Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Macho Yasiyo na Oksijeni

Baadhi ya watu wanaovaa lenzi zinazoambatanishwa na mboni yaelekea wanazuia macho yao kupata oksijeni, laripoti gazeti la The Globe and Mail. “Mishipa mingi ya damu huibuka kwa sababu konea [utando wa jicho] haiwezi kupata oksijeni inayohitajiwa kutoka kwa hewa na hivyo mishipa ya damu huanza kukua ili kujazia upungufu huo.” Hali hiyo yaweza kusababisha kasoro za kuona au hata upofu. Dakt. Raymond Stein, msimamizi wa utaalamu wa magonjwa ya macho katika hospitali moja ya Toronto, asema kwamba “hatari kubwa zaidi huzuka wakati mgonjwa anaposhindwa kutunza lenzi zake na anapokosa kwenda kupimwa macho.” Wapimaji wa macho huwatia moyo wagonjwa wamfikie mtaalamu wa utunzaji wa macho ili kuhakikisha kwamba wana lenzi za kuambatanishwa na mboni zinazofaa macho yao hasa kisha wafuate ratiba iliyopendekezwa ya kuvaa na kutunza lenzi hizo.

Urafiki Waporomoka Brazili

Wabrazili sasa hawasitawishi urafiki sana kama walivyofanya miaka 10 iliyopita, laripoti gazeti la O Globo. Kulingana na mtaalamu wa afya ya akili Maria Abigail de Souza wa Chuo Kikuu cha São Paulo, ugumu wa kupata kazi, jitihada ya kudumisha mtindo fulani wa maisha, na wakati haba wa mapumziko ni mambo yanayochangia. César Vasconcelos de Souza, mkurugenzi wa tiba katika Adventist Healthy Life Center, São Paulo, asema hivi: “Ili kuwa na marafiki wa kweli, ni sharti kuelezana hisia zetu, tuseme ya moyoni, na kueleza mambo ya kufurahisha na ya kuhuzunisha yaliyo moyoni, yaliyo magumu kueleza na yasiyo magumu kueleza. Hilo huhitaji muda na kuimarishwa kwa vifungo vya kihisia-moyo. Watu wengi wangependa kushiriki hisia zao na wengine lakini wanahofu kufanya hivyo. Ili kuepuka hatari wanapendelea urafiki wa kijuu-juu tu.”

Kuhuzunika na Kushuka Moyo

Uchunguzi wa wanaume na wanawake wenye umri wa kati ya miaka 70 na 79 waonyesha kwamba wajane fulani wanawake na wanaume huwa na dalili mbaya sana za kushuka moyo kwa muda wa miaka miwili hivi baada ya kufiwa na mwenzi wao. Wale waliochunguzwa waligawanywa katika vikundi sita, ikitegemea muda uliopita tangu kufiwa na mwenzi wao. Mahoji na maswali yalitumiwa kupima dalili za kushuka moyo. Kati ya waliohojiwa, asilimia 38 walikuwa wanaume, na asilimia 62 walikuwa wanawake. Uchunguzi huo uligundua kwamba kiwango cha kushuka moyo miongoni mwa wale waliofiwa karibuni ni mara tisa zaidi ya wale waliofunga ndoa ambao hawakuwa wamefiwa.

Waraibu wa Ponografia Kwenye Internet

Watafiti wamegundua kwamba “angalau wateja 200,000 wa Internet ni waraibu wa vituo vya ponografia, vituo vya maongezi machafu sana au wa habari nyinginezo za ngono kwenye mtandao huo,” laripoti gazeti la The New York Times. Uchunguzi huo ulifanywa na wanasaikolojia katika vyuo vikuu vya Stanford na Duquesne na ni mojawapo ya uchunguzi wa kwanza kukadiria idadi ya “waraibu wa kutazama ngono kwenye Internet.” Watafiti hao walisema kwamba watu hao hutazama Vituo vyenye mambo machafu sana kwenye Internet zaidi ya saa 11 kwa juma. Gazeti hilo liliwanukuu watafiti hao wakisema hivi: “Hii ni hatari isiyoonekana kwa afya ya umma inayoongezeka kasi, kwa sehemu, ni kwa sababu si wengi wanaoiona kuwa hatari wala kulichukulia jambo hilo kwa uzito.”

UKIMWI Waangamiza Afrika

Mwaka uliopita, UKIMWI uliwaangamiza watu wengi zaidi katika Afrika kuliko wale waliouawa vitani, asema Kofi Annan, katibu-mkuu wa Umoja wa Mataifa. Hivyo vyatia ndani vita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sierra Leone, Angola, Jamhuri ya Kongo, Ethiopia, Somalia, Eritrea, na Sudan. Takriban thuluthi mbili ya wagonjwa milioni 36 wenye UKIMWI ulimwenguni huishi katika eneo lililo kusini mwa jangwa la Sahara katika Afrika. Nchini Côte d’Ivoire, mwalimu mmoja hufa kutokana na UKIMWI kila siku ya shule, na huko Botswana, tarajio la muda wa kuishi limeshuka kutoka miaka 70 hadi 41. Zimbabwe inatarajia kwamba kufikia mwaka wa 2005, UKIMWI utatumia asilimia 60 ya fedha zake za afya, na bado hizo hazitatosha. Masuala kuhusu UKIMWI huepukwa nchini Malawi na Zambia, ambako kiwango cha maambukizo kiko juu sana; na walioambukizwa UKIMWI huepukwa huko Afrika Kusini, laripoti gazeti la London The Guardian. “Hakuna nchi yoyote ambayo imeanza kupata athari kamili za tisho hilo—kuelekea hali ya maisha barani Afrika, uwezo wake wa kiuchumi na uthabiti wake wa kijamii na kisiasa,” akasema Bw. Annan.

