Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ufalme Uliotetea Uhuru wa Kidini Kujapokuwa Upinzani

Ufalme Uliotetea Uhuru wa Kidini Kujapokuwa Upinzani

Ufalme Uliotetea Uhuru wa Kidini Kujapokuwa Upinzani

“KILA MTU ANAWEZA KUFUATA DINI ANAYOPENDA KWA HIARI YAKE, NA YUKO HURU KUWAUNGA MKONO WAHUBIRI WA DINI YAKE.”

IWAPO ungeombwa utaje wakati ambapo maneno hayo yaliandikwa, ungejibuje? Watu wengi wangesema kwamba maneno hayo ni sehemu ya katiba ya kisasa au sheria ya haki za binadamu.

Hata hivyo, huenda ukashangaa kujua kwamba tangazo hilo lilitolewa zaidi ya miaka 400 iliyopita—katika nchi ambayo iliruhusu dini mbalimbali kujapokuwa upinzani wa kidini ulimwenguni. Hiyo ilikuwa nchi gani? Kwanza, hebu tuchunguze historia fupi kuhusu jambo hilo.

Upinzani wa Kidini Ulikuwa Jambo la Kawaida

Upinzani wa kidini ulikuwa jambo la kawaida katika Zama za Kati (500-1500 W.K.), na uliongezeka zaidi katika karne ya 16. Dini ilichochea vita vyenye kuogopesha vilivyowaua watu wengi katika nchi kama Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, na Ujerumani. Kati ya mwaka wa 1520 na mwaka wa 1565, watu wapatao 3,000 waliuawa katika nchi za Magharibi zilizodai kuwa za Kikristo eti kwa sababu walikuwa waasi wa dini. Yaelekea mtu yeyote aliyepinga kanuni zilizokuwapo—hasa zile za kidini—angekabili upinzani.

Utatu—ile imani kwamba kuna watu watatu katika Mungu mmoja—ni fundisho la Kanisa Katoliki ambalo lilisababisha ubishi kwa muda mrefu. Mwanahistoria Earl Morse Wilbur anasema kwamba “wanatheolojia Wakatoliki katika Zama za Kati, na hata Mapapa, walibishana sana kuhusu fundisho hilo.” Hata hivyo, mara nyingi watu wa kawaida hawakuhusika katika mijadala hiyo, kwani walipaswa tu kukubali mafundisho hayo bila uthibitisho na kuyaona kuwa “siri za Mungu.”

Lakini, watu fulani katika karne ya 16 walikataa maoni hayo na wakaamua kuchunguza Maandiko ili kuelewa siri hizo waziwazi. Wito wao ulikuwa sola Scriptura (Maandiko peke yake). Mara nyingi, wale waliopinga fundisho la Utatu walinyanyaswa vikali na Wakatoliki na Waprotestanti. Baadaye, baadhi yao waliitwa wapinzani wa Utatu. Walichapa vitabu ambavyo vilisomwa na watu wengi huku wakitumia majina bandia, na walijificha ili kuepuka mnyanyaso. Pia, wapinzani wa Utatu walipigania sana uhuru wa kidini. Baadhi yao, kama vile mwanatheolojia Mhispania Michael Servetus, waliuawa kwa sababu ya imani yao. *

Waliunganishwa na Uhuru wa Kidini

Badala ya kupinga dini au kuwanyanyasa watu wenye maoni tofauti, nchi moja ilifanya mambo kwa njia nyingine. Nchi hiyo iliitwa Transylvania, na sasa eneo hilo ni sehemu ya Rumania katika Ulaya Mashariki. Wakati huo eneo hilo lilitawaliwa na mwana-mfalme. Mwanahistoria Mhungaria Katalin Péter anaeleza kwamba Malkia Isabella, aliyerithi cheo cha mumewe, “alijaribu kuepuka migogoro ya kidini kwa kutetea dini zote.” Kati ya mwaka wa 1544 na 1574, Bunge la Transylvania lilipitisha sheria 22 zilizoruhusu uhuru wa kidini.

