Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Blini za Urusi—Si chapati za maji za kawaida

Blini za Urusi—Si chapati za maji za kawaida

Blini za Urusi—Si chapati za maji za kawaida

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Urusi

Wafaransa hupika chapati za maji zinazoitwa crepes, raia wa Scotland hupika bannock, nao Wamarekani hupika flapjack. Kwa hiyo, si ajabu kwamba Warusi nao wana aina yao ya chapati za maji, zinazoitwa blini, ambazo wamekula kwa muda mrefu.

Waslav wa zamani walitoa dhabihu za blin katika desturi zao za kipagani nao waliona blin kuwa ishara inayofaa ya jua ambalo ni mviringo, lenye joto, na la rangi ya dhahabu. Wanawake waliojifungua karibuni walilishwa blin. Zililiwa pia katika arusi na mazishi, kwa hiyo zilikuwa sehemu ya maisha ya watu kuanzia kuzaliwa hadi kufa.

Kwa kawaida, Warusi leo hutengeneza blin kwa kutumia unga wa ngano, lakini mtu anaweza kutumia unga mwingine. Kwa kawaida mchanganyiko huo hutayarishwa kwa maziwa au maji au unaweza kutumia vitu vyote viwili. Lakini pia, mchanganyiko huo unaweza kutengenezwa kwa krimu, siagi ya maziwa, maziwa yaliyochacha, krimu iliyochacha, au kitu chochote kinachotokana na maziwa. Unahitaji kuwa stadi ili kukaanga blini kwani kila moja inapaswa kuwa nyembamba sana, jambo ambalo si rahisi kufanya!

Inahitaji ustadi mkubwa zaidi kutayarisha kitu cha kutia ndani ya blin. Unaweza kutumia jemu iliyotayarishwa nyumbani, kama vile ya rasiberi, stroberi, blackberry, zabibu kavu nyekundu au nyeusi, au cranberry. Au unaweza kuiandaa pamoja na dagaa, heringi, samoni, sadini, samaki wanaoitwa sprat, uyoga, nyama zilizosagwa, au jibini. Lakini Warusi huipenda pamoja na mayai mekundu au meusi ya samaki. Kumbuka kwamba blini huwa tamu zinapoliwa zikiwa moto!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

KUTAYARISHA BLINI KWA BUCKWHEAT

Viungo

Kikombe 1 cha unga wa buckwheat

Kikombe 1 cha unga wa ngano

Vijiko 2 vikubwa vya hamira kavu

Vijiko 3 vikubwa vya siagi iliyoyeyushwa

Mayai 2

Vikombe 3 hivi vya maziwa

Vijiko 2 vikubwa vya sukari

Chumvi kidogo sana

Matayarisho: Changanya unga wa buckwheat na kikombe cha maziwa. Pasha joto kikombe kingine cha maziwa na ukiongeze kwenye mchanganyiko huo, ukikoroga vizuri. Mchanganyiko huo unapopoa, uchanganye na hamira kavu. Acha mchanganyiko ufure hadi uwe na ukubwa maradufu.

Koroga mchanganyiko huo kwa kijiko cha mbao, ukiongeza chumvi na sukari. Tenganisha sehemu ya katikati ya yai na ile nyeupe. Tia sehemu hizo za katikati yai kwenye mchanganyiko huo, pamoja na siagi iliyoyeyushwa, na unga wa ngano, kisha ukoroge vizuri. Koroga sehemu nyeupe ya mayai kando, kisha uitie ndani ya mchanganyiko huo pamoja na maziwa mengine kama inavyohitajika. Acha mchanganyiko huo ufure tena.

Pasha joto kikaangio, na ukipake mafuta kidogo au siagi iliyoyeyushwa. Mwaga kiasi kidogo cha mchanganyiko wa blin ili uenee kwenye kikaangio na uwe mwembamba iwezekanavyo. Pika kwa moto mdogo hadi sehemu ya chini ya blin iwe na rangi ya dhahabu. Geuza blin na uipike kwa sekunde 15 zaidi. Iweke kwenye sahani na uihifadhi ikiwa na joto kisha upike blin zilizobaki kwa njia hiyohiyo. Andaa blini zikiwa zimepangwa juu ya nyingine.