Majiji Yabadili Tabia ya Nchi

“Ukuzi wa kasi wa majiji unatokeza ‘maeneo yenye joto kali’ sana kiasi cha kuanzisha mifumo tofauti kabisa ya halihewa,” laripoti gazeti la The Times la London. Majiji hayo hunasa joto wakati wa mchana na kulisambaza angani usiku. Ndiyo sababu halijoto ya majiji kama vile Beijing na Atlanta imeongezeka kwa nyuzi Selsiasi 5.5 au zaidi. Katika miaka 19 iliyopita, Atlanta imepoteza ekari 380,000 za misitu kwa ajili ya ujenzi wa barabara na nyumba. Kusitawi kwa majiji huzidisha uchafuzi wa hewa, husababisha mvua ya radi isiyo ya kawaida, na hupunguza uzalishaji wa mashamba wa usanidinuru. Akizungumzia athari za “maeneo hayo yenye joto kali,” Dakt. Marc Imhoff, mwanasayansi wa Shirika la National Aeronautics and Space Administration, alisema hivi: “Uhai wa mwanadamu unategemea uwezo wa ardhi wa kuzalisha chakula. Iwapo uwezo wa ardhi wa kuendeleza usanidinuru umepungua sana, basi uwezo wa dunia wa kutegemeza uhai wa mwanadamu hauna budi kudidimia pia.” Mara nyingi ni ardhi yenye rutuba ya kilimo inayoharibiwa kwa ajili ya upanuzi wa majiji.

Uchafuzi Wafaidi Nyangumi

Yamkini uchafuzi umechangia jitihada ya kuokoa nyangumi. Uchunguzi wa hivi karibuni umeonyesha kwamba nyangumi na pomboo waliovuliwa karibu na ufuo wa Japani wana kiasi kikubwa cha sumu ya DDT, dioxin, PCB, na methylmercury. Jaribio moja lilionyesha kwamba kula gramu 50 tu za nyama ya pomboo yenye sumu kwaweza kuhatarisha sana uhai wa mtu. Wengine wanatarajia kwamba, huenda habari hizo zikakomesha ulaji wa nyama ya nyangumi.

Yungiyungi “Wenye Kujisafisha”

Kwa nini mmea wa yungiyungi, ambao huonwa na dini za Mashariki kuwa mtakatifu, huonekana ukiwa safi daima? Wanasayansi Wajerumani sasa wanadai kwamba wamepata jawabu kwa swali hilo ambalo limewakanganya wanabiolojia kwa miaka mingi. “Kwa muda mrefu imejulikana kwamba maji huteleza juu ya mimea,” wasema wanasayansi W. Barthlott na C. Neinhuis. “Lakini uwezo wa kujisafisha wa mimea . . . umepuuzwa kabisa.” Kama inavyoelezwa kwenye gazeti la The Sunday Times of India, “matone ya maji yanayobingirika kwenye jani la yungiyungi hukusanya uchafu, na hivyo husafisha kabisa sehemu ya juu ya majani.” Si kwa sababu majani yake ni laini. Litazamwapo kwa hadubini, jani hilo huonekana likiwa na “mabonge, mikunjo na vitufe” vyenye “mbenuko au umbo la kuba linalomwaga maji.” Uwezo wa kukinza maji wa fuwele za nta zinazofunika mmea huo unachangia pia. Watafiti hao wasema kwamba “tabia [hiyo] ya yungiyungi” hupunguza kabisa unataji wa maji na chembe za uchafu, nao waongezea kwamba mmea huo waweza kutengeneza upya nta licha ya hali mbaya za mazingira. Wasema kwamba hilo hufanya yungiyungi uwe na uwezo wa asili wa kukinza maji ulio bora zaidi ya rangi zisizopenywa na maji au sabuni zilizotengenezwa na wanadamu.

Je, Ni Salama Kunywewa?

Uchunguzi uliofanywa na shirika la World Wide Fund for Nature (WWF) waonya kwamba “ni lazima hatua za usalama zichukuliwe” kabla maji ya Ufaransa hayajachafuka “kiasi cha kutoweza kusafishwa.” Kwa mujibu wa shirika la WWF, maji yaliyo ardhini na ya mabwawa nchini Ufaransa yanachafuliwa na dawa za kuulia wadudu na nitriti. Uchafuzi wa nitriti hutukia hasa wakati kinyesi cha nguruwe na ng’ombe kinapotumbukia majini. Ripoti hiyo yasema kwamba “kinyesi cha nguruwe wapatao milioni nane walio katika jimbo la Brittany chaweza kulinganishwa na uchafu utokao kwa jiji lisilokuwa na mifereji ya kuondoa maji machafu, lenye wakazi milioni 24!” Isitoshe, “kuenea kwa utiaji-mbolea kwenye mashamba makubwa” huchafua pia maji kwa nitriti, lasema shirika la WWF. Zaidi ya hayo, matumizi yaliyoenea sana ya dawa za kuulia wadudu katika kilimo cha mahindi yameongeza kiasi cha dawa hizo kwa zaidi ya asilimia 40 ya viwango vilivyowekwa. Ripoti ya WWF yapendekeza vinamasi na matuta yenye miti yajengwe ili viwe kama vichujio vya asili.