Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Uvumbuzi Wenye Kushangaza Katika Ikweta ya Dunia

Uvumbuzi Wenye Kushangaza Katika Ikweta ya Dunia

Uvumbuzi Wenye Kushangaza Katika Ikweta ya Dunia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI EKUADO

KULIKUWA na mjadala mkali kuhusu umbo hususa la dunia kwenye Chuo cha Sayansi cha Paris kilicho maarufu mnamo 1735. Wale waliounga mkono nadharia za Isaac Newton walikata kauli kwamba dunia ilikuwa mviringo lakini ilikuwa tambarare kidogo kwenye ncha. Wale waliounga mkono nadharia za Cassini walisema kwamba dunia ilikuwa tambarare kwenye ikweta.

Kwa hiyo, mnamo 1736, vikundi viwili vya wanasayansi vilitumwa ili kupima mpindo wa dunia. Kikundi kimoja kilienda Lapland, kuelekea Ncha ya Kaskazini, na kile kingine kikaenda Ekuado ya leo, kwenye ikweta. * Uchunguzi huo ulithibitisha kwamba waliotetea nadharia za Newton walikuwa sahihi.

Ili kuadhimisha mwaka wa 200 tangu wanasayansi hao Wafaransa walipofunga safari ya kwenda Ekuado, mnara wa ukumbusho ulijengwa karibu na Quito, mji mkuu wa Ekuado mnamo 1936. Mnara huo umesimamishwa kwenye mstari ambao wanasayansi hao Wafaransa wa karne ya 18 walifikiri kuwa ndio ikweta. Hadi leo, watalii hutembelea mnara huo unaoitwa, Katikati ya Dunia. Wakiwa hapo wanaweza kukanyaga pande mbili za dunia zinazotenganishwa na ikweta. Lakini je, hilo ni kweli?

La! Uvumbuzi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba mstari wa ikweta uko mbali kidogo na mahali hapo. Kwa kushangaza, karne nyingi kabla ya wanasayansi Wafaransa waliotumwa kuchunguza nadharia ya Newton kufika huko, wenyeji wa eneo hilo walikuwa tayari wamegundua mahali hususa ambapo mstari huo ulipaswa kuwa. Hilo lingewezekanaje?

Ikweta Halisi

Mnamo 1997, magofu ya ukuta wa nusu duara yaliyoonekana kuwa hayana maana yoyote yalivumbuliwa kwenye kilele cha Mlima Catequilla, ambao uko kaskazini kidogo ya Quito. Kwa kutumia mfumo wa kupokea habari kutoka kwa setilaiti (GPS), mchunguzi, Cristóbal Cobo aligundua kwamba mwisho mmoja wa ukuta huo ulikuwa umejengwa kabisa kwenye ikweta. *

Huenda kujengwa kwa ukuta huo kwenye mstari mmoja na ikweta halisi kukaonwa kuwa jambo lililotukia tu bila kufikiriwa. Hata hivyo, mstari unaounganisha miisho miwili ya ukuta huo hufanyiza pembe ya digirii 23.5 kuelekea ikweta. Hiyo inakaribia kulingana kabisa na pembe ya mwinamo wa mhimili wa dunia! * Isitoshe, mwisho mmoja wa mstari unaounganisha pande mbili za ukuta huo huelekea kwenye upande ambao jua huchomoza linapokuwa kaskazini kabisa ya ikweta katika mwezi wa Desemba, na mwisho ule mwingine huelekea kwenye upande ambao jua hutua linapokuwa kusini kabisa ya ikweta katika mwezi wa Juni. Mambo mengine mengi yangevumbuliwa.

Kwa kutumia kifaa cha kupima pembe juu ya Mlima Catequilla, watafiti waligundua kwamba piramidi za Cochasquí zilizojengwa na watu walioishi kabla ya Wainka zilikuwa kwenye pembe inayolingana na kuchomoza kwa jua linapokuwa kusini kabisa ya ikweta mwezi wa Juni. * Jambo lenye kutokeza ni kwamba, jiji la Pambamarca, eneo lingine ambapo vitu vya kale vimechimbuliwa, liko kwenye pembe inayolingana na kuchomoza kwa jua linapokuwa kaskazini kabisa ya ikweta mwezi wa Desemba.

Je, inawezekana kwamba Mlima Catequilla ulitumiwa kama kituo cha kuchunguza nyota? Je, miji mingine ilijengwa kulingana na hesabu iliyofanywa katika kituo hicho?

Uvumbuzi Zaidi Wenye Kushangaza

Mistari mingine inayolingana na ikweta ilipochorwa kwenye ramani, umbo la nyota yenye ncha nane lilianza kutokea. Umbo hilo hupatikana katika vyombo vya udongo vya kale na mara nyingi linawakilisha jua kwa kuwa wenyeji wa kale wa eneo hilo waliabudu jua. Vigae vya udongo vilivyofukuliwa huko Catequilla vimechunguzwa na kuonekana kuwa vya miaka elfu moja hivi mapema. Hadi leo, wenyeji hufuma nyota hiyo yenye ncha nane kwenye vitambaa na nguo sawa na walivyofanya babu zao wa kale. Hata hivyo, huenda babu zao wa kale waliona nyota hiyo kuwa muhimu zaidi kuliko watu wengi wanavyodhania.

