Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tauni Mbaya Zaidi Katika Historia

Tauni Mbaya Zaidi Katika Historia

Tauni Mbaya Zaidi Katika Historia

MNAMO Oktoba 1918, Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vilikuwa bado vikiendelea. Ingawa vita hivyo vilikuwa karibu kwisha, vyombo vya habari vilikuwa bado vimewekewa vizuizi. Kwa hiyo, Hispania ambayo haikuwa ikipigana ndiyo nchi pekee iliyoweza kuripoti kwamba raia katika sehemu nyingi walikuwa wakiugua na kufa kwa kiwango chenye kushtua. Hali hizo ndizo zilizofanya ugonjwa huo uitwe homa ya Hispania.

Ugonjwa huo ulioenea sana ulianza mnamo Machi 1918. Wachunguzi wengi wanasema kwamba homa hiyo ilianzia jimbo la Kansas, Marekani. Yaonekana kwamba baada ya hapo ilienezwa Ufaransa na majeshi ya Marekani yaliyoenda huko. Baada ya idadi ya vifo vilivyosababishwa na homa hiyo kuongezeka haraka, ni kana kwamba hali ilitulia kufikia Julai 1918. Madaktari hawakujua kwamba wakati huo tauni hiyo ilikuwa ikipata nguvu na kuwa hatari zaidi.

Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vilipokoma Novemba 11, 1918, ulimwengu ulishangilia. Kwa kushangaza, karibu na wakati huohuo, ugonjwa huo wa kuambukiza ulilipuka ulimwenguni pote. Ugonjwa huo uliokuwa hatari ulitangazwa na vyombo vya habari ulimwenguni pote. Ni watu wachache tu walioishi wakati huo ambao hawakuathiriwa. Kila mtu aliogopa. Mtaalamu mmoja wa kuchunguza ugonjwa wa homa alisema hivi: “Muda ambao watu walitarajiwa kuishi nchini Marekani ulipungua kwa zaidi ya miaka 10 katika 1918.” Ugonjwa huo wa kuambukiza ulitofautianaje na magonjwa mengine?

Ugonjwa Usio wa Kawaida

Tofauti kubwa kati ya homa hiyo na nyingine ni kwamba iliua haraka. Iliua haraka kadiri gani? Katika kitabu cha karibuni kinachoitwa The Great Influenza, mwandikaji John M. Barry ananukuu visa fulani kuhusu ugonjwa huo: “Huko Rio de Janeiro, mwanamume fulani alimwuliza Ciro Viera Da Cunha, aliyekuwa akisomea udaktari, habari fulani kwa sauti ya kawaida kabisa walipokuwa wakingojea tramu, kisha akaanguka na kufa; huko Cape Town, Afrika Kusini, Charles Lewis alipanda tramu kuelekea nyumbani kwake umbali wa kilometa tano wakati kondakta alipoanguka na kufa. Gari hilo liliposafiri kilometa tano zilizosalia, watu wengine sita kutia ndani dereva walikufa.” Wote walikufa kutokana na homa hiyo.

Halafu, kulikuwa na woga, yaani, woga wa kitu kisichojulikana. Wanasayansi hawangeweza kueleza ni nini hasa kilichosababisha ugonjwa huo na jinsi ulivyoenea. Hatua za kulinda afya ya umma zilichukuliwa: watu walioishi katika miji yenye bandari hawakuruhusiwa kutoka; majumba ya sinema, makanisa, na sehemu nyingine za umma za kukutania zilifungwa. Kwa mfano, huko San Francisco, California, Marekani, maofisa waliwaamuru watu wote wafunike midomo na pua zao kwa vitambaa. Yeyote ambaye angepatikana akiwa hajajifunika mahali pa umma angetozwa faini ama kufungwa. Lakini hakuna mbinu iliyofua dafu. Mbinu hizo hazikufanikiwa kwani zilitumiwa ikiwa kuchelewa mno.

Pia, watu waliogopa kwa sababu homa hiyo iliwapata watu bila kubagua. Kwa sababu ambazo bado hazieleweki, ugonjwa huo wa mwaka wa 1919 haukuwapata tu wazee; uliwapata na kuwaua vijana wenye afya. Wengi wa waliokufa kutokana na homa ya Hispania walikuwa na umri wa kati ya miaka 20 na 40.

Isitoshe, tauni hiyo ilienea ulimwenguni pote. Hata ilifika kwenye visiwa vya tropiki. Homa hiyo ilipelekwa Samoa Magharibi (sasa inaitwa Samoa) na meli Novemba 7, 1918, na baada ya miezi miwili, asilimia 20 hivi ya wakazi 38,302 wa huko walikufa. Nchi zote kubwa za ulimwengu ziliathiriwa sana!

