Marko 16:1-20

16  Kwa hiyo siku ya sabato+ ilipokuwa imepita, Maria Magdalene,+ na Maria mama ya Yakobo, na Salome wakanunua manukato kusudi waje kumpaka.+  Na mapema sana siku ya kwanza+ ya juma wakaja kwenye kaburi, jua lilipokuwa limechomoza.+  Nao walikuwa wakisemezana: “Ni nani atakayetuviringishia lile jiwe kutoka kwenye mlango wa kaburi?”  Lakini walipotazama juu, wakaona kwamba jiwe lilikuwa limeviringishwa, ijapokuwa lilikuwa kubwa sana.+  Walipoingia ndani ya kaburi, wakaona kijana ameketi upande wa kuume akiwa amevaa kanzu nyeupe, nao wakafadhaika.+  Akawaambia: “Acheni kufadhaika. Mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyetundikwa mtini.+ Alifufuliwa,+ hayupo hapa. Tazameni! Mahali walipomlaza.+  Lakini nendeni, mkawaambie wanafunzi wake na Petro, ‘Yeye anawatangulia kuingia Galilaya;+ huko mtamwona, kama vile alivyowaambia ninyi.’ ”+  Kwa hiyo walipotoka wakakimbia kutoka kwenye kaburi, kwa maana walikuwa wakitetemeka nao walikuwa na hisia nyingi. Nao hawakumwambia mtu jambo lolote, kwa maana walikuwa wanaogopa.+ UMALIZIO MFUPI Hati na tafsiri fulani za mwisho-mwisho zina umalizio mfupi baada ya Marko 16:​8, kama ifuatavyo: Lakini mambo yote yaliyokuwa yameamriwa wakayasimulia kwa ufupi kwa wale waliomzunguka Petro. Tena, baada ya mambo hayo, Yesu mwenyewe akapeleka kupitia wao tangazo takatifu na lisiloweza kuharibika la wokovu wa milele kutoka mashariki mpaka magharibi. UMALIZIO MREFU Hati nyingine za kale (Codex Alexandrinus, Codex Ephraemi, Codex Bezae) na tafsiri (Latin Vulgate, Curetonian Syriac, Syriac Peshitta) huongeza umalizio mrefu unaofuata, lakini ambao Codex Sinaiticus, Codex Vaticanus, Sinaitic Syriac codex, na Armenian Version huondoa:  Baada ya kufufuka mapema siku ya kwanza ya juma akamtokea kwanza Maria Magdalene, ambaye alikuwa amefukuza roho waovu saba kutoka kwake. 10  Maria Magdalene akaenda, akawaambia wale waliokuwa wamekuwa pamoja na Yesu, kwa maana walikuwa wakiomboleza na kulia. 11  Lakini wao, waliposikia alikuwa amefufuka na Maria Magdalene alikuwa amemwona, hawakuamini. 12  Tena, baada ya mambo hayo aliwatokea katika umbo lingine wawili kati yao wakitembea, walipokuwa wakienda mashambani; 13  nao wakarudi wakawaambia wale wengine. Wala hawakuwaamini. 14  Lakini baadaye akawatokea wale kumi na mmoja wenyewe walipokuwa wameketi mezani, naye akaushutumu ukosefu wao wa imani na ugumu wa moyo, kwa sababu hawakuwaamini wale waliokuwa wamemwona sasa akiwa amefufuka kutoka kwa wafu. 15  Naye akawaambia: “Nendeni, mkaingie katika ulimwengu wote na kuhubiri habari njema kwa uumbaji wote. 16  Yeye anayeamini na kubatizwa ataokolewa, lakini yule ambaye hataamini atahukumiwa adhabu. 17  Zaidi ya hayo, ishara hizi zitafuatana na wale wanaoamini: Kwa kutumia jina langu watatoa roho waovu, watasema kwa lugha, 18  nao watainua nyoka kwa mikono yao, na wakinywa kitu chochote chenye kuua hakitawaumiza hata kidogo. Wataweka mikono yao juu ya watu wagonjwa, nao watapona.” 19  Kwa hiyo, basi, Bwana Yesu, alipokuwa amekwisha kusema nao, akachukuliwa juu mpaka mbinguni na kuketi kwenye mkono wa kuume wa Mungu. 20  Basi, wakatoka kwenda na kuhubiri kila mahali, huku Bwana akifanya kazi pamoja nao na kuutegemeza ujumbe huo kupitia ishara zenye kufuatana nao.

Maelezo ya Chini