Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Watumwa Waliosahauliwa wa Bahari za Kusini

Watumwa Waliosahauliwa wa Bahari za Kusini

 Watumwa Waliosahauliwa wa Bahari za Kusini

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FIJI

UMATI unasisimuka meli mbili zinapoingia kwenye wangwa wa kisiwa fulani cha Pasifiki. Miaka kadhaa mapema, mtu fulani aliyeokoka kuvunjika kwa meli alikuwa ameipa kila familia kurasa chache kutoka kwa Biblia yake iliyoraruka. Maskini hao walisoma kurasa hizo kwa hamu na tangu wakati huo walikuwa wamesubiri mwalimu Mkristo awasili.

Sasa, mabaharia hawa wameahidi kuwapeleka mahali watakapojifunza mengi zaidi kumhusu Mungu. Wanaume na wanawake 250 hivi wanaingia kwenye meli hizo, wengi wao wakiwa wameshika kurasa zao za Biblia walizothamini sana.

Hata hivyo, walikuwa wamedanganywa sana. Mara tu walipopanda meli hizo, walifungwa, wakatupwa kwenye vyumba vya chini, na kupelekwa safari ya mbali hadi kwenye bandari ya Callao huko Amerika Kusini. Njiani watu wengi sana walikufa kwa sababu ya ukosefu wa usafi. Wengi walitendewa vibaya kingono. Waliookoka waliuzwa kuwa watumwa na kufanyishwa kazi katika mashamba na migodi au kuwa watumishi wa nyumbani, na hawakuwahi kurudi nyumbani kwao.

Biashara ya Watumwa Yasitawi Pasifiki Kusini

Wakaaji wa visiwa vya Pasifiki Kusini walitekwa katika karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20. Hilo lilifanya maelfu ya wenyeji wa visiwa hivyo waletwe Amerika Kusini mapema katika miaka ya 1860. Katika miaka kumi iliyofuata, wakazi wa visiwa hivyo walipelekwa magharibi huko Australia. Mnamo 1867, Ross Lewin, aliyekuwa katika Jeshi la Wanamaji la Uingereza, aliwauzia wapandaji wa miwa na pamba “wenyeji bora na wenye bidii zaidi wa visiwani kwa [pauni] saba tu kila mmoja.”

Jitihada za wenye mamlaka wa Uingereza za kukomesha biashara hiyo ya watumwa hazikufaulu. Kwanza, haikuwa rahisi kutekeleza sheria ya Uingereza kwa raia wa mataifa mengine. Pili, sheria ya Uingereza haikufafanua utumwa ni nini. Hivyo, walipofikishwa mahakamani, wafanyabiashara hao walifaulu kusema kwamba wakaaji wa visiwa hivyo, ingawa walidanganywa na kuchukuliwa mateka, hakuwa watumwa bali walikuwa watu wanaofanya kazi chini ya mkataba fulani na watalipwa na hata baadaye waruhusiwe kurudi nyumbani. Wengine hata walidai kwamba walikuwa wakiwanufaisha wapagani hao kwa kuwaleta chini ya sheria ya Uingereza na kuwafundisha kufanya kazi! Kwa hiyo, biashara ya watumwa ilinawiri kwa muda fulani.

Mkondo Wabadilika

Kadiri raia waliokuwa na maoni yaliyosawazika walivyopinga biashara ya watumwa, ndivyo  mambo yalivyoanza kubadilika. Baadhi ya wakaaji wa visiwa waliajiriwa kazi kwa hiari yao. Kuwateka watu kwa nguvu hakukuruhusiwa. Pia kuwatendea watu vibaya hakukuruhusiwa kama vile kuwapiga viboko, kuwatia alama, au hali zenye kutisha ambazo baadhi ya wafanyakazi walikabili nyumbani na kazini.

