Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Nani Anayeongea?

Ni Nani Anayeongea?

Ni Nani Anayeongea?

PAZIA lafunguliwa kisha aibuka mtumbuizaji mmoja na mwanasesere wake. Wanapotaniana, mwanasesere huyo aonekana ni kama yuko hai, akiwa na sauti na utu halisi. Bila shaka, ni yule mtumbuizaji—mtaalamu wa kutoa sauti kana kwamba inatoka kwa mwingine (ventriloquist)—anayetoa “sauti” ya mwanasesere, daima akiwa mwangalifu kutosogeza midomo yake mwenyewe anapofanya hivyo.

Je, ungependa kujifunza zaidi kuhusu ustadi huu wa pekee? Amkeni! lilimhoji Nacho Estrada, ambaye amekuwa mtaalamu wa kutoa sauti kwa njia hiyo ya pekee kwa miaka 18 hivi.

Kuna namna zipi za utoaji-sauti?

Katika ule unaoitwa utoaji-sauti wa karibu, sauti ya mtumbuizaji husikika ni kama inatoka karibu, kama vile kutoka kwa mwanasesere aliyempakata. Katika utoaji-sauti wa mbali, sauti ya mtumbuizaji husikika ni kana kwamba inatoka mbali sana. Mtoaji-sauti aweza pia kugumia sauti yake hivi kwamba yaweza kusikika ni kama inatoka mahali palipofunikwa—labda ndani ya sanduku lililofunikwa. Watoaji-sauti fulani wanaweza kuiga sauti, kama vile sauti za wanyama au kilio cha mtoto mchanga. Nao hawasogezi midomo yao wanapotumbuiza.

Mtoaji-sauti hodari husadikisha kabisa. Yasemekana kwamba mtoaji-sauti mmoja alitoa kilio cha kuomba msaada kilichogumiwa wakati mkokoteni uliojaa nyasi kavu ulipokuwa ukipita. Kwa kweli watu walisimamisha mkokoteni huo na kupakua hizo nyasi kavu, wakitarajia kumkuta mtu fulani aliyefichwa ndani yake! Bila shaka, hawakumkuta yeyote.

Utoaji-sauti umesitawije katika miaka iliyopita?

Yaaminika kwamba miaka mingi iliyopita utoaji-sauti ulitumiwa kuwahadaa watu washirikina waamini kwamba walikuwa wakiwasiliana na wafu. Baada ya muda, utoaji-sauti ulifunuliwa kuwa ustadi tu wa wanadamu. Baada ya hapo ukaja kuwa mashuhuri katika uwanja wa vitumbuizo, na leo hutumiwa nyakati nyingine kwa kusudi la kuelimisha.

Katika karne zilizopita hali mbalimbali zimetumiwa ili kuwachekesha watazamaji na kuonyesha ustadi wa pekee wa watoaji-sauti. Kufikia karne ya 20, watoaji-sauti walipenda sana kuzungumza na wanasesere wa mbao.

Ni nini kilichokuchochea upendezwe na utoaji-sauti?

Nilivutiwa na uwezo wake wa kuwafurahisha na kuwachekesha watu. Nilipokuwa kivulana, mchuuzi mmoja alichochea upendezi wangu kwa ustadi huo kwa kunieleza kuwa neno “ventriloquist” latokana na maneno ya Kilatini venter na loqui, yanayomaanisha “kuongea kwa tumbo” au “kuongea kutoka tumboni.” Hiyo ni kwa sababu hapo awali ilidhaniwa kwamba utoaji-sauti (ventriloquism) ulitokana na matumizi ya ajabu ya tumbo. Kisha akanionyesha baadhi ya mambo ya msingi.

Siku iliyofuata nilijaribu ustadi huo shuleni. Huku nikitumia mbinu ya utoaji-sauti wa mbali, nilifanya sauti yangu isikike ni kana kwamba ilikuwa ikitoka kwa mfumo wa kupaaza sauti, nami nikajiita kutoka darasani. Nilifaulu! Baadaye, nilijifunza mengi kuhusu utoaji-sauti huo kupitia kwa mtalaa wa elimu kwa njia ya posta kisha nikaanza kuifanya kazi hiyo.

Kazi yako ukiwa mtoaji-sauti huhusisha nini?

Ijapokuwa mara kwa mara nimewatumbuiza watu katika sherehe na maonyesho ya watoaji-sauti na hata mara kadhaa nimekuwa na maonyesho kwenye televisheni, mimi hutumia wakati wangu mwingi kuwafundisha watoto kwenye mikutano shuleni. Uchekeshaji hutimiza fungu muhimu katika maonyesho hayo. Kwa mfano, katika kipindi kinachohusu usafi wa kimwili, namwambia Maclovio, mwanasesere wangu wa mbao, kwamba kwa sababu hakupiga meno yake mswaki, naweza kuona kuwa alikula mayai wakati wa kiamsha kinywa asubuhi hiyo. Maclovio anajibu, “Umekosea—nilikula jana!”

Utoaji-sauti hufanywaje?

Kwa kawaida yasemekana kwamba mtoaji-sauti hurusha sauti yake, lakini huo ni uwongo tu. Sisi hupinda ulimi kwa njia ya pekee ili kutokeza sauti mbalimbali kwa herufi zinazohitaji mdomo usogee, na mbinu ya kupumua kutoka kwa kiwambo cha moyo huashiria umbali wa bandia.

Utoaji-sauti hufaulu kwa sababu watu wengi hawajazoeza masikio yao kutambua chanzo na umbali wa sauti. Wanahitaji kutazama ili kutambua. Kwa kielelezo: Unaposikia tu sauti ya king’ora, masikio yako hukufanya ufikiri kuwa gari la dharura linakaribia na kwamba linatoka mbali sana. Lakini gari hilo liko umbali gani? Linakuja kutoka upande gani? Ili kujibu maswali hayo, yamkini utahitaji kutazama taa zenye kumweka-mweka za gari hilo.

Mtoaji-sauti hutumia vyema hali hiyo kwa kutokeza sauti ya kiasi kinachofaa na kwa kuelekeza uangalifu wa wasikilizaji kwa chanzo ambacho yeye anataka wafikiri kinatoa sauti hiyo.

Waweza kumpa madokezo gani mtu anayependezwa kujifunza ustadi wa kutoa-sauti?

Kwanza, fahamu kusudi lako, na uwe tayari kuepuka kikwazo chochote. Nasema hivyo kwa sababu sawa na utumbuizaji mwingine mwingi, utoaji-sauti hutumiwa nyakati nyingine kwa makusudi mabaya. Mimi binafsi, huvutiwa na utoaji-sauti kwa sababu ya uwezo wake wa kuchochea upendo na kuleta burudani. Kazi yangu huhusisha mazungumzo na matukio yanayotimiza kusudi hilo peke yake.

Ili kuwa bingwa katika utoaji-sauti, utahitaji mambo matatu—mbinu, ubunifu, na mazoezi. Waweza kujifunza mbinu kutokana na kitabu chenye maagizo na mashauri au vidio. Kisha, tumia ubunifu wako kutokeza utu halisi wa mwanasesere wako au karagosi, na ujifunze jinsi uwezavyo kumfanya aonekane ni kana kwamba yu hai. Hatimaye, fanya mazoezi. Ustadi utakaokuwa nao utategemea jitihada ya kufanya mambo hayo.