Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Kuna Dalili za Matatizo?

Je, Kuna Dalili za Matatizo?

 Je, Kuna Dalili za Matatizo?

“Veu Lesa, mwanakijiji mwenye umri wa miaka 73 huko Tuvalu, hahitaji ripoti za kisayansi ili kutambua kwamba maji ya bahari yanaongezeka,” linasema gazeti The New Zealand Herald. “Fuo alizofurahia akiwa mtoto zinatoweka. Mimea aliyokuwa akitumia kulisha familia yake imeharibiwa na maji ya chumvi. Mnamo Aprili (Mwezi wa 4) [2007], alilazimika kuhama baada ya nyumba yake kupigwa na mawimbi yenye nguvu ambayo yalileta mawe na takataka.”

GAZETI Herald linasema kwamba wakaaji wa Tuvalu hawaoni kuongezeka kwa joto duniani kuwa jambo linalozungumziwa tu na wanasayansi, bali ni “jambo halisi la kila siku,” kwani visiwa hivyo viko mita nne hivi juu ya usawa wa bahari. * Tayari maelfu ya watu wamehama visiwa hivyo na wengine wengi wanajitayarisha kuhama.

Wakati huohuo, Naisula, anayeishi mashariki mwa Kenya, lazima atembee kwa kilomita 10 hivi ili apate maji safi. Kisha anahitaji kusubiri zamu yake ili ajaze mtungi wake kwa maji na kuubeba mtungi huo mzito kurudi nyumbani ili atosheleze mahitaji ya msingi tu ya familia yake. Kwa nini wakati na jitihada nyingi hivyo zinahitajika ili kupata maji? Kwa sababu eneo analoishi limekumbwa na ukame katika miaka ya karibuni. Je, matatizo yanayokumba Kenya na Tuvalu yanathibitisha kwamba kiwango cha joto duniani kinaongezeka?

Matabiri ya Watu Fulani

Wengi wanaamini kwamba shughuli za wanadamu zimechangia kwa sehemu kubwa kuongezeka kwa joto duniani, na huenda hilo likasababisha madhara kwa hali ya hewa na mazingira. Kwa mfano, kuyeyuka kwa kiwango kikubwa cha theluji na kuongezeka kwa kiwango cha joto kunaweza kufanya kiwango cha maji ya bahari kiongezeke sana. Visiwa kama vile Tuvalu ambavyo haviko juu sana ya usawa wa bahari vinaweza kufunikwa, na vilevile sehemu kubwa za Uholanzi na Florida, kutaja tu sehemu mbili nyingine. Mamilioni ya watu wanaweza kulazimika kuhama kutoka maeneo kama vile Shanghai na Calcutta, na pia sehemu fulani za Bangladesh.

Wakati huohuo, kuongezeka kwa viwango vya joto kunaweza kuzidisha uharibifu unaosababishwa na dhoruba, mafuriko, na ukame. Katika milima ya Himalaya, kutoweka kwa miamba ya barafu, iliyo katika maeneo yanayosambazia mito saba maji, kunaweza kutokeza upungufu wa maji safi kwa ajili ya asilimia 40 ya watu duniani. Pia maelfu ya jamii za wanyama zimo hatarini, kutia ndani dububarafu ambao maisha yao yanategemea hasa maeneo ya barafu. Kwa kweli, ripoti zinaonyesha kwamba dubu wengi wanakonda na wengine hata wanakufa njaa.

Pia, kuongezeka kwa kiwango cha joto kunaweza kufanya mbu, kupe, na wadudu wengine wanaoeneza magonjwa kutia ndani kuvu, wafikie maeneo mengi zaidi na hivyo kueneza magonjwa. Kikundi fulani cha wanasayansi (Bulletin of the Atomic Scientists) kinasema kwamba “hatari zinazoweza kutokezwa na mabadiliko katika hali ya hewa ni mabaya kama yale yanayoweza kutokezwa na silaha za nyuklia. Madhara yanaweza kutokea polepole kwa sasa  . . . , lakini katika muda wa miaka 30 au 40 ijayo mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kutokeza madhara yasiyoweza kurekebishwa katika maeneo ambayo wanadamu wanategemea ili waendelee kuishi.” Jambo lingine linalotisha zaidi ni kwamba wanasayansi fulani wanaamini mabadiliko yanayotokana na kuongezeka kwa joto duniani yanatokea haraka kuliko walivyotarajia.

Tunaweza kukata kauli gani kutokana na matabiri hayo? Je, maisha duniani yamo hatarini? Watu wenye mashaka kuhusu kuongezeka kwa joto duniani wanasema kwamba matabiri hayo hayana msingi. Wengine hawajui waamini nini. Kwa hiyo, ukweli ni nini? Je, wakati ujao wa dunia, kutia ndani wetu, umo hatarini?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Tunapozungumzia kuongezeka kwa joto duniani, hilo linahusisha kuongezeka kwa joto la angahewa na bahari.