Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ninapaswa Kujua Nini Kuhusu Dawa za Steroidi?

Ninapaswa Kujua Nini Kuhusu Dawa za Steroidi?

Vijana Huuliza . . .

Ninapaswa Kujua Nini Kuhusu Dawa za Steroidi?

“Mimi hufikiria kuhusu [madhara ya kutumia steroidi] . . . Nitaishi muda gani? . . . Lakini bado ninataka kuzitumia sasa.”—John, mnyanyua-vyuma.

JE, UNARIDHIKA na mwili wako? Au ungependa kuwa na mwili wenye misuli kama ya mwana-michezo mashuhuri au umbo jembamba kama la mwanamitindo maarufu? Je, wewe huvutiwa sana na michezo na ungependa kuongeza nguvu zako na kuboresha uwezo wako wa kukimbia?

Ikiwa unapendezwa na mambo yaliyotajwa, basi huenda ukashawishiwa kumeza vidonge au vinywaji ambavyo rafiki zako wanaahidi vitakusaidia utimize lengo lako haraka zaidi. Jarida American Academy of Family Physicians linasema: “Vijana milioni moja hivi [nchini Marekani] walio na umri wa kati ya miaka 12 na 17 wametumia dawa zinazoongeza nguvu mwilini.”

Mojawapo ya dawa maarufu zaidi zinazoongeza nguvu mwilini ni steroidi ambazo huongeza ukubwa wa misuli. Hizo ni dawa za aina gani? Kwa nini watu huzitumia? Na unawezaje kuepuka kishawishi cha kuzitumia?

Kuboresha Uwezo wa Asili

Ripoti moja ya Wizara ya Afya na Huduma za Jamii ya Marekani ilieleza hivi: “Dawa za steroidi za kuongeza ukubwa wa misuli ni kemikali zinazohusiana na homoni za kiume (androgens). Dawa hizo huchochea ukuzi wa misuli ya kiunzi na kusitawi kwa maumbile ya kiume.” Wavulana wanapobalehe homoni hizo huongezeka na kubadilika na hivyo kuchochea mabadiliko ambayo humfanya mvulana awe mwanamume.—Zaburi 139:15, 16.

Steroidi zilitengenezwa viwandani kwa mara ya kwanza katika miaka ya 1930 ili kuwatibu wanaume ambao walishindwa kutokeza homoni za kutosha. Leo, steroidi hutumiwa kurekebisha kudhoofika kwa mwili kunakosababishwa na virusi vya UKIMWI na magonjwa mengine. Hata hivyo, steroidi hutumiwa sana na watu wasio na uhitaji wa kitiba. Katika miaka ya 1950, steroidi zilianza kupatikana kimagendo, na wana-michezo waliojitakia sifa walianza kuzitumia kuongeza nguvu mwilini.

Hata hivyo, si wana-michezo tu ambao hushawishiwa kutumia steroidi. Uchunguzi uliochapishwa katika jarida la kitiba Pediatrics unakadiria kwamba karibu asilimia 3 ya wavulana na wasichana nchini Marekani walio na umri wa miaka 9 hadi 13 wametumia dawa hizo. Hivi majuzi, Dakt. Nora D. Volkow, mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Dawa za Kulevya, aliambia kikao kimoja kilichoteuliwa na bunge la Marekani kwamba mnamo 2004 “inakadiriwa kwamba wanafunzi 79,000 hivi wa shule ya sekondari [walikiri] kutumia vibaya dawa za kuongeza ukubwa wa misuli mwaka uliotangulia.” Watu wengi pia hutumia steroidi huko Uingereza. Kichapo New Statesman kinasema: “Katika mwaka wa 2003, huko Merseyside na Cheshire watu waliotumia steroidi ndio waliokuwa wengi katika programu ya kubadilishana sindano zilizotumiwa na kupewa mpya, na hata kwa mara ya kwanza walizidi watumizi wa heroin.” *

Kwa Nini Watu Huvutiwa na Steroidi?

Kwa nini watu wengi zaidi wanatumia vibaya steroidi? Sababu moja ni kwamba wana-michezo wazuri wanaweza kupata sifa na utajiri haraka. Inaonekana kwamba steroidi zinaweza kumfanya mtu apate vitu hivyo haraka zaidi. Kocha mmoja maarufu alifunua waziwazi mtazamo ambao wengi huwa nao aliposema: “Hakuna jambo jingine muhimu isipokuwa kushinda.” Volkow, aliyetajwa awali, alisema: “Tunakabili maoni mabaya yanayozidi kuenea katika jamii yetu, kwamba kuwa na misuli mikubwa ni muhimu sana, na kuwa namba moja ni muhimu bila kujali mbinu ulizotumia.”

Inaonekana kwamba uchunguzi uliofanywa na Bob Goldman, daktari anayeshughulika na majeraha yanayosababishwa na michezo, unathibitisha jambo hilo lenye kuhuzunisha. Aliwauliza wana-michezo vijana ikiwa wangetumia dawa za kuongeza nguvu chini ya hali zifuatazo: Hawangekamatwa, wangeshinda mashindano yote kwa miaka mitano ijayo na baadaye, wangekufa kutokana na madhara ya dawa hizo. Zaidi ya nusu ya vijana hao walisema wangezitumia.