Kwa mfano, baada ya kikao cha Bunge la Torda mnamo mwaka wa 1557, malkia na mwanawe, waliamuru kwamba “kila mtu [anaweza] kufuata dini yoyote anayopenda, iwe ina desturi za zamani au mpya, na Sisi tunawaruhusu watu kuamua jinsi wanavyopenda kuhusiana na dini, maadamu tu, hawatamdhuru mtu yeyote.” Imesemekana kwamba hiyo ndiyo “sheria ya kwanza kabisa kutungwa katika nchi yoyote ili kuhakikisha uhuru wa kidini.” Uhuru wa kidini ulifikia kilele huko Transylvania wakati mwana wa Isabella, John wa Pili Sigismund, alipoanza kutawala mnamo mwaka wa 1559.

Mjadala wa Hadharani

Daktari mmoja Mwitaliano aliyeitwa Georgio Biandrata ni mtu mwingine aliyeshiriki sana katika harakati za kupinga Utatu. Huenda ikawa alianza kushuku fundisho la Utatu wakati alipokuwa Italia na Uswisi, ambako wapinzani wengi wa Utatu walikimbilia. Alipohamia Poland, Biandrata alijitahidi sana kuunga mkono lile Kanisa Dogo, ambalo baadaye liliitwa Ndugu wa Poland. * Mnamo mwaka wa 1563, aliteuliwa kuwa daktari na mshauri wa Sigismund na akahamia Transylvania.

Mtu mwingine mwenye elimu huko Transylvania aliyepinga Utatu alikuwa Francis Dávid, mwangalizi wa Kanisa la Reformed na mhubiri kwenye makao ya mfalme. Aliandika hivi kuhusu mafundisho magumu yaliyohusiana na Utatu: “Iwapo mambo haya ni ya lazima ili mtu apate wokovu, ni dhahiri kwamba hakuna Mkristo wa hali ya chini ambaye ameokolewa, kwa sababu hawezi kamwe kuyaelewa katika maisha yake yote.” Dávid na Biandrata walichapisha kitabu chenye maandishi kadhaa ya Servetus. Walikichapisha kwa heshima ya Sigismund.

Mabishano kuhusu Utatu yalianza kupamba moto, na watu wakaitisha mjadala wa hadharani kuhusiana na suala hilo. Kupatana na ile kanuni ya sola Scriptura, Biandrata alisema kwamba maoni ya Kimaandiko peke yake, wala si ya kifalsafa, ndiyo yanayopasa kutolewa kwenye mijadala hiyo. Baada ya mjadala ambao haukufikia mkataa wowote kufanywa mwaka wa 1566, Sigismund aliwapa wapinzani wa Utatu mashine ya uchapishaji ili wasambaze maoni yao.

Biandrata na Dávid walianza kufanya kazi hiyo kwa bidii na wakachapisha kitabu De falsa et vera unius Dei Patris, Filii, et Spiritus Sancti cognitione (Ujuzi wa Uwongo na wa Kweli Kuhusu Umoja wa Mungu Baba, Mwana, na Roho Takatifu). Kitabu hicho kilieleza historia ya watu waliokataa kuamini Utatu. Sura moja ilikuwa na picha za Utatu ambazo zilichorwa ili kudhihaki jinsi makanisa mbalimbali yalivyofundisha Utatu. Watu walioamini Utatu walichukizwa, wakasema kwamba picha hizo zinaudhi, na wakajaribu kuharibu nakala zote. Mazungumzo yakachacha kwa sababu ya kitabu hicho kilichozusha ubishi. Hivyo, Sigismund akapanga mjadala wa pili.

