Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kipandauso—Kitulizo Ni Nini?

Kipandauso—Kitulizo Ni Nini?

 Kipandauso—Kitulizo Ni Nini?

Joyce, mfanyakazi mchangamfu anaangalia karatasi aliyoshika. Kwa ghafula, sehemu ya karatasi hiyo inaonekana kana kwamba haina maandishi. Kisha anaona vimulimuli vya mwanga mbele ya macho yake, halafu vimulimuli hivyo vinakuwa mistari ya kiajabu iliyojipindapinda. Baada ya dakika chache, Joyce hawezi kuona chochote. Anapotambua kinachompata, anameza tembe moja ambayo yeye hutumia hali hiyo inapotokea.

JOYCE anaugua kipandauso, ugonjwa ambao ni tofauti sana na maumivu ya kawaida ya kichwa. Kwa mfano, tofauti na maumivu ya kawaida ya kichwa, kipandauso hufuata mpangilio fulani. Pia maumivu hayo yanaweza kuwa makali sana hivi kwamba yanamzuia mtu kufanya shughuli zake za kawaida.

Dalili za kipandauso ni nini? Kichwa huuma kwa kupigapiga upande mmoja tu. Huenda mgonjwa akahisi pia kichefuchefu na asiweze kustahimili mwangaza mwangavu. Maumivu hayo yanaweza kuchukua saa chache au hata siku kadhaa.

Ingawa watu wengi huumwa na kichwa kwa sababu ya mkazo, ni mtu 1 kati ya 10 tu anayepatwa na kipandauso. Tatizo hilo huwaathiri sana wanawake kuliko wanaume. Ingawa watu fulani huwa na maumivu makali zaidi kuliko wengine, wengi wao hukosa kwenda kazini kwa siku kadhaa kila mwaka. Kipandauso hufanya watu wapoteze mapato na huathiri sana familia na maisha ya mtu. Kwa sababu hiyo, Shirika la Afya Ulimwenguni lilisema kwamba ugonjwa huo ni kati ya magonjwa 20 ulimwenguni ambayo husababisha ulemavu.

 Muda mfupi kabla ya kupatwa na kipandauso, watu fulani huwa na dalili kama vile mikono kuwa baridi, uchovu, kuhisi njaa, au kubadilika kwa hisia. Kisha, kabla tu ya maumivu ya kichwa kuanza, huenda wakahisi kizunguzungu, mlio kama wa nyuki masikioni, mwasho kana kwamba wanachomwa na sindano, kuona vitu viwili-viwili, matatizo ya kusema, au misuli kuwa dhaifu.

Bado haijulikani vizuri ni nini husababisha kipandauso, lakini inadhaniwa kwamba huenda ikawa ni tatizo la mfumo wa neva ambalo huathiri mishipa ya damu kichwani. Huenda maumivu hayo yenye kupigapiga yakawa yanasababishwa na damu inapoingia kwenye mishipa ya damu iliyoathiriwa. Jarida Emergency Medicine kinasema: “Watu wanaopatwa na kipandauso wamerithi mfumo wa neva unaoweza kuathiriwa kwa urahisi sana na mambo mbalimbali maishani kama vile, kukosa usingizi, harufu kali, kusafiri, kukosa kula, mkazo, na mabadiliko ya homoni mwilini.” Watu ambao hupatwa na kipandauso, huenda pia wakawa na matatizo ya kuharisha au kufunga choo, kushikwa na wasiwasi ghafula, na kushuka moyo.

Jinsi ya Kutuliza Kipandauso

Huwezi kubadili mfumo wa neva uliorithi. Lakini huenda ukazuia mambo yanayochochea kipandauso. Kwa kuandika kila mara wanapopatwa na kipandauso, watu fulani wamegundua vyakula na hali zinazochochea ugonjwa huo.

Mambo yanayochochea ugonjwa huu hutofautiana kwa kila mtu. Lorraine aligundua kwamba yeye hupatwa na kipandauso wakati wa siku zake za hedhi. “Katika kipindi hicho,” anasema, “utendaji wowote wenye kupita kiasi kama vile kazi ngumu, joto au baridi, kelele nyingi, au hata chakula chenye vikolezo—hunifanya nipatwe na kipandauso. Kwa hiyo mimi hutulia na kufanya mambo kwa kiasi wakati huo.” Joyce, ambaye ameugua kipandauso kwa zaidi ya miaka 60, anasema, “Nimegundua kwamba machungwa, nanasi, na divai nyekundu hufanya nipatwe na kipandauso mara moja, hivyo mimi huepuka vitu hivyo.”

