Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Dunia Inakabili Hatari?

Je, Dunia Inakabili Hatari?

Je, Dunia Inakabili Hatari?

KUONGEZEKA kwa joto duniani kumefafanuliwa kuwa hatari kubwa zaidi inayowakabili wanadamu. Kulingana na jarida Science, jambo linalowahangaisha watafiti “ni kwamba tumeanzisha mabadiliko ya polepole yasiyoweza kusimamishwa.” Watu wenye mashaka hawakubaliani na hilo. Wengi wanakubali kwamba joto linaongezeka duniani, lakini wana mashaka kuhusu kinachosababisha ongezeko hilo na matokeo yake. Wanasema kwamba huenda wanadamu wanachangia hali hiyo lakini wao si kisababishi kikuu. Kwa nini kuna maoni tofauti?

Kwanza, mifumo inayotegemeza hali ya hewa duniani ni tata na haijaeleweka vizuri. Pia, vikundi vinavyoshughulikia mazingira hutoa maoni yao kuhusu takwimu za kisayansi, kama zile zinazotumiwa kuonyesha kwa nini joto linaongezeka.

Je, Kweli Joto Linaongezeka?

Kulingana na ripoti ya karibuni ya Kamati ya Serikali Mbalimbali Kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa (IPCC) iliyofadhiliwa na Umoja wa Mataifa, kuongezeka kwa joto duniani ni jambo hakika; au “lisilotiliwa shaka” na “inawezekana sana” kwamba wanadamu wamechangia kwa sehemu kubwa hali hiyo. Wengine wanaopinga mkataa huo, hasa kuhusiana na shughuli za wanadamu kuchangia, wanasema kwamba huenda majiji yana joto zaidi kwa sababu yanakua. Isitoshe, saruji na chuma huhifadhi joto kwa haraka na kulipoteza joto hilo polepole wakati wa usiku. Watu wenye mashaka wanasema kwamba takwimu kutoka majijini hazionyeshi hali katika maeneo ya vijijini na zinaweza kupotosha takwimu za dunia nzima.

Kwa upande mwingine, Clifford, mzee wa kijiji anayeishi kwenye kisiwa karibu na ufuo wa Alaska anasema kwamba amejionea mabadiliko. Watu katika kijiji chake husafiri juu ya theluji ya bahari hadi kwenye nchi kavu ili kuwinda kuro na kongoni. Hata hivyo, kuongezeka kwa joto kunafanya hilo lisiwezekane. “Mikondo ya maji imebadilika, hali ya barafu imebadilika, na kugandamana kwa Bahari ya Chukchi . . . kumebadilika,” anasema Clifford. Anaeleza kwamba bahari ilikuwa ikigandamana mwishoni mwa Oktoba (Mwezi wa 10), lakini sasa inagandamana mwishoni mwa Desemba (Mwezi wa 12).

Mnamo 2007, joto liliongezeka katika Njia ya Kaskazini-Magharibi, ambayo ingeweza kupitika kwa mara ya kwanza katika historia. “Mwaka huu tumeona kuongezeka kwa kipindi ambacho hakuna theluji,” alisema mwanasayansi mkuu katika Kituo cha Kitaifa cha Kuhifadhi Habari za Theluji na Barafu huko Marekani.

Gesi Zinazoongeza Joto Ni Muhimu kwa Uhai

Jambo moja linalosababisha mabadiliko hayo ni kuongezeka sana kwa gesi zinazoongeza joto. Hilo ni tukio la asili ambalo ni muhimu ili kuendeleza uhai duniani. Nishati kutoka kwa jua inapofika duniani, asilimia 70 inafyonzwa na hivyo kuongeza joto la hewa, nchi kavu, na bahari. Kama hakungekuwa na utaratibu huo, kwa wastani kiwango cha joto juu ya dunia kingekuwa Selsiasi 18 chini ya sufuri. Hatimaye, joto hilo linaruhusiwa kutoka na hivyo huzuia dunia isiwe na joto jingi kupita kiasi. Lakini vitu vinavyochafua hewa vinapobadili muundo wa angahewa, hilo huzuia joto lisilohitajiwa lisitoke. Hilo linaweza kufanya joto liongezeke duniani.

