Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kundi la Pekee la Ng’ombe-Mwitu Weupe

Kundi la Pekee la Ng’ombe-Mwitu Weupe

Kundi la Pekee la Ng’ombe-Mwitu Weupe

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

MBUGA YA CHILLINGHAM, iliyoko katika mkoa wa Northumberland unaopakana na Scotland, ni makao ya kundi dogo la ng’ombe-mwitu weupe. Kila mwaka watu kutoka mbali huja kuwatazama ng’ombe hao. Kwa nini? Kwa sababu wanyama hao ni wa pekee sana. Leo, mimi na mke wangu tumekuja kuwatazama ng’ombe hao.

Inadhaniwa kwamba ng’ombe hao wamekuwa katika Mbuga ya Chillingham tangu miaka ya 1200. Wakati huo, ukuta uliozunguka mbuga hiyo yenye eneo la ekari 1,500 ulijengwa ili kuwafungia ng’ombe-mwitu kwa ajili ya chakula. Siku hizi, wanyama hao wa pekee wanaishi kwenye eneo la ekari 350 la mbuga hiyo. Ng’ombe hao wote wana masikio mekundu, miguu myeusi, na vichwa vyenye madoa-madoa. Madoa-madoa hayo hutokea wanapofikia umri wa miaka miwili hivi na huenea hatua kwa hatua kwenye shingo na mabega.

Hakuna kati ya ng’ombe hao ambaye ana rangi nyingine. Inasemekana kwamba hawajajamiiana kamwe na ng’ombe wanaofugwa, nao ni tofauti na ng’ombe wengine 1,000 hivi wa Mbuga ya Chillingham, ambao siku hizi wanaweza kupatikana katika makundi madogo-madogo kotekote Uingereza na Amerika Kaskazini. Uchunguzi unaonyesha kwamba damu ya ng’ombe wa kundi hili ni tofauti na damu ya ng’ombe wengine wa Ulaya Magharibi.

Pembe za fahali zinajipinda kuelekea mbele, lakini pembe za ng’ombe-jike zinaelekea nyuma. Umbo la kichwa na pembe linafanana na lile la ng’ombe-mwitu wa kale kabisa waliochorwa katika kuta za mapango huko Ulaya ambao wametoweka. Baadhi ya wataalamu wanadhani kwamba ng’ombe wa Chillingham walitokana na ng’ombe-mwitu walioishi kwenye Visiwa vya Uingereza. Hata hivyo, asili yao haijulikani.

Ng’ombe Anayeongoza

Ili tuweze kuwatazama wanyama hao kwa ukaribu, tunaingia katika gari la msimamizi wa kundi moja la ng’ombe hao. Tunasafiri kwa mwendo wa kasi kwenye malisho yenye mashimo-mashimo, na ghafula tunawaona wanyama hao wakijikinga na jua chini ya miti kadhaa. Wengine wao wanatutazama, kama ambavyo ng’ombe huzoea kufanya. Wawili au watatu wanatukaribia polepole na kusugua pembe zao kubwa kwenye gari.

Msimamizi anatuonyesha kiongozi wa kundi hilo, ambaye anajulikana kama fahali mfalme. Huyo fahali ana nguvu nyingi na afya bora kushinda fahali wengine. Wakati wa “utawala” wake, unaoendelea kwa muda wa miaka mitatu hivi, yeye ndiye huwa baba wa ndama wote. Kwa njia hiyo, yaelekea kwamba mwaka baada ya mwaka ndama wanaozaliwa huwa na nguvu na afya bora. Hakuna fahali anayeruhusiwa kujamiiana na uzao wake mwenyewe, na hakuna mwana anayeandama baba yake kama fahali anayezalisha.

Tabia za Kisilika

Zamani, mbwa-mwitu alikuwa adui mkuu wa wanyama hao, na aliwawinda hasa wanyama dhaifu. Hata hivyo, mbwa-mwitu alitoweka huko Uingereza katika miaka ya 1500. Nyakati nyingine ng’ombe hao hutimua mbio wakitishwa, na wanaposimama hatimaye, fahali hujipanga katika duara wakiwazingira ng’ombe-jike na ndama ili wasishambuliwe na mnyama mwindaji yeyote.

Ng’ombe hao ni wanyama-mwitu kwelikweli. Kwa hiyo, haiwezekani kuwatunza kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo. Hata wakati ambapo nyasi haipatikani katika majira ya baridi kali, wao hula tu nyasi-kavu na mabua. Wao hawali kamwe nafaka na vyakula vya pekee vya ng’ombe. Kwa sababu ndama ni wadogo wanapozaliwa, kwa kawaida ng’ombe-jike huzaa bila matatizo, lakini kama tatizo la kuzaa lingetokea, daktari wa mifugo hataweza kusaidia. Inadhaniwa kwamba kama mmojawapo wa wanyama hao angeguswa na mwanadamu, mnyama huyo angeweza kuuawa na wanyama wengine kundini.

Ng’ombe-jike huzaa wakiwa mbali na kundi, nao huwaficha ndama kwa juma moja hivi. Baadaye, mama na ndama hukaribia kundi, na fahali mfalme huwaendea na kuwasindikiza hadi kundini. Kisha, ng’ombe-jike wengine humnusa-nusa ndama na kumchunguza kabla hajakubaliwa kundini. Baada ya hapo, hatachunguzwa tena.

Mwaka wa 1967, mifugo wengi waliokuwa kilometa nne tu kutoka Mbuga ya Chillingham waliambukizwa ugonjwa wa mguu na mdomo. Mbuga hiyo ilifungwa mara moja na kundi hilo halikuambukizwa. Baadaye ikaamuliwa kwamba ng’ombe wachache wapelekwe Scotland, ili ng’ombe hao wasitoweke kabisa endapo kundi la awali lingepatwa na madhara. Kwa sababu ng’ombe wote wa kundi hilo jipya walihamishwa pamoja, hakuna mmoja wao aliyefukuzwa kundini.

Tumefurahia safari yetu fupi ya kwenda kuwaona ng’ombe-mwitu weupe na kujifunza kuhusu asili yao. Siku moja huenda ukaweza kutembea na kujionea mwenyewe wanyama hao wa pekee katika makao yao matulivu.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 27]

Courtesy Chillingham Wild Cattle Association ▼

Loaned by courtesy of Lawrence Alderson