Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Makasri Madogo ya Istanbul

Makasri Madogo ya Istanbul

 Makasri Madogo ya Istanbul

● Nyumba za ndege zilizojengwa kwa mbao zinapatikana sehemu nyingi ulimwenguni. Nyumba hizo ni mahali pazuri sana kwa ndege kula, kujipasha joto, kujenga kiota, kulea makinda yao, na kujikinga kutokana na wawindaji hatari na pia hali mbaya ya hewa. Huko Istanbul, nyumba za ndege zimebuniwa ili zifanane na nyumba za kawaida za wanadamu. Nyingine hufanana na makasri au misikiti. * Kwa kawaida, zinajulikana kama makasri ya njiwa au hata shomoro.

Nyumba za zamani zaidi kati ya hizo, zilijengwa katika karne ya 15, na zina muundo wenye kuvutia wa wakati huo. Nyumba hizo ni sahili, lakini kuanzia karne ya 18, zilijengwa zikiwa na mapambo mengi. Baadhi ya nyumba hizo zilikuwa na vyombo vya kuweka chakula na maji, vijia, na hata veranda ambapo ndege hao wangeweza kuketi na kutazama nje. Nyumba hizo ziliwekwa kwenye upande wa jengo ambapo zingepata jua la kutosha, zingekingwa kutokana na upepo—na mahali ambapo paka, mbwa, na hata wanadamu hawangeweza kufikia. Wakati mwingine nyumba hizo ziliongezwa kwenye jengo, si kwa matumizi ya ndege tu bali pia ili kulirembesha. Nyumba hizo za ndege zinaweza kuonekana kando ya misikiti mikubwa na midogo, na pia kando ya mifereji ya umma ya kunywa maji, majengo ya maktaba, madaraja, na pia katika nyumba za watu binafsi.

Jambo la kuhuzunisha ni kwamba baadhi ya nyumba hizo za ndege zimechakaa kwa sababu ya hali mbaya ya hewa, na nyingine zimeharibiwa na watu ambao hawakujua thamani yake. Ni vigumu sana kuona nyumba hizo siku hizi. Hata hivyo, unapotembelea Istanbul na unapendezwa na majengo ya kale, ona ikiwa unaweza kuona makasri hayo madogo. Kwa kuwa sasa unajua makasri hayo madogo yalitumika jinsi gani utafurahia sana kutembelea jiji hilo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Ingawa zinafanana na nyumba halisi, kwa kawaida hazijengwi kwa kuiga nyumba fulani hususa.