, ingawa huenda zikarundamana pia kwenye vifundo vingine. Huenda kifundo hicho kikaanza kuwasha na kuvimba, kikawa moto unapokigusa, na kutokeza maumivu makali sana. * Alfred ambaye anasumbuliwa na ugonjwa huo anasema kwamba “hata kukigusa kidogo tu kunasababisha maumivu makali kupita kiasi.”

“Bila matibabu, kwa kawaida ugonjwa wa jongo unaendelea kwa muda wa juma moja hivi,” inasema ripoti moja iliyochapishwa na Arthritis Australia. “Huenda mtu asipatwe na ugonjwa huo kwa miezi mingi au hata miaka. Ugonjwa huo usipotibiwa kwa njia inayofaa, unaweza kurudi baada ya muda mfupi zaidi, na [huenda ukawa] mbaya zaidi na vifundo vinaweza kuharibika kabisa. Wakati mwingine ugonjwa wa jongo unaweza kufikia hatua ya kuwa ugonjwa wa kudumu.”

Jongo ni moja kati ya aina za yabisi-kavu inayoweza kutibiwa kwa urahisi. Kwa kawaida, matibabu yanahusisha kutumia dawa za kutibu uvimbe zisizo na steroidi au, ugonjwa huo unapotokea mara nyingi au maumivu yanapokuwa makali, mtu hupewa dawa za allopurinol, ambazo zinasaidia kuzuia kutokezwa kwa asidi ya yurea. Je, inawezekana kuzuia ugonjwa wa jongo usitokee tena? Inawezekana, ikiwa mtu anayeugua anajua visababishi vyake.

Mambo Yanayoweza Kufanya Jongo Itokee Tena

Mambo yanayoweza kufanya jongo itokee tena ni umri, jinsia, na chembe za urithi. Kulingana na wataalamu fulani, zaidi ya asilimia 50 ya watu wanaougua jongo ni wale ambao watu wao wa ukoo waliwahi kuugua ugonjwa huo. Alfred aliyenukuliwa hapo awali anasema: “Baba yangu na babu yangu walikuwa na ugonjwa wa jongo.” Isitoshe, jongo huwaathiri wanaume zaidi, na hasa wale walio na umri wa kati ya miaka 40 na 50. Kwa kweli, wanaume wanapata ugonjwa huo mara tatu au nne zaidi kuliko wanawake, ambao si rahisi kupatwa na ugonjwa huo kabla ya kukoma hedhi.

Kunenepa kupita kiasi na aina ya vyakula: Kitabu Encyclopedia of Human Nutrition kinasema hivi: “Siku hizi ugonjwa wa jongo haudhibitiwi hasa kwa kuepuka tu vyakula vilivyo na purini nyingi, bali pia kwa kutibu matatizo ya umeng’enyaji yanayohusianishwa na jongo kama vile: kunenepa kupita kiasi, tatizo la kukosa kutokeza insulini, na dyslipidemia,” au kuweko kwa viwango vya juu vya shahamu kwenye damu, kama vile kolesteroli.

Hata hivyo, wataalamu fulani hupendekeza kupunguza vyakula vyenye purini nyingi kama vile, hamira, aina fulani ya samaki, na aina mbalimbali za nyama nyekundu. *

Kileo: Kutumia kileo kupita kiasi kunaweza kufanya iwe vigumu kwa mwili wako kuondoa asidi ya yurea, na hivyo kuifanya irundamane.

Matatizo ya afya: Kulingana na Kliniki ya Mayo, huko Marekani, jongo inaweza kusababishwa na matatizo fulani ya afya, kutia ndani “kutotibu kupanda kwa shinikizo la damu (hypertension) na matatizo sugu kama vile kisukari, viwango vya juu vya mafuta na kolesteroli kwenye damu (hyperlipidemia), na ateri kuanza kuwa nyembamba (arteriosclerosis).” Pia jongo inahusianishwa na “ugonjwa au majeraha mabaya yanayoweza kumpata mtu ghafla, na mwili kulegea kwa sababu kulala kwa muda mrefu,” na pia ugonjwa wa figo. Kwa kweli, kidole kikubwa cha mguu ndicho huathiriwa mara kwa mara na jongo kwa sababu ni kiasi kidogo cha damu kinachofika humo na kina kiwango cha chini cha joto, na mambo hayo mawili ndiyo yanayoweza kuchochea kuongezeka kwa asidi ya yurea.