Hata ikiwa hujaathiriwa na maoni ya kupata ushindi kupitia njia yoyote ile, huenda ukavutiwa na steroidi. Kwa nini? Volkow anasema: “Watu huamua kutumia steroidi kwa sababu, kwa kweli, hizo huboresha utendaji fulani wa mwili na sura.” Katika tamaduni nyingi leo, sura ya mtu ndiyo jambo muhimu zaidi. Dakt. Harrison Pope, profesa wa magonjwa ya akili katika Chuo cha Kitiba cha Harvard, anadai hivi: “Mamilioni ya wanaume huaibika na kukosa ujasiri kwa sababu ya kukazia fikira jinsi wanavyoonekana.” Steroidi huwawezesha vijana wengi wajifanye kuwa wajasiri kwa sababu ya kuwa na mwili wenye misuli mikubwa.

Sababu hizo pia huwafanya wasichana wavutiwe na steroidi. Charles Yesalis, profesa wa afya na ukuzi wa wanadamu katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Pennsylvania alisema hivi kuhusu matumizi mabaya ya steroidi: “Katika miaka ya 1990 wasichana walianza kuzitumia zaidi, na sasa wanazitumia kwa kiasi kikubwa zaidi.” Wasichana fulani hutumia steroidi ili wawe na nguvu na waboreshe uwezo wao wa kukimbia. Hata hivyo, inaonekana kwamba wengi wao hutumia dawa hizo wakitumaini zitawafanya wawe na maumbo membamba, yaliyo wima ambayo wanamitindo na waigizaji maarufu wa sinema leo hujivunia. Jeff Hoerger wa Chuo Kikuu cha Rutgers huko New Jersey, anasema, “wasichana huzitumia hasa kudhibiti uzito wao na [kama njia ya] kupunguza mafuta mwilini.”

Fikiria Hatari

Ukishawishiwa kutumia steroidi bila mwongozo wa daktari, ni muhimu kufikiria mambo yafuatayo. Mtu anayezitumia hata kwa muda mfupi anaongeza hatari ya kupatwa na mshtuko wa moyo, kuharibu ini na figo, na kupatwa na matatizo makubwa ya akili. Wanawake ambao hutumia steroidi wanakabili hatari ya kupatwa na matatizo ya hedhi, kuongezeka kwa nywele mwilini, kuwa na upara kama mwanamume, na kuwa na sauti nzito kabisa. Kwa upande mwingine, wanaume ambao hutumia steroidi wanaweza kutokeza matiti na huenda hata mapumbu yao yakaanza kuwa madogo. Wanaume na wanawake huanza kuwa wajeuri. Na kwa kushangaza, steroidi zinaweza kumfanya mtu asikue anapozitumia wakati wa kubalehe.

Ikiwa wewe ni kijana anayetaka kumpendeza Yehova Mungu, ni kanuni gani za Biblia zinazohusu matumizi mabaya ya steroidi? Biblia inasema wazi kwamba uhai wako ni zawadi kutoka kwa Yehova. (Matendo 17:25) Kama habari zilizotajwa zinavyoonyesha, kijana anayetumia steroidi anaweza kudhuru afya yake. Kwa hiyo, jiulize, “Je, ningekuwa nikimwonyesha Yehova kwamba ninathamini mwili wangu, ambao ‘umeumbwa kwa njia ya ajabu,’ ikiwa ningetumia vitu ambavyo mwishowe vingedhuru mwili kabisa?”—Zaburi 139:14.

Jambo jingine la kufikiria ni kwamba steroidi zinaweza kumfanya mtu awe na mwelekeo wa kukasirika upesi. Mfalme Sulemani mwenye hekima alisema: “Mtu yeyote mwenye mwelekeo wa ghadhabu ana makosa mengi.” (Methali 29:22) Mtume Paulo anaonya kwamba wale ambao huruhusu hasira iwaongoze hawataurithi Ufalme wa Mungu. (Wagalatia 5:19-21) Je, kuna haja ya kujihatarisha kwa steroidi ili tu kupata manufaa ya muda mfupi?

Unapaswa kufikiria nini unaposhawishiwa kutumia steroidi ili kuboresha uwezo wako katika michezo? Biblia inataka tujiendeshe “kwa unyoofu katika mambo yote.” (Waebrania 13:18) Ikiwa utafanikiwa katika michezo kwa sababu ya kutumia dawa za steroidi, je, wewe ni mnyoofu kuelekea wale unaoshindana nao au hata kwako mwenyewe?

Kumbuka kwamba hata ingawa huenda rafiki zako wakazingatia umbo lako au mambo unayotimiza, Yehova huwaona watu kwa njia tofauti. Kwa maoni yake, thamani yako haitegemei umbo la mwili wako. Alipokuwa akimchagua Daudi awe mfalme wa Israeli, Yehova alimwambia hivi Samweli kuhusu ndugu ya Daudi mwenye umbo zuri: “Usiangalie sura yake wala urefu wa umbo lake, kwa maana nimemkataa. Kwa kuwa Mungu haoni kama mwanadamu anavyoona, kwa maana mwanadamu huona kile kinachoonekana kwa macho, lakini Yehova huona jinsi moyo ulivyo.”—1 Samweli 16:7.

Iwe wewe ni mtumishi wa Yehova au la, ni jambo la hekima kuepuka kushawishiwa kutumia steroidi. Mchezaji wa mpira katika chuo huko Marekani anatoa shauri hili linalofaa: “Ukitaka kuepuka ushawishi wa kutumia steroidi, uwe mwangalifu kuhusu watu unaoshirikiana nao. ‘Manufaa’ yoyote unayopata kwa kutumia dawa za steroidi ni udanganyo mtupu.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Mara nyingi steroidi huingizwa mwilini kupitia sindano, na hivyo kuongeza uwezekano wa kuambukizwa virusi vya UKIMWI na magonjwa mengine yanayoambukizwa kupitia damu kati ya watu wanaotumia sindano moja.

[Picha katika ukurasa wa 20]

Wasichana fulani hutumia steroidi ili kubadili umbo lao