Baadhi ya gesi zinazochangia ongezeko la joto ni kaboni dioksidi, nitrasi oksidi, na methini, vilevile mvuke wa maji. Gesi hizo zimeongezeka sana katika miaka 250 iliyopita, tangu mwanzo wa mvuvumko wa kiviwanda na kutumiwa zaidi kwa nishati yenye kaboni, kama vile makaa ya mawe na mafuta. Inaelekea kwamba jambo lingine linaloongeza joto ni kuongezeka kwa wanyama wa kufugwa ambao mfumo wao wa kumeng’enya chakula unatokeza methini na nitrasi oksidi. Watafiti fulani wanataja sababu zingine za kuongezeka kwa joto ambazo wanasema zilitokea kabla wanadamu hawajaathiri mazingira.

Je, Ni Badiliko la Kawaida Tu?

Watu wenye mashaka kuhusu jinsi wanadamu wanavyochangia kuongezeka kwa joto, wanasema kwamba kiwango cha joto kimebadilika sana wakati uliopita. Kama uthibitisho wanataja wakati ambapo dunia ilikuwa na barafu nyingi zaidi kuliko sasa. Na kuhusu kuongezeka kwa joto wanasema kwamba maeneo yenye baridi kama vile Greenland, wakati fulani yalikuwa na mimea inayopatikana hasa katika maeneo yenye joto. Bila shaka, wanasayansi wanakubali kwamba kadiri wanavyochunguza wakati wa zamani zaidi ndivyo uhakika kuhusu hali ya hewa unavyopungua.

Kabla shughuli za wanadamu hazijaathiri mazingira, ni nini kilichofanya kiwango cha joto kibadilike sana? Huenda chanzo kimoja ni utendaji katika jua unaoathiri kiwango cha joto kinachotolewa na jua. Umbali wa dunia kutoka kwa jua hubadilika kwa kuwa njia ambayo dunia hutumia kuzunguka jua hubadilika baada ya maelfu ya miaka. Pia mavumbi ya volkano na mabadiliko katika mikondo ya bahari yanachangia kubadilika kwa kiwango cha joto.

Kuchunguza Mazingira

Hata chanzo kiwe nini, ikiwa kiwango cha joto duniani kinaongezeka, hilo litakuwa na matokeo gani kwetu na kwa mazingira? Ni vigumu kutabiri kwa njia hususa jinsi hali itakavyokuwa. Hata hivyo, siku hizi wanasayansi wana kompyuta za hali ya juu wanazoweza kutumia kutabiri matokeo katika mazingira. Mfumo huo wa kompyuta unatia ndani sheria za fizikia, takwimu za mazingira, na mambo ya asili yanayoathiri hali ya hewa.

Mifumo hiyo ya kompyuta inawawezesha wanasayansi kufanya majaribio kuhusiana na hali ya hewa katika njia ambazo hazingewezekana kihalisi. Kwa mfano, wanaweza “kubadili” kiwango cha joto la jua ili waone jinsi inavyoathiri barafu kwenye ncha za dunia, kiwango cha joto kwenye hewa na bahari, kadiri ambavyo maji yanavukizwa, shinikizo la hewa angani, kufanyizwa kwa mawingu, upepo, na mvua. Wanaweza “kufanyiza” milipuko ya volkano na kuchunguza matokeo ya mavumbi ya volkano katika hali ya hewa. Na wanaweza kuchunguza matokeo ya ongezeko la watu, kuharibiwa kwa misitu, matumizi ya ardhi, mabadiliko katika kutokezwa kwa gesi zinazoongeza joto, na kadhalika. Wanasayansi wanatumaini kwamba hatua kwa hatua mifumo yao ya kompyuta itakuwa sahihi na yenye kutegemeka zaidi.

Mifumo ya sasa ni sahihi kadiri gani? Bila shaka, mengi yanategemea usahihi na wingi wa takwimu zinazoingizwa katika mifumo hiyo. Hivyo kunakuwa na matokeo mbalimbali, mengine yakitabiri mabadiliko madogo na mengine matokeo mabaya. Hata hivyo, kulingana na jarida Science “kunaweza kuwa na mambo yasiyotarajiwa katika mfumo wa [asili] wa hewa.” Tayari kumekuwa na mambo yasiyotarajiwa, kama vile kuyeyuka kwa haraka sana kwa theluji ya Aktiki, ambako kumewashangaza wataalamu wengi wa hali ya anga. Ikiwa wenye mamlaka ya kutunga sheria na viwango wangejua matokeo ya kile ambacho mwanadamu anafanya au hafanyi sasa, wangeweza kufanya maamuzi ambayo yangepunguza matatizo ya wakati ujao.