Waamini wa Mungu Mmoja Washinda

Mjadala huo ulianza saa kumi na moja alfajiri mnamo Machi 3, 1568. Ulifanywa katika Kilatini na uliendelea kwa muda wa siku kumi. Waamini wa Utatu waliongozwa na Peter Melius, kiongozi wa Kanisa la Reformed la Transylvania. Yeye na wale waliotetea Utatu walitumia kanuni za imani, maandishi ya Mababa wa Kanisa, theolojia ya Othodoksi, na Biblia. Kwa upande mwingine, Dávid alitumia Biblia peke yake. Dávid alimtambulisha Baba kuwa Mungu, Mwana kuwa chini ya Baba, na roho kuwa nguvu ya Mungu. Sigismund alishiriki katika mjadala huo, kwani alipendezwa sana na mambo ya dini na aliamini kwamba mazungumzo ndiyo njia bora ya kupata ukweli. Kuwepo kwake kuliwawezesha washiriki kusema waziwazi na kwa uhuru, japo mazungumzo yalikuwa motomoto.

Ilionekana kwamba wapinzani wa Utatu walishinda. Dávid alikaribishwa kwa vifijo na nderemo aliporudi katika mji wa kwao huko Kolozsvár (ambao sasa unaitwa Cluj-Napoca, Rumania). Yasemekana kwamba alipowasili, alisimama juu ya jiwe kubwa pembeni mwa barabara na kuzungumza kuhusu imani yake kwa usadikisho sana hivi kwamba aliwashawishi watu wote kuamini mafundisho yake.

Kugeuzwa Imani na Kifo

Hapo awali mijadala ilifanywa katika Kilatini, lugha iliyoeleweka tu na watu wenye elimu. Hata hivyo, Dávid alitaka watu wa kawaida wasikie ujumbe wake. Kwa hiyo, Sigismund alikubali kwamba mjadala uliofuata ufanywe katika Kihungaria kwenye jiji la Nagyvárad (ambalo sasa linaitwa Oradea, Rumania) mnamo Oktoba 20, 1569. Kwa mara nyingine tena, Sigismund aliongoza mazungumzo baina ya pande hizo mbili.

Yule mwamini wa Utatu Peter Melius alitangaza kwamba katika njozi aliyoona usiku uliotangulia, Bwana alimfunulia jinsi alivyo kikweli. Mfalme akajibu: “Kasisi Peter, iwapo jana usiku tu ndipo ulipofunuliwa jinsi Mwana wa Mungu alivyo, basi nakuuliza, umekuwa ukihubiri juu ya nini hapo awali? Ni wazi kwamba hadi kufikia sasa umekuwa ukiwadanganya watu!” Melius alipomshambulia Dávid kwa maneno makali, Sigismund alimkemea mwamini huyo wa Utatu na kumkumbusha kwamba “imani ni zawadi kutoka kwa Mungu” na kwamba “dhamiri ya mtu haiwezi kulazimishwa.” Alipotoa hotuba ya kumaliza mjadala huo, mfalme alisema hivi: “Tunaamuru kwamba kuwe na uhuru wa dhamiri katika milki zetu.”

Baada ya mjadala huo, Sigismund na maafisa wake wengi walishawishiwa kujiunga na wapinzani wa Utatu. Mnamo mwaka wa 1571, mfalme alitoa amri ambayo ilihalalisha Kanisa la wapinzani wa Utatu. Ni katika Nchi ya Transylvania peke yake ndiko Wapinzani wa Utatu walikuwa sawa na Wakatoliki, Walutheri, na Wafuasi wa Calvin, na Sigismund ndiye mfalme mmoja tu anayejulikana kuwa alijiunga na dini ya wapinzani wa Utatu. Kwa kusikitisha, muda mfupi baadaye, mfalme huyo mwenye umri wa miaka 30 alijeruhiwa alipokuwa amekwenda kuwinda pamoja na Dávid na Biandrata, na akafa miezi kadhaa baadaye.

Mwandamizi wake, Mkatoliki Stephen Báthory, alikazia tena ile amri iliyokubali dini zilizohalalishwa lakini akasema kwamba hangekubali mabadiliko mengine. Mwanzoni, Stephen alisema kwamba aliwatawala watu, bali si dhamiri zao. Lakini punde akapiga marufuku uchapaji wa vitabu—njia kuu ya kueneza imani. Dávid akapoteza wadhifa wake, na wapinzani wengine wa Utatu wakapoteza madaraka yao katika makao ya mfalme na serikalini.

