Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Maji Yanakwisha?

Je, Maji Yanakwisha?

Je, Maji Yanakwisha?

Msemo mmoja wa Kiuzbeki unasema kwamba “ukiishiwa na maji, maisha yako yanakwisha.” Wataalamu fulani wanasema kwamba msemo huo ulitabiri mambo yanayotokea sasa. Kila mwaka karibu watu milioni mbili wanakufa kwa sababu hakuna mifumo mizuri ya kuondoa maji-taka na kwa sababu ya kunywa maji yaliyochafuliwa, na asilimia 90 ya wale wanaoathiriwa ni watoto.

WEWE unapata maji yako jinsi gani? Je, unafungulia tu bomba na yanatiririka? Au, kama ilivyo katika nchi fulani, je, unahitaji kutembea mbali sana, kupanga laini, na kisha kubeba ndoo nzito iliyojaa maji hayo yenye thamani hadi nyumbani? Je, unahitaji kutumia saa kadhaa kila siku ili tu kupata maji ya kutosha kufanya usafi na kupika? Katika nchi nyingi, maji hayapatikani kwa urahisi na si mengi! Katika kitabu chake kuhusu jitihada za ulimwengu za kutatua matatizo ya maji (Water Wars—Drought, Flood, Folly, and the Politics of Thirst) Diane Raines Ward anasema kwamba asilimia 40 ya watu ulimwenguni “wanateka maji yao katika visima, mito, au vidimbwi.” Katika nchi fulani, wanawake wanaweza kutumia muda wa saa sita hivi wakiteka maji kwa ajili ya familia zao na kung’ang’ana kuyabeba katika mitungi, ambayo inapojazwa kabisa huwa na uzito wa zaidi ya kilo 20.

Ukweli ni kwamba ni vigumu kwa zaidi ya asilimia 33 ya idadi ya watu ulimwenguni kupata maji safi na pia hawana mfumo wa kuondoa maji-taka. Tatizo ni kubwa hasa barani Afrika, ambako watu 6 kati ya 10 hawana vyoo vizuri, jambo ambalo kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni, linachangia “kuenea kwa bakteria, virusi, na vijidudu vinavyopatikana katika kinyesi na mkojo wa binadamu . . . vinachafua maji, udongo, na vyakula.” Ripoti hiyo inasema kwamba uchafuzi huo “ni chanzo kikuu cha ugonjwa wa kuharisha, ambao ni kisababishi cha pili kikuu cha vifo vya watoto katika nchi zinazoendelea, na uchafuzi huo unachangia kuenea kwa magonjwa mengine makubwa kama vile kipindupindu, kichocho, na ugonjwa wa macho.”

Maji yamekuwa yenye thamani kama dhahabu ama mafuta katika karne ya 21. Hata hivyo, mataifa yanatumia vibaya kitu hicho chenye thamani hivi kwamba ni kiasi kidogo tu cha maji kinachoingia baharini kutoka kwenye mito mikuu ya nchi hizo. Kwa sababu ya uvukizaji na watu kunyunyizia mashamba maji, mito mikubwa inakauka kama vile, Mto Colorado ulio magharibi mwa Marekani, Mto Yangtze huko China, Mto Indus nchini Pakistan, Mto Ganges nchini India, na Mto Nile nchini Misri. Ni hatua gani ambayo imechukuliwa ili kutatua matatizo hayo? Suluhisho kamili ni nini?

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 3]

MAJI YANAKAUKA

▪ “Mnamo 1960, Bahari ya Aral iliyo Asia ya Kati lilikuwa ndilo ziwa la nne kwa ukubwa duniani. Kufikia mwaka wa 2007 ziwa hilo lilikuwa limepungua na kufikia asilimia 10 ya lilivyokuwa awali.”—Scientific American.

▪ Maziwa matano Makubwa ya Marekani na Kanada, yaani, Maziwa Erie, Huron, Michigan, Ontario, na Superior, yanapungua “haraka sana.”—The Globe and Mail.

▪ Wakati fulani, kinu cha Deniliquin huko Australia kilitokeza nafaka ya kutosha kutimiza mahitaji ya watu milioni 20. Hata hivyo, sasa kiwango cha mpunga kimepungua kwa asilimia 98, na kinu hicho kilifungwa Desemba (Mwezi wa 12) 2007. Kwa nini? Kumekuwa na “miaka sita ya ukame.” —The New York Times.

[Picha]

Mashua ikiwa imeachwa kwenye nchi kavu kwenye Bahari ya Aral

[Hisani]

© Marcus Rose/Insight/Panos Pictures

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]

“KUKAUSHA MITO NA VIJITO”

“Ziwa Chad barani Afrika ambalo zamani lilionekana waziwazi na wataalamu wa anga walipokuwa wakiizunguka dunia, sasa halionekani kwa urahisi. Likiwa limezingirwa na nchi ya Chad, [Kamerun,] Niger, na Nigeria . . . , ziwa hilo limepungua kwa asilimia 95 tangu miaka ya 1960. Uhitaji unaoongezeka wa kunyunyizia mashamba maji katika eneo hilo unakausha mito na vijito ambavyo ziwa hilo linategemea. Kwa hiyo, huenda hivi karibuni Ziwa Chad likatoweka kabisa, na lisijulikane na vizazi vijavyo.”—Plan B 2.0—Rescuing a Planet Under Stress and a Civilization in Trouble, cha Lester R. Brown.

[Ramani]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Maji

☒ Mimea

□ Nchi kavu

1963

NIGER

CHAD

Ziwa Chad

NIGERIA

KAMERUN

2007

NIGER

CHAD

Ziwa Chad

NIGERIA

KAMERUN

[Hisani]

NASA/U.S. Geological Survey