Si rahisi kutambua ni vitu gani hususa huchochea kipandauso kwa sababu kwa kawaida huenda vitu kadhaa vikahusika. Kwa mfano, wakati mmoja unaweza kula chokoleti bila tatizo lolote, lakini wakati mwingine huenda ikakufanya upatwe na kipandauso, labda kwa sababu ya hali fulani.

Hata ingawa huenda usitambue au kuepuka vitu ambavyo vinachochea kipandauso, kuna njia nyingine za kuzuia uwezekano wa kupatwa na tatizo hilo. Wataalamu wanapendekeza kwamba ufuate ratiba ileile ya kulala siku zote saba kwa juma. Ikiwa unataka kulala kwa muda mrefu zaidi mwisho wa juma, wanapendekeza uamke saa za kawaida, ufanye jambo fulani kwa dakika chache, kisha urudi kulala. Kubadili kiwango cha kafeini unachokunywa kunaweza kuchochea kipandauso, kwa hiyo jaribu kunywa vikombe viwili tu vya kahawa au soda mbili zenye kola kwa siku. Kwa kuwa njaa pia huchochea kipandauso, usikose kula mlo wowote. Ingawa ni vigumu kuepuka mkazo, ambao mara nyingi huchochea kipandauso, jaribu kutafuta njia za kujituliza, pengine kwa kubadili ratiba yako, kusoma Biblia, au kusikiliza muziki mwororo.

Je, Kuna Tiba ya Kipandauso?

Kuna njia mbalimbali za kutibu kipandauso. * Kwa mfano, usingizi ni moja kati ya tiba bora zaidi. Dawa za kutuliza maumivu ambazo unaweza kununua dukani bila maagizo ya daktari zinaweza kumtuliza mgonjwa na kumwezesha kulala.

Katika mwaka wa 1993, dawa mpya ya kutibu hasa kipandauso inayoitwa triptan, iligunduliwa. Jarida The Medical Journal of Australia lilisema “hiyo ni hatua kubwa katika tiba,” na kuongeza: “Kugunduliwa kwa dawa ya triptan . . . ya kutibu kipandauso na maumivu mengine ya kichwa ni hatua kubwa, sawa tu na kugunduliwa kwa penicillin inayotibu magonjwa yanayoambukizwa na bakteria!”

Mtu hawezi kufa kutokana na kipandauso. Kwa hiyo, tofauti na dawa ya kutibu maambukizo, dawa ya kutibu kipandauso haitumiwi kuokoa  uhai. Hata hivyo, triptan imewaletea watu fulani kitulizo kikubwa ambao kwa miaka mingi shughuli zao za kila siku zilikatizwa na kipandauso. Ingawa bado lazima wagonjwa wafanye mabadiliko yaliyotajwa, watu fulani ambao hupatwa na kipandauso wamesema kwamba triptan ni dawa inayofanya miujiza.

Hata hivyo, bado dawa zote zina faida na madhara yake. Kuna matatizo gani yanayohusiana na triptan? Kwanza, kila tembe inauzwa kwa bei ghali sana sawa na bei ya kununua mlo katika mkahawa wa kifahari, kwa hiyo zinapewa tu watu ambao hupata maumivu makali sana. Pia triptan haimtulizi kila mtu, na pia watu fulani wenye matatizo ya kiafya wanashauriwa wasitumie dawa hizo. Ingawa hakuna tiba kwa watu ambao wamerithi kipandauso, jarida Emergency Medicine linasema hivi: “Mgonjwa hana sababu ya kuteseka kwa kuwa kuna dawa mpya na zilizoboreshwa za kutuliza kipandauso.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 14 Amkeni! halipendekezi matibabu yoyote hususa. Kila mtu anapaswa kuchunguza matibabu mbalimbali kabla ya kufanya uamuzi wake.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kwa kuandika kila mara wanapopatwa na kipandauso, watu fulani wameweza kugundua vyakula na hali zinazochochea ugonjwa huo

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kusikiliza muziki mwororo kunaweza kupunguza mkazo, ambao mara nyingi huchochea kipandauso

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kipandauso ni ugonjwa wa kurithiwa ambao unaweza kutibiwa