Dávid alipoanza kufundisha kwamba Kristo hapaswi kuabudiwa, amri ilitolewa ili kumkataza kuhubiri. Licha ya marufuku hayo, Dávid alihubiri mara mbili Jumapili iliyofuata. Alikamatwa, akashtakiwa kwa madai ya “kutunga” mafundisho ya kidini, na akahukumiwa kifungo cha maisha. Alikufa mnamo mwaka wa 1579 katika gereza la jumba la mfalme lililokuwa chini ya ardhi. Kabla ya kufa, Dávid aliandika maneno haya kwenye ukuta wa gereza hilo: “Wala upanga wa mapapa . . . wala tisho la kifo halitazuia maendeleo ya ukweli. . . . Nina uhakika kwamba baada ya kifo changu mafundisho ya manabii wa uwongo yatatokomea.”

Masomo Tunayojifunza Kutoka kwa Mfalme

Mfalme John Sigismund aliendeleza elimu, muziki, na sanaa. Hata hivyo, maisha yake yalikuwa mafupi, na alikuwa mgonjwa mara nyingi. Wakati wa utawala wake alitishwa na watu wa nchi yake—angalau kulikuwa na njama tisa za kumwua. Pia, mataifa ya kigeni yalichochea uasi. Mfalme huyo aliyeruhusu dini mbalimbali ameshutumiwa vikali mara nyingi kwa sababu ya maoni yake ya kidini. Mpinzani mmoja alisema hivi baadaye: “Bila shaka [mfalme huyo] alikwenda motoni.”

Hata hivyo, mwanahistoria Wilbur, anaeleza mambo ifaavyo: “Katika mwaka ambao Mfalme John [Sigismund] alitoa uhuru kamili wa ibada kwa mara ya mwisho hata kwa yale madhehebu ya Kiprotestanti ambayo yalipingwa vikali, wanatheolojia Waprotestanti bado walikuwa wakimsifu Calvin kwa sababu alimteketeza Servetus akiwa hai, Baraza la Kuwahukumu Waasi lilikuwa likiwaua Waprotestanti nchini Uholanzi, . . . na zaidi ya miaka 40 ingepita kabla ya kukomeshwa kwa zoea la kuwateketeza kwenye mti watu wenye maoni tofauti ya kidini huko Uingereza.”

Kwa kweli, kama vile msimulizi mmoja alivyosema, “unapomlinganisha na watawala wa kipindi chochote kile—na hasa wa kipindi chake—Mfalme John Sigismund alikuwa mtawala wa pekee sana. . . . Jambo kuu katika utawala wake lilikuwa uhuru wa kidini.” Kwa kuwa alitambua kwamba amani ya kidini ingefaidi Serikali, alitetea kwa bidii uhuru wa dhamiri na wa kidini.

Kwa kuwa bado kuna upinzani wa kidini leo, twaweza kujifunza masomo muhimu kutokana na ufalme huo mdogo wa kale. Kwa muda mfupi, ufalme wa Transylvania ulitetea uhuru wa kidini kujapokuwa upinzani wa wakati huo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Ona gazeti la Amkeni!, Februari 8, 1990, ukurasa wa 15-18.

[Blabu katika ukurasa wa 14]

“Dhamiri ya mtu haiwezi kulazimishwa . . . tunaamuru kwamba kuwe na uhuru wa dhamiri katika milki zetu.”—Mfalme John wa Pili Sigismund

[Picha katika ukurasa wa 12, 13]

Georgio Biandrata

Kurasa za kitabu kilichochapishwa na Biandrata na Dávid, kutia ndani picha mbili zilizowachukiza waamini wa Utatu

Francis Dávid mbele ya Bunge la Torda

[Hisani]

Michoro miwili ya Utatu: © Cliché Bibliothèque nationale de France, Paris; picha nyingine zote: Országos Széchényi Könyvtár

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]

Ukurasa wa 2 na wa 14: Országos Széchényi Könyvtár