Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Katika Jamhuri ya Georgia huko kusini-mashariki mwa Ulaya, “idadi ya talaka imeongezeka karibu maradufu katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.” Wengi wa wanaotalikiana wako chini ya umri wa miaka 20.​—FINANCIAL, GEORGIA.

Huko Ireland, asilimia 17 ya vijana wenye umri wa miaka 11 hadi 16 “wametoa jina lao kamili kwa mtu fulani wasiyemfahamu kwenye Intaneti.” Asilimia kumi pia wametoa “anwani ya barua pepe, namba ya simu ya mkononi au picha.”​—SHIRIKA LA KUZUIA UKATILI DHIDI YA WATOTO LA IRELAND.

Ni asilimia 4 hivi ya mioto ya msituni inayosababishwa na hali za kiasili. Mioto mingine yote husababishwa na watu​—iwe ni kwa kutojali au kimakusudi.​—PRESSEPORTAL, UJERUMANI.

“Karibu asilimia 10 ya Wamarekani [wenye umri wa miaka 12 na zaidi] wamekiri kwamba wao hutumia dawa za kulevya, kutia ndani bangi, kokeini, heroini, dawa za kupumbaza akili, dawa za kunusa au za kitiba ambazo watu hutumia kujiburudisha.”​—USA TODAY, MAREKANI.

Kujidhibiti Ni Siri ya Kuwa Imara

“Utafiti unadokeza kwamba kukosa kujidhibiti wakati mtu anapokuwa kijana kunaweza kuwa ishara ya kwamba atakuwa na matatizo ya afya, ya fedha na kuwa mhalifu atakapokuwa mtu mzima,” linasema gazeti Time. Zaidi ya watu 1,000 walichunguzwa tangu walipozaliwa hadi walipofikia umri wa miaka 32. Kufikia wakati walipokuwa watu wazima, “wale ambao [utotoni] walikuwa na tatizo la kufanya mambo bila kufikiri na kukata tamaa upesi na hawakuwa na subira au hawangeweza kungojea zamu yao kupata wanachotaka” walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na afya mbaya, kuwa na mapato ya hali ya chini, kuwa wazazi wasio na mwenzi, au kujihusisha katika uhalifu. Na bado, “kujidhibiti ni jambo ambalo mtu anaweza kujifunza,” linasema gazeti hilo, na linaongezea hivi: “Shule na familia zinazojitahidi kuwafundisha watoto wasitawishe sifa ya kujizuia tangu utotoni huwasaidia wawe watu wazima wenye afya nzuri na walio imara.”

Kuwafundisha Adabu Madereva Watundu

Mamlaka nchini India zinajaribu njia mpya za kushughulika na wakiukaji wakubwa wa sheria za barabarani kwa kuwafanyisha kazi ya polisi wa barabarani. Lengo hasa ni kuwasaidia madereva kuelewa ugumu wa kazi ya kutatua vurugu wanazosababisha barabarani. Mbali na kuwakamata wakosaji na kuwatoza faini, sasa polisi katika jiji la Gurgaon, lililo kaskazini-magharibi mwa India, wanawashurutisha madereva hao wajiunge na polisi katika kuelekeza magari kwa nusu saa au zaidi. Madereva fulani wanakiri kwamba somo hilo limebadili mtazamo wao. “Tunatoza [faini] elfu moja kila siku kwa ukiukaji wa sheria za barabarani hapa Gurgaon,” anasema Bharti Arora, naibu wa kamishna wa polisi wa eneo hilo. “Lakini badala ya kufanya hivyo, tungeweza kuwa na ‘polisi’ 1000 wa ziada kila siku.”