Mradi wa Quitsa-to, uliosimamiwa na Cobo, unakusanya uthibitisho wenye nguvu kuhusu ujuzi wa nyota wa wenyeji wa kale. * Imegunduliwa kwamba nyota hiyo inapowekwa kwenye ramani juu ya ikweta, Mlima Catequilla utakuwa katikati, na miji mingi ya kale na zaidi ya maeneo 12 ambapo vitu vya kale vimechimbuliwa hujipanga kabisa kwenye mistari ya nyota hiyo.

Jambo la kushangaza hata zaidi ni kwamba mahali ambapo magofu hayakuwa yamegunduliwa wakati huo palikuwa pametabiriwa. Hilo liliwezekanaje? Mnamo Septemba 1999 Mradi wa Quitsa-to ulipendekeza kwamba uchimbuzi ufanywe kwenye sehemu ya Altamira huko Quito, mahali ambapo mojawapo ya ncha zenye digirii 23.5 ya ile nyota ilielekeza kutoka Catequilla. Kaburi mashuhuri pamoja na vyombo vya udongo vilivyokuwapo wakati wa ukoloni, wakati wa Wainka, na kabla ya kipindi cha Wainka lilichimbuliwa huko.

Baadhi ya mistari kutoka Catequilla hupita pia kwenye makanisa yaliyojengwa wakati wa ukoloni wa Hispania. Cobo anaeleza kwamba mnamo 1570, baraza la jiji la Lima lilisisitiza kwamba “makanisa, makao ya watawa, makanisa madogo na misalaba yajengwe juu ya maeneo yote matakatifu ya kipagani yanayoitwa “guacas” na mahali pa ibada pa wenyeji.” Kwa nini walifanya hivyo?

Serikali ya Hispania iliona sehemu hizo za ibada kuwa za kipagani. Hivyo ziliharibiwa, na makanisa ya Wakatoliki yakajengwa. Kujenga makanisa mahali pa mahekalu ya ibada ya kale ya jua kulifanya iwe rahisi kuwageuza wenyeji wawe Wakatoliki.

Mstari mmoja kutoka Catequilla unapita kwenye Kanisa la San Francisco ambalo liko katika sehemu ya Quito iliyokuwa chini ya ukoloni. Kanisa hilo lilijengwa katika karne ya 16 juu ya jengo lililokuwapo kabla ya Wainka. Jengo hilo lilijengwa katika njia ya kwamba jua lilipochomoza kaskazini kabisa ya ikweta mwezi wa Desemba, miale yake ingepenya kwenye kuba la kanisa na kumulika pembetatu iliyokuwa juu ya madhabahu. Jua linapozidi kuchomoza, mwale wa nuru huelekea chini na kutokeza mng’ao kwenye uso wa sanamu inayoitwa “Mungu Baba.” Jambo hilo hutukia tu wakati jua linapochomoza kaskazini kabisa ya ikweta mwezi wa Desemba! Makanisa mengine ya eneo hilo yamejengwa kwa njia hiyohiyo kwa kusudi la kuwageuza wenyeji walioabudu jua wawe Wakatoliki.

Walijuaje?

Watu hao wa kale walijuaje kwamba Catequilla ilikuwa “katikati ya dunia”? Kuna mahali pamoja tu ambapo vitu havina kivuli saa sita mchana wakati jua linapovuka ikweta. Mahali hapo ni ikweta yenyewe. Kwa hiyo Mradi wa Quitsa-to unadokeza kwamba kuchunguza vivuli kwa uangalifu kungewasaidia watu hao wa kale wafahamu mahali ambapo ikweta ilikuwa.

Isitoshe, Mlima Catequilla ni kituo cha asili cha kutazama angani ambacho kingewavutia watu walioabudu jua. Mlima huo una kimo cha meta 300 na uko katikati ya safu ya mashariki na magharibi ya Milima ya Andes. Kwa hiyo, mlima huo ungeweza kutumiwa kutazama kuchomoza na kutua kwa jua kila siku. Kwa mfano, vilele vyenye kuvutia vya volkano ya Cayambe na Antisana vyenye kimo cha kilometa tano hivi ambavyo huonekana waziwazi upande wa mashariki hutumiwa kupima mwendo wa jua.

Pia mtu akiwa kwenye Mlima Catequilla anaweza kutazama pande zote na kuona bila kutumia darubini karibu miji 20 ya kale na maeneo 50 ambapo vitu vya kale vimechimbuliwa. Isitoshe, mtu anaweza kuona anga lote upande wa kusini na kaskazini kutoka Mlima Catequilla kwa sababu uko kwenye ikweta. Hivyo kwa kweli, Mlima Catequilla unaweza kusemwa kuwa uko katikati ya dunia kwani hakuna mahali pengine kwenye ikweta ambapo mtu anaweza kuona mambo yote hayo akiwa meta 3,000 juu ya usawa bahari.