Dawa: Dawa ambazo zinaweza kuongeza hatari ya kupata jongo zinatia ndani zile zinazoitwa thiazide diuretics (dawa za kuondoa maji mwilini ambazo kwa kawaida zinatumiwa kutibu kupanda kwa shinikizo la damu) kiwango kidogo cha aspirini, dawa anazotumia mgonjwa aliyepandikizwa viungo vya mwili, na dawa za kutibu kansa.

Mambo Matano Yanayoweza Kuzuia Jongo Isitokee Tena

Kwa sababu jongo imehusianishwa na mtindo wa maisha, madokezo yafuatayo huenda yakawasaidia watu kupunguza uwezekano wa jongo kutokea tena. *

1. Kwa sababu jongo ni ugonjwa unaotokea mwili unaposhindwa kumeng’enya madini, wagonjwa wanapaswa kujitahidi kudumisha uzito unaofaa kwa kupunguza kiasi cha kalori wanachokula. Isitoshe, kunenepa kupita kiasi kunaongeza uzito kwenye vifundo.

2. Jihadhari na mbinu za kupunguza uzito kwa ghafla, ambazo zinaweza kuongeza kiasi cha asidi ya yurea katika damu.

3. Epuka kula kiasi kikubwa cha protini inayotokana na wanyama. Watu fulani hupendekeza mtu ale gramu 170 hivi kila siku za nyama isiyo na mafuta mengi, kama vile nyama ya kuku na samaki.

4. Ikiwa wewe hunywa kileo, fanya hivyo kwa kiasi. Unapopatwa na jongo, huenda likawa jambo la busara kuepuka kabisa kunywa kileo.

5. Kunywa kiasi kikubwa cha vinywaji visivyo na kileo. Hilo linasaidia kuyeyusha na kuondoa asidi ya yurea mwilini. *

Hatua za kuzuia jongo zilizotajwa hapo juu huenda zikatukumbusha amri ya Biblia kwamba tuwe wenye “kiasi katika mazoea” na tusinywe “divai nyingi.” (1 Timotheo 3:​2, 8, 11) Kwa hakika Muumba wetu mwenye upendo anajua mambo yanayotufaa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Dalili kama hizo huenda zikatokea wakati chembechembe za kalisi aina ya pyrophosphate zinaporundamana kwenye vifundo, na hasa ndani ya gegedu laini kwenye miisho ya mifupa. Hata hivyo, ugonjwa huo unaoitwa “pseudogout” ni tofauti ingawa unafanana na jongo na huenda ukahitaji matibabu tofauti.

^ fu. 9 Kulingana na makala iliyochapishwa katika jarida Australian Doctor, “hakuna uthibitisho unaoonyesha kuwa mtu anaweza kupatwa na ugonjwa wa jongo” kwa kula uyoga na mboga zilizo na purini nyingi, kama vile maharagwe, dengu, njegere, spinachi, na koliflawa.

^ fu. 14 Makala hii haijakusudiwa kutoa mwongozo wa kitiba. Huenda kila mgonjwa akahitaji matibabu yanayomfaa yeye. Pia, hapaswi kuacha kutumia dawa alizoelekezwa au kubadili chakula chake bila kuwasiliana na daktari.

^ fu. 19 Habari hii inategemea madokezo yaliyotolewa na Taasisi ya Mayo ya Elimu na Utafiti wa Kitiba.

[Mchoro/​Picha katika ukurasa wa 24]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kiungo kilichovimba

Umajimaji kwenye kifundo

[Picha]

Chembechembe za asidi ya yurea zilizorundamana