Wakifikiria uwezekano huo, wanakamati wa IPCC walichunguza majaribio sita ya mifumo ya kompyuta yaliyohusisha hali mbalimbali kila moja ikiathiri hewa na mazingira kwa njia tofauti. Hali hizo zilitia ndani kutokezwa kwa wingi kwa gesi zinazoongeza joto duniani, vizuizi vichache vilivyopo, na pia kuwekwa kwa vizuizi vikali. Kupatana na matarajio hayo, wachanganuzi wanahimiza kuwe na sheria kadhaa. Sheria hizo zinatia ndani vikwazo kwa matumizi ya nishati ya kaboni, adhabu kwa watakaokiuka sheria hizo, kutokezwa kwa nishati nyingi zaidi ya nyuklia, na kuanzishwa kwa teknolojia zisizoathiri mazingira.

Je, Mifumo Hiyo Inategemeka?

Wachambuzi wanasema kuwa mbinu za sasa za kutabiri “zinarahisisha sana mifumo ya hewa ambayo haijaeleweka vizuri” na “zinapuuza mifumo mingine.” Pia wanataja kwamba matokeo ya kompyuta hayapatani nyakati zote. Mwanasayansi mmoja aliyeshiriki mazungumzo katika kamati ya IPCC alisema hivi: “Baadhi yetu tunahisi kwamba kupima na kuelewa mfumo wa hewa ulio tata sana ni kazi kubwa hivi kwamba tuna mashaka kuhusu uwezo wetu wa kujua mfumo huo unafanya nini na kwa nini.” *

Bila shaka, wengine watasema kwamba kukosa kufanya mabadiliko kwa sababu hatuna hakika kuhusu chanzo cha matatizo si uamuzi wa busara. Wanasema hivi: “Tunaweza kuwaelezaje watoto wetu?” Iwe mifumo hiyo ya kompyuta ni sahihi au la, tunaweza kuwa na hakika kwamba dunia imo hatarini. Baadhi ya mambo machache yasiyopingika na yanayoharibu uwezo wa mazingira wa kuendeleza uhai ni uchafuzi, kuharibiwa kwa misitu, kupanuka kwa majiji, na kutoweka kwa jamii za viumbe.

Kulingana na yale tunayojua, je, tunaweza kuwatarajia wanadamu kwa ujumla wabadili mtindo wao wa maisha ili wahifadhi makao yetu yanayopendeza na kutuhifadhi pia? Isitoshe ikiwa shughuli za binadamu zinaongeza kiwango cha joto duniani, huenda tuna miaka tu wala si karne nyingi za kufanya mabadiliko. Kufanya mabadiliko hayo kunamaanisha kushughulikia haraka vyanzo vya matatizo ya dunia, yaani, pupa ya mwanadamu, ubinafsi, kukosa ujuzi, serikali zisizo na uwezo, na kutojali. Je, hilo ni jambo linalowezekana au ni ndoto tu? Ikiwa ni ndoto, je, tuna tumaini lolote? Swali hilo litazungumziwa katika makala inayofuata.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 20 John R. Christy, msimamizi wa Kituo cha Sayansi cha Mfumo wa Dunia katika Chuo Kikuu cha Alabama, Huntsville, Marekani, kama ilivyoripotiwa katika gazeti The Wall Street Journal la Novemba 1, 2007 (1/11/2007).

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

KIWANGO CHA JOTO CHA DUNIA HUPIMWAJE?

Ili kuonyesha ugumu wa kufanya hivyo, wewe ungepimaje kiwango cha joto katika chumba kikubwa? Kwa mfano, ungeweka wapi kipima-joto? Kwa kuwa joto hupanda, kuna uwezekano kwamba hewa iliyo juu itakuwa yenye joto zaidi ya ile iliyo chini. Vilevile kiwango cha joto kinachoonyeshwa na kipima-joto kitatofautiana ikiwa utakiweka karibu na dirisha, ikiwa kinapigwa na jua, au kikiwa chini ya kivuli. Pia rangi inaweza kufanya kipima-joto kionyeshe vipimo tofauti kwa kuwa maeneo yasiyo na rangi nyangavu hufyonza joto zaidi.

Kwa hiyo, huenda kipimo kimoja hakitatosha. Utahitaji kuchukua kiwango cha joto kutoka sehemu mbalimbali kisha ukadirie wastani. Na huenda vipimo vyenyewe vikabadilika siku tofauti-tofauti na majira tofauti-tofauti. Ili kupata wastani unaotegemeka, utahitaji kuchukua vipimo vingi kwa muda mrefu. Hivyo, hebu wazia jinsi ilivyo vigumu kupima kiwango cha ujumla cha joto cha nchi kavu, angahewa, na bahari! Hata hivyo, takwimu hizo ni muhimu ili kuchunguza kwa usahihi mabadiliko ya hali ya hewa.

