Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ushirikiano wa Ajabu Katika Udongo

Ushirikiano wa Ajabu Katika Udongo

 Je, Ni Kazi ya Ubuni?

Ushirikiano wa Ajabu Katika Udongo

▪ Katika udongo, kuna ushirikiano wa ajabu unaoendeleza uhai kati ya mimea fulani na bakteria.

Fikiria hili: Nitrojeni ni muhimu ili mimea ikue na kuzaa. Lakini lazima gesi hiyo igeuzwe kuwa mchanganyiko wa aina fulani kama vile amonia kabla ya kutumiwa na mimea. Mikundekunde hufanya hilo liwezekane kwa kushirikiana kwa njia yenye kunufaisha na bakteria inayoitwa rhizobia.

Kupitia kemikali ya pekee, mikundekunde huvutia bakteria iingie katika mizizi yake. Ingawa bakteria na mmea huo si za jamii moja, gazeti Natural History linasema, hizo hufanya kazi pamoja “ili kutokeza kiungo kipya: mzizi wenye kifundo cha kugeuza nitrojeni.” Bakteria huishi na kufanya kazi ndani ya kifundo hicho. Bakteria hizo hutumia hasa kimeng’enyaji cha pekee, yaani, aina fulani ya protini inayoitwa nitrogenase, inayotumiwa kugeuza nitrojeni inayopatikana katika hewa iliyo katika udongo.

“Ulimwenguni pote kiwango cha nitrogenase . . . kinaweza kutoshea ndani ya ndoo moja kubwa,” linasema gazeti Natural History. Kwa hiyo, kila molekuli ni muhimu! Lakini kuna tatizo. Kimeng’enyaji hicho huharibiwa na oksijeni. Suluhisho la tatizo hilo ni nini? Mikundekunde hutokeza kemikali fulani ya pekee ambayo huondoa oksijeni inayoweza kudhuru.

Utando unaozunguka kifundo hudhibiti kazi ya kugeuzwa kwa amonia, sukari, na virutubisho vingine kati ya bakteria na mmea. Kama tu mimea mingine, mikundekunde hufa. Inapokufa, amonia hubaki katika udongo. Hivyo, kwa kufaa, mikundekunde imeitwa “mbolea ya kijani.”

Una maoni gani? Je, bakteria na mimea inaweza “kubuni” mfumo huo tata wenye kustaajabisha unaotegemeza uhai, au je, huo ni uthibitisho mwingine wa kazi ya ubuni?

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mzizi wenye kifundo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Background: © Wally Eberhart/Visuals Unlimited; inset: © Dr. Jack M. Bostrack/Visuals Unlimited