Pia, tauni hiyo iliua watu wengi sana. Kwa mfano, ugonjwa huo ulitokea mapema na kuua watu wengi sana huko Philadelphia, Pennsylvania, Marekani. Kufikia katikati ya Oktoba 1918, kulikuwa na upungufu mkubwa sana wa majeneza. “Mtengenezaji mmoja alisema kwamba angeweza kuuza majeneza 5,000 kwa muda wa saa mbili ikiwa angekuwa nayo. Nyakati nyingine chumba cha kuhifadhia maiti cha jiji kilikuwa na maiti zilizozidi idadi ya majeneza mara kumi,” anasema mwanahistoria Alfred W. Crosby.

Baada ya muda mfupi tu, homa hiyo ilikuwa imeua watu wengi zaidi kuliko tauni yoyote iliyowahi kutokea katika historia ya wanadamu. Makadirio ya kawaida yanaonyesha kwamba watu milioni 21 walikufa ulimwenguni pote, lakini sasa wataalamu fulani wanasema kwamba idadi hiyo ni ndogo. Leo wataalamu fulani wa magonjwa ya kuambukiza wanadokeza kwamba huenda watu milioni 50 walikufa au labda milioni 100 hivi! Barry aliyetajwa juu anasema hivi: “Homa hiyo iliua watu wengi zaidi kwa mwaka mmoja kuliko wale waliouawa na Tauni iliyotokea Zama za Kati katika karne moja; iliua watu wengi zaidi katika majuma 24 kuliko wale ambao wameuawa na UKIMWI katika miaka 24.”

Jambo la ajabu ni kwamba homa ya Hispania iliwaua Wamarekani wengi zaidi kwa mwaka mmoja hivi kuliko jumla ya waliokufa katika vita viwili vya ulimwengu. Mwandishi Gina Kolata anaeleza hivi: “Ikiwa tauni hiyo ingetokea leo, na kuua asilimia kama hiyohiyo ya Wamarekani, basi Wamarekani milioni 1.5 wangekufa. Idadi hiyo inazidi idadi ya wale wanaokufa kwa mwaka mmoja kutokana na ugonjwa wa moyo, kansa, kiharusi, magonjwa mabaya ya mapafu, UKIMWI, na ugonjwa wa Alzheimer yakijumlishwa.”

Kwa ufupi, homa ya Hispania ndiyo tauni ambayo iliwaua watu wengi zaidi katika historia ya wanadamu. Sayansi ilitoa msaada gani?

Sayansi Iliposhindwa

Kufikia mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, ilionekana kwamba sayansi ya tiba ilikuwa imefanya maendeleo makubwa kushinda magonjwa. Hata wakati wa vita hivyo, madaktari walijivunia mafanikio waliyopata katika kupunguza athari za magonjwa ya kuambukiza. Wakati huo, jarida The Ladies Home Journal lilisema kwamba Wamarekani hawakuhitaji tena kuwa na vyumba vya kuwalaza waliokufa ili kuwatazama. Lilidokeza kwamba kuanzia wakati huo vyumba hivyo viitwe vyumba vya walio hai. Lakini homa ya Hispania ikalipuka, nayo sayansi ya tiba ikashindwa kabisa.

Crosby anaandika: “Madaktari wote wa 1918 walichangia kushindwa kabisa kwa sayansi ya tiba katika karne ya 20 au, ikiwa kushindwa kwa tiba kungetegemea idadi ya vifo, basi madaktari hao walichangia kushindwa kabisa kwa sayansi ya tiba katika historia yote.” Ili madaktari peke yao wasilaumiwe, Barry anatoa hoja hii: “Wakati huo wanasayansi walielewa kabisa ukubwa wa tisho hilo, walijua jinsi ya kutibu aina nyingi za bakteria zinazosababisha nimonia, nao walitoa mashauri ya afya kwa umma ambayo yangeokoa makumi ya maelfu ya Wamarekani. Wanasiasa walipuuza mashauri hayo.”

Kwa hiyo, sasa, miaka 85 hivi baadaye, watu wamejifunza nini kuhusu tauni hiyo mbaya? Ilisababishwa na nini? Je, inaweza kutokea tena? Je, utaweza kudhibitiwa ukitokea tena? Huenda ukashangazwa na baadhi ya majibu.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Wengi wa wale ambao walikufa kutokana na homa ya Hispania walikuwa na umri wa kati ya miaka 20 na 40

[Picha katika ukurasa wa 4]

Darasa la shule mnamo 1919, huko Canon City, Colorado, Marekani

[Hisani]

Courtesy, Colorado Historical Society, 10026787

[Picha katika ukurasa wa 4, 5]

Ofisa wa polisi

[Hisani]

Photo by Topical Press Agency/Getty Images

[Picha katika ukurasa wa 5]

Wachezaji wa besiboli wakiwa wamevaa vifuniko vya kujikinga

[Hisani]

© Underwood & Underwood/CORBIS