[Hisani]

NASA photo

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

JE, NISHATI YA NYUKLIA NDILO SULUHISHO?

Nishati inazidi kutumika ulimwenguni pote kwa wingi zaidi. Kwa kuwa kutumiwa kwa mafuta na makaa ya mawe kunatokeza gesi zinazosababisha ongezeko la joto, serikali fulani zinafikiria kutumia nishati ya nyuklia kwa kuwa haitokezi uchafu mwingi. Lakini hilo linatokeza matatizo pia.

Gazeti International Herald Tribune linasema kwamba huko Ufaransa, ambayo ni mojawapo ya nchi zinazotegemea zaidi nishati ya nyuklia, kila mwaka inahitaji lita bilioni 18,900 za maji ili kupoesha mitambo ya nyuklia. Kulipokuwa na joto kali sana mnamo 2003, maji moto ambayo hutolewa kwa ukawaida katika mitambo hiyo ya nyuklia ilitishia kuongeza kiwango cha joto katika mito hivi kwamba viumbe wote wangehatarishwa. Hivyo, mitambo fulani iliacha kutumiwa. Inatazamiwa kwamba hali hiyo itakuwa mbaya zaidi ikiwa viwango vya joto duniani vitaongezeka.

“Ni lazima tusuluhishe tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa ili tutumie nishati ya nyuklia,” mtaalamu wa mambo ya nyuklia David Lochbaum ambaye ni mwanachama wa Muungano wa Wanasayansi Wanaojali.

[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 7]

MISIBA ILIYOSABABISHWA NA HALIi YA HEWA MNAMO 2007

Katika mwaka wa 2007, kulikuwa na misiba mingi iliyosababishwa na hali ya hewa. Kufuatia hilo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Masuala ya Kibinadamu, ilitoa wito wa msaada wa dharura mara 14, na hiyo ilikuwa mara 4 zaidi ya rekodi ya awali iliyowekwa mnamo 2005. Misiba iliyoorodheshwa hapa ni baadhi ya ile iliyotukia katika 2007. Kumbuka kuwa kila tukio halionyeshi hali ya muda mrefu ya eneo fulani.

Uingereza: Watu zaidi ya 350,000 waliathiriwa na mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutukia katika zaidi ya miaka 60. Uingereza na Wales zilipata kiwango kikubwa zaidi cha mvua katika miezi ya Mei (Mwezi wa 5) hadi Julai (Mwezi wa 7) tangu rekodi zilipoanza kuwekwa mnamo 1766.

Afrika Magharibi: Mafuriko yaliwaathiri watu 800,000 katika nchi 14.

Lesotho: Kiwango cha juu cha joto na ukame uliharibu mimea. Huenda watu 553,000 hivi wakahitaji msaada wa chakula.

Sudan: Mvua nyingi iliwaacha watu 150,000 bila makao. Angalau watu 500,000 walipokea msaada.

Madagaska: Tufani na mvua kubwa zilipiga kisiwa hicho na kuwaacha watu 33,000 bila makao na kuharibu mimea ya watu 260,000.

Korea Kaskazini: Inakadiriwa kuwa watu 960,000 waliathiriwa sana na mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi.

Bangladesh: Mafuriko yaliathiri watu milioni 8.5 na kuua zaidi ya watu 3,000, kutia ndani mifugo milioni 1.25. Nyumba milioni 1.5 hivi ziliharibiwa au kubomolewa kabisa.

India: Mafuriko yaliathiri watu milioni 30.

Pakistan: Mvua inayoambatana na tufani iliwaacha watu 377,000 bila makao huku mamia wakifa.

Bolivia: Watu zaidi ya 350,000 waliathiriwa na mafuriko huku 25,000 wakiachwa bila makao.

Mexico: Mafuriko katika eneo hilo yaliwaacha watu 500,000 bila makao na kuathiri watu zaidi ya milioni moja.

Jamhuri ya Dominika: Mvua iliyonyesha kwa muda mrefu ilisababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, na kufanya watu 65,000 wapoteze makao.

Marekani: Mioto iliyokumba eneo la kusini la California liliwafanya wakaaji 500,000 wahame.

[Hisani]

Based on NASA/Visible Earth imagery