Hali zilibadilika hata zaidi wakati kasisi Mwanglikana J. C. Patteson aliyepinga waziwazi biashara ya watumwa alipouawa na wenyeji wa visiwa aliotaka kuwalinda. Kwa kutumia njia yao ya kawaida ya ujanja, wafanyabiashara wa utumwa walifika kisiwani kabla ya Patteson katika meli iliyokarabatiwa kimakusudi ili ionekane kama yake. Wenyeji walikaribishwa ndani ya meli ili wakutane na kasisi. Hawakuonekana tena. Patteson mwenyewe alipowasili, alikutana na umati wenye hasira, na akauawa kimakosa ili kulipiza kisasi. Kwa sababu ya kisa hicho na kwa sababu watu wengi waliteta, meli za kijeshi za Waingereza na Wafaransa ziliwekwa kwenye Bahari ya Pasifiki zikiwa na amri ya kukomesha biashara hiyo.

Serikali za majimbo ya New South Wales na Queensland huko Australia ziliungana na serikali ya Uingereza kupitisha sheria kadhaa za kukomesha watu kutendewa vibaya na kudhibiti biashara iliyokuwa imekita mizizi ya kutafuta wafanyakazi. Wakaguzi waliwekwa rasmi, na wawakilishi wa serikali walitumwa kwenye meli zilizoenda kutafuta wafanyakazi. Jitihada hizo zilikuwa na matokeo mazuri kwa sababu mashtaka sasa yalihusisha utekaji nyara na mauaji, badala ya sheria zisizofanya kazi dhidi ya wafanyabiashara wa utumwa. Kulikuwa na mabadiliko makubwa kwenye Bahari za Kusini katika miaka kumi ya mwisho ya karne ya 19. Kwa kiwango kikubwa, zoea la kuwateka nyara watumwa lilikuwa limekoma, na kuingia kwa “wafanyakazi” wapya kulipungua sana mwanzoni mwa karne ya 20.

Mnamo 1901, bunge jipya la Jumuiya ya Madola ya Australia lilidhibiti uhamiaji katika nchi yote. Sera zake zilionyesha maoni ya watu ambao kufikia wakati huo walikuwa wameanza kuchukia wafanyakazi wa nchi nyingine kwa sababu wengi waliogopa watafanya wenyeji wakose kazi. Iwe walifanya kazi kwa mkataba au la, wenyeji wa visiwa vya Bahari za Kusini hawakutakikana. Maelfu walilazimishwa kurudi kwao, jambo ambalo lilisababisha huzuni zaidi kwa sababu watu fulani waliohamishwa walitenganishwa na wapendwa wao.

Watumwa Waliosahauliwa Wakumbukwa

Mnamo Septemba (Mwezi wa 9) 2000, serikali ya jimbo la Queensland ilitoa taarifa iliyowekwa mahali pa umma. Inaonyesha jukumu la wenyeji wa visiwa vya Bahari za Kusini katika ukuzi wa uchumi, utamaduni, na maendeleo ya eneo la Queensland. Wakati huohuo, taarifa hiyo inaonyesha kwamba wasimamizi wanajuta juu ya jinsi watu hao walivyotendewa kwa ukatili.

Katika historia yote, watu wengi wametumia nafasi za kujitajirisha kwa kuwatumia watu vibaya na kuwanyima uhuru. Biblia inaahidi kwamba chini ya Ufalme wa Mungu hakutakuwa na ukosefu wa haki. Kwa kweli, watu watakaokuwa raia wa kidunia chini ya serikali hiyo ya mbinguni “wataketi, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, wala hakutakuwa na mtu yeyote anayewatetemesha.”—Mika 4:4.

[Mchoro/Ramani katika ukurasa wa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Watumwa walipelekwa Australia na Amerika Kusini

BAHARI YA PASIFIKI

MICRONESIA

VISIWA VYA MARSHALL

New Guinea

VISIWA VYA SOLOMON

TUVALU

AUSTRALIA KIRIBATI

QUEENSLAND VANUATU

NEW SOUTH WALES NEW CALEDONIA AMERIKA KUSINI

Sydney ← FIJI → Callao

SAMOA

TONGA

VISIWA VYA COOK

POLINESIA YA UFARANSA

Kisiwa cha Easter

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

National Library of Australia, nla.pic-an11279871