Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Bass Rock—Mahali Ambapo Membe Hukutana

Bass Rock—Mahali Ambapo Membe Hukutana

Bass Rock—Mahali Ambapo Membe Hukutana

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

MWAMBA mkubwa wa Bass Rock una kimo cha meta 110 na kipenyo cha karibu kilometa 2. Uko mbali kidogo na ufuo wa kaskazini-mashariki ya Edinburgh, Scotland, kwenye mlango wa mto unaoitwa Firth wa Mto Forth. Membe wa kaskazini wapatao 100,000 ambao ni asilimia 10 ya ndege hao wa majini wenye kuvutia huishi hapo. *

Mapema katika karne ya 20, membe waliwindwa kwa ajili ya chakula. Mafuta yao yalitumiwa kama dawa, nayo manyoya yao yalitumiwa kutengeneza matandiko. Manyoya ya ndege wapatao 300 yalihitajiwa ili kujaza godoro moja tu. Mayai yao ambayo wakati mmoja yaliliwa, hayaliwi leo.

Membe wanaweza kuishi kwa miaka 30 na kwa kawaida huwa na mwenzi mmoja tu. Wao huhama-hama, na katika mwezi wa Januari wao hurudi mahali palepale ili kujenga viota ambavyo wao hulinda kwa bidii. Kwenye mwamba wa Bass Rock, viota hivyo hujengwa kwa magugu-maji na nyasi, na kila kiota hujengwa umbali wa meta moja hivi kutoka kwa kingine. Ndege hao hupendelea maeneo yenye upepo ambayo huwawezesha kuruka na kutua.

Inapendeza kuwatazama membe. Wanaponyoosha shingo zao na kuinua midomo yao hewani, hiyo huonyesha kwamba wanataka kuruka. Wanapoinamisha kichwa na kunyoosha mabawa yao kuelekea ndege mwingine, hiyo ni ishara kwamba wako tayari kulinda kiota chao. Ndege wanaotaka kujamiiana hufanya kana kwamba wanapigana kwa midomo yao, na yule wa kike hukubali wakati wa kiume anapouma shingo yake kidogo. Membe hutaga yai moja kwa mwaka, na mzazi yeyote yule hulalia yai hilo kwa kulikanyaga kwa mguu wake wenye utando ili kulipasha joto.

Membe aliyekomaa ni mweupe, na ana rangi nyeusi kwenye ncha ya mabawa yake ambayo huwa na urefu wa meta mbili. Tofauti na hilo, membe wadogo ni weusi nao huwa na madoa meupe madogo. Majuma 12 baada ya kuanguliwa, guga (kama aitwavyo membe mdogo) huwa na uzani mkubwa kuliko wa wazazi wake. Yeye huwa na mafuta ya ziada atakayotumia wakati wa kuhama.

Membe mdogo huanza kujitegemea wakati anapojitosa baharini na kuogelea. Hata hivyo, membe wengi wadogo hufa wakati huo, kwani mara nyingi wao huvunjika bawa au mguu wanapoteleza kwenye mwamba. Ndege ambao hufaulu kuingia majini hujifunza kuvua samaki mara moja. Mwishowe wao huhama, mara nyingi hadi Afrika Magharibi, na huenda wasirudi Bass Rock kwa miaka mitatu au minne.

Inapendeza sana kuwatazama membe wakijitosa baharini ili kukamata samaki. Wao huteremka kwa mwendo wa kilometa 100 kwa saa. Kabla tu ya kujitosa majini kutoka kimo cha meta 30 hivi, wao hurudisha mabawa yao nyuma na pua zao hujiziba. Macho yao hufunikwa na utando fulani ili kuyalinda. Wakati huohuo, vifuko vya hewa vilivyo chini ya ngozi hulinda mwili wakati unapogonga maji, kwani wao huyagonga kwa nguvu sana hivi kwamba maji hurushwa juu hewani. Nyakati nyingine samaki huduwazwa ndege hao wanapogonga maji.

Wanapokuwa chini ya maji, membe hutumia mabawa na miguu yao kuogelea ili kushika samaki. Wao hula kibua, sprati, heringi, na mkunga. Wanaweza kuvua samaki kwa muda wa saa 30 au zaidi kwa wakati mmoja. Membe fulani huenda kuvua samaki maeneo ya mbali sana upande wa mashariki hadi pwani ya Norway.

Jamii nyingine kumi hivi za ndege wa baharini huishi Bass Rock. Lakini wao hushindwa kuzaana kwa sababu ya kuongezeka kwa membe katika eneo hilo. Zamani katika miaka ya 1400, watu walienda Bass Rock ili kusali na kutafakari. Baadaye ngome ilijengwa huko, na kwa muda fulani, ikawa gereza. Ingawa mnara wa taa uliojengwa mnamo 1902 hautumiwi tena, bado taa zake humulika eneo lote la mlango wa mto.

Shamba la mtunza-mnara limejaa magugu, na sasa membe ndio wanaotawala. Mashua za kuwatembeza watu kutoka bandari ndogo ya North Berwick huwazungusha wageni kwenye kisiwa hicho ili wawaone ndege hao kwa ukaribu. Safari hiyo huwa yenye kupendeza wakati ambapo bahari imetulia.

Hata hivyo, teknolojia ya kisasa huwawezesha wageni kuwatazama membe hata kunapokuwa na hali mbaya ya hewa. Kituo cha Ndege wa Baharini cha North Berwick huko Scotland huonyesha video ya pekee kuhusu viumbe walioko Bass Rock. Kwa hiyo, mgeni anaweza kuwatazama ndege hao wasio wa kawaida wa Bass Rock kwa kutumia njia yoyote ile. Safari hiyo haiwezi kusahaulika.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Jina la Kilatini la membe wa kaskazini linaonyesha kwamba walitoka Bass Rock. Leo wanaainishwa katika jamii ya Morus bassanus, au Sula bassana.

[Picha katika ukurasa wa 27]

Membe hujitosa baharini kwa mwendo wa kilometa 100 kwa saa

[Hisani]

© NHPA/Bill Coster

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

Two gannets: Stefan Ernst/Naturfoto-Online; background: Jörn Meier/Naturfoto-Online