Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Dini Inapaswa Kulaumiwa?

Je, Dini Inapaswa Kulaumiwa?

Je, Dini Inapaswa Kulaumiwa?

MWANDISHI na kasisi wa karne ya 18, Jonathan Swift, aliandika hivi: “Tumejihusisha sana katika dini hivi kwamba tumeanza kuchukiana badala ya kupendana.” Watu wengi wamesema kwamba kwa kweli dini inachochea migawanyiko badala ya umoja. Lakini si kila mtu anayekubaliana na maoni hayo.

Kwa mfano, fikiria mkataa uliofikiwa na kikundi kimoja cha watafiti katika Idara ya Masomo ya Amani katika Chuo Kikuu cha Bradford, Uingereza. Kikundi hicho kilisimamiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza na kilipaswa kuchunguza ikiwa dini inachochea amani au vita.

Katika ripoti iliyochapishwa, watafiti hao walisema hivi: “Baada ya kupitia uchunguzi wa kihistoria uliofanywa na wataalamu mbalimbali, tunafikia mkataa kwamba kumekuwa na vita vichache sana ambavyo vilisababishwa hasa na dini katika miaka 100 iliyopita.” Kikundi hicho cha watafiti kilieleza kwamba vita fulani ambavyo “mara nyingi vinatajwa na vyombo vya habari na sehemu nyingine kuwa vita kuhusu dini, au vita vinavyosababishwa na tofauti za kidini, kwa kweli ni vita vya kizalendo, vya kukomboa eneo fulani au vya kujilinda.”

Hata hivyo, watu wengine wengi wanasema kwamba viongozi wa kidini, kwa matendo au kwa kukaa kimya, wamekubali au kuunga mkono vita vingi kama inavyoonyeshwa na manukuu yafuatayo:

● “Ni kana kwamba dini imejihusisha na jeuri kila mahali. . . . Katika miaka ya hivi karibuni, jeuri ya kidini imetokea kati ya Wakristo wenye msimamo mkali nchini Marekani, Waislamu na Wayahudi wenye hasira huko Mashariki ya Kati, Wahindu wanaozozana na Waislamu huko Asia Kusini, na pia kati ya watu wa dini za kiasili huko Afrika na Indonesia. . . . Watu wanaohusika katika visa hivyo wameacha dini iwaamulie mambo ya kisiasa na iendeleze mawazo yao ya kulipiza kisasi.”—Terror in the Mind of God—The Global Rise of Religious Violence.

● “Kinyume na inavyotazamiwa, mara nyingi mataifa yaliyo na ushupavu wa kidini ndiyo yaliyo na matendo maovu zaidi ya kijamii. . . . Kuwepo kwa dini nyingi hakujazuia kuongezeka sana kwa uhalifu. . . . Uthibitisho wa wazi unaonyesha hivi: Ili uweze kuishi mahali ambapo ni salama, penye utaratibu, na penye ‘ustaarabu,’ epuka maeneo yaliyo na watu wengi wanaoshikilia sana mambo ya kidini.”—Holy Hatred.

● “Wabaptisti wanajulikana zaidi kwa kupigana badala ya kufanya amani. . . . Suala la utumwa [nchini Marekani] na mambo mengine yalipogawanya makanisa na taifa lote katika karne ya 19, Wabaptisti wa Kaskazini na Kusini waliunga mkono harakati ya vita na kusema vilikuwa vita vya uadilifu na kudai kwamba Mungu alikuwa upande wao. Wabaptisti pia waliunga mkono jitihada za kitaifa za kupigana na Uingereza (1812), Mexico (1845), na Hispania (1898), wakijitetea kwamba walihusika katika vita dhidi ya [Mexico na Hispania] ‘ili kuwakomboa kidini watu waliokandamizwa na kufungua maeneo mapya kwa ajili ya kazi ya umishonari.’ Jambo kuu si kwamba Wabaptisti walipenda vita badala ya amani, lakini ni kwamba, kwa sehemu kubwa, vita vilipotokea, Wabaptisti waliviunga mkono na kushiriki.”—Review and Expositor—A Baptist Theological Journal.

● “Wanahistoria wamegundua kwamba uchochezi wa kidini katika vita umekuwepo kwa vizazi vingi na miongoni mwa watu mbalimbali na tamaduni zote za ulimwengu, na mara nyingi uchochezi huo unakuwa pande zote zinazopigana. Maneno haya ‘miungu iko upande wetu’ ni mojawapo ya maneno yaliyoanza kutumiwa zamani sana kuwachochea watu kwa ajili ya vita.”—The Age of Wars of Religion, 1000-1650—An Encyclopedia of Global Warfare and Civilization.

● “Viongozi wa kidini . . . wanapaswa kufikiria kwa uzito kwa nini wameshindwa kutoa uongozi unaofaa na kuendeleza viwango vya msingi vya imani yao. . . . Ni kweli kwamba dini zote hutaka kuwe na amani lakini haionekani kama dini imewahi kutimiza daraka hilo.”—Violence in God’s Name—Religion in an Age of Conflict.

Muda wote wa historia, viongozi wa kidini wa dini zote kuu zinazodai kuwa za Kikristo (Wakatoliki, Waothodoksi, na Waprotestanti) wa pande zote zinazopigana, wamewatuma makasisi kwenda kuwachochea wanajeshi na kusali kwa ajili ya waliokufa na waliokuwa wakielekea kufa. Kwa kufanya hivyo, wameunga mkono umwagikaji wa damu na kubariki wanajeshi wote.

Huenda wengine bado wakapinga kwamba dini haipaswi kulaumiwa kwa sababu ya vita. Lakini swali ni, Je, dini imefaulu katika jitihada zake za kuwaunganisha wanadamu?

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

“Padri Dakt. Charles A. Eaton, kasisi wa Kanisa la Madison Avenue Baptist, jana alitangaza kutoka jukwaani kwamba nyumba ya parokia iliyojengwa kwenye uwanja wa kanisa itageuzwa kuwa kituo cha kuwaandikisha wanaume wanaotaka kujiunga na jeshi la nchi kavu au la majini.

“Yeye ni kasisi mmoja kati ya zaidi ya kumi katika jiji hilo ambao huhubiri kuhusu vita mara kwa mara wakati wa ibada ya asubuhi ya Jumapili (Siku ya Yenga) na kuwahimiza wanaume na wanawake waonyeshe ushikamanifu wao kwa taifa na demokrasia kwa kutoa huduma zao vitani haraka iwezekanavyo. Bendera zilipeperushwa katika makanisa mengi.”—“The New York Times,” Aprili 16, 1917 (16/4/1917).