Sehemu kubwa ya ikweta inapitia baharini au kwenye msitu wa tropiki, ambako mimea humzuia mtu asione nyota. Isitoshe, mimea hiyo haiwezi kutumiwa kupima mwelekeo kwa usahihi, kwa kuwa hubadilika-badilika inapokua na kunyauka. Kenya ndiyo nchi pekee yenye milima karibu na ikweta, lakini milima hiyo haijazungukwa na safu za milima kama huko Catequilla. Naam, Mlima Catequilla uko mahali panapofaa kabisa kutazama angani.

Walikuwa Nani?

Watu hao wa zamani waliochunguza nyota walikuwa nani? Mradi wa Quitsa-to unadokeza kwamba huenda ikawa makabila ya wenyeji, kama vile Quitu au Cara ndiyo yaliyokuwa ya kwanza kuwa na ujuzi huo. Hata hivyo, mradi huo ungali mchanga, na bado kuna mengi ya kujifunza.

Hata hivyo, mafundisho fulani ya msingi kuhusu wakazi wa mapema yako wazi. Ilikuwa muhimu kuelewa mwendo wa jua ili kujua wakati unaofaa wa kulima. Kwa kuwa jua ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza uhai, si ajabu kwamba liliabudiwa. Kwa hiyo, kutazama na kupima jua kuliacha kuonwa kuwa jambo la kielimu na kuonwa kuwa jambo la kidini.

Inaonekana kwamba bidii kwa ajili ya mambo ya kidini iliwachochea watu wajifunze kwa makini mbingu, jua, mwezi, na nyota. Inaonekana kwamba baada ya kujifunza kwa karne nyingi walipata ujuzi mwingi kuhusu nyota ambao sasa unafunuliwa kupitia uvumbuzi wenye kushangaza katika maeneo yanayozunguka Mlima Catequilla.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 “Ekuado” ni neno la Kihispania la “ikweta.”

^ fu. 8 Kwa upande mwingine, kulingana na mfumo wa GPS, mnara maarufu wa ukumbusho wa Katikati ya Dunia uko meta 300 hivi kusini ya ikweta halisi.

^ fu. 9 Mwinamo kamili ni digirii 23.45.

^ fu. 10 Wainka walivamia nchi ambayo sasa inaitwa Ekuado na kuimiliki kwa kipindi kifupi, kuanzia mwaka wa 1470 hadi mwaka wa 1532 hivi, mwaka ambao Hispania ilianza kutawala nchi nyingine.

^ fu. 14 Neno “Quitsa-to” linatokana na lugha ya Wahindi wa Tsáchila nalo linamaanisha “katikati ya dunia.” Watu fulani wanaamini kwamba neno Quito linatokana na Quitsa-to.

[Sanduku[Mchoro katika ukurasa wa 23]

Solistasi na Ikwinoksi

Kwa kuwa dunia imeinama kwenye mhimili wake kwa digrii 23.5, jua halichomozi na kutua mahali palepale kila siku. Badala yake, jua husonga polepole kutoka kaskazini na kusini ya ikweta. Bila shaka, jua lenyewe halisongi kwa kuwa dunia ndiyo husonga inapozunguka jua mwaka mzima.

Mara moja kwa mwaka, wakati dunia inapozunguka na kuinamisha mhimili wake kabisa kuelekea jua katika Kizio cha Kaskazini, jua litachomoza kaskazini kabisa ya mhimili wa dunia: digrii 23.5 kaskazini ya ikweta. Hilo hutukia karibu na Juni 21. Wakati Kizio cha Kusini kinapoinamisha kabisa mhimili wake kuelekea jua, jua huchomoza kusini kabisa ya mhimili wa dunia: digrii 23.5 kusini ya ikweta. Hilo hutukia karibu Desemba 21. Matukio hayo mawili huitwa solistasi.

Hata hivyo, katikati ya matukio hayo mawili, jua huwa juu kabisa ya ikweta. Tukio hilo linaitwa ikwinoksi, linalomaanisha kwamba mchana na usiku zina urefu sawa duniani pote. Machi 20 na Septemba 21 hivi jua huchomoza mashariki kabisa, na kufuata ikweta kwa muda wa saa 12, kisha hutua magharibi kabisa. Saa sita mchana wakati wa ikwinoksi, jua huwa juu kabisa ya ikweta na hakuwi na kivuli chochote katika sehemu hiyo.

[Mchoro]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Solistasi

Desemba 20, 21, 22, au 23

Ikwinoksi

Machi 19, 20, au 21

Solistasi

Juni 20, 21, au 22

Ikwinoksi

Septemba 21, 22, 23, au 24

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Mlima Catequilla, juu yake kuna magofu ya kale yaliyojengwa juu ya ikweta

[Picha katika ukurasa wa 25]

Maeneo mengi ambapo vitu vya kale vimechimbuliwa na miji mingi ya kale imejipanga kabisa kwenye mistari ya nyota

[Picha katika ukurasa wa 25]

Nyota yenye ncha nane inayopatikana katika vyombo vya udongo vya kale na vitambaa vilivyofumwa