Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Lazima Ujumbe Uenezwe

Lazima Ujumbe Uenezwe

Lazima Ujumbe Uenezwe

KABLA ya telegrafu kubuniwa, mara nyingi ilichukua muda mrefu na pia ilikuwa vigumu kuwa na mawasiliano ya masafa marefu, ikitegemea namna ya usafiri na eneo. Kwa mfano, fikiria magumu waliyokabili Wainka, ambao walikuwa na milki kubwa huko Amerika Kusini.

Milki hiyo ilipofikia kilele mwishoni mwa karne ya 15 na mapema katika karne ya 16 W.K., ilitia ndani sehemu fulani za nchi ya sasa ya Argentina, Bolivia, Chile, Kolombia, Ekuado, na Peru. Cuzco, mji mkuu wa milki hiyo ulikuwa huko Peru. Ilikuwa vigumu kusafiri kwa sababu ya milima mirefu, misitu mikubwa, na umbali. Isitoshe, Wainka hawakuwa na wanyama wa kubeba mizigo isipokuwa mnyama anayeitwa lama. Hawakuwa na magari yenye magurudumu wala lugha iliyoandikwa. Hivyo, waliwasilianaje katika milki hiyo kubwa?

Wainka walifanya lugha ya Quechua, kuwa lugha ya taifa. Pia walijenga barabara nyingi. Barabara yao kuu ya kifahari ilikuwa na urefu wa kilometa zaidi ya 5,000 kupitia milima ya Andes, huku barabara nyingine iliyokuwa sambamba na hiyo ikiwa na urefu wa kilometa 4,000 hivi kandokando ya Pwani ya Pasifiki. Barabara hizo ziliunganishwa na barabara nyingine za kando. Pia Wainka walijenga barabara zenye ngazi katika sehemu za milimani, madaraja yaliyojengwa juu ya jukwaa kwenye vinamasi, na madaraja hatari ya kuning’inia juu ya makorongo. Daraja moja la kuning’inia lenye urefu wa meta 45, lilikuwa na nyaya zenye unene kama wa binadamu, nalo lilitumiwa kwa miaka 500 hadi mwaka wa 1880!

Wainka waliwasiliana kwa kutumia wakimbiaji walioitwa chasquis, ambao walisimama mahali hususa kwenye barabara kuu. Kila mmoja wao alikimbia kilometa tatu au nne na kumpokeza mwenzake ujumbe. Inasemekana kwamba wangeweza kukimbia kwa zaidi ya kilometa 150 kabla ya giza kuingia. Walieneza ujumbe mwingi kwa mdomo lakini walibeba habari zilizokuwa na takwimu za serikali katika kifaa cha pekee kilichoitwa quipu. Kifaa hicho kilichotengenezwa kwa kamba na nyuzi zenye rangi mbalimbali kiliwasaidia wajumbe kukumbuka mambo. Kamba hizo zilikuwa na mafundo yaliyowakilisha namba katika makumi, na mamia. Wahispania walipowashinda Wainka, kifaa hicho kiliacha kutumiwa na mbinu hiyo ikasahauliwa.

‘Miguu Inayopendeza Juu ya Milima’

Leo, ujumbe ulio muhimu zaidi unaenezwa kwa mamilioni ya watu wanaozungumza lugha ya Quechua. Ujumbe huo ni habari njema ya Ufalme wa Mungu, yaani, serikali ya ulimwengu itakayoleta amani kwa wote wanaotii utawala wake. (Danieli 2:44; Mathayo 24:14) Bado ni vigumu kusafiri katika nchi hiyo iliyotawaliwa na Wainka, na kwa kiwango fulani, bado lugha ya Quechua haijaandikwa. Lakini Mashahidi wa Yehova ambao wengi wao wamejifunza kuzungumza lugha ya Quechua, wanafurahia kugawanya vichapo na video katika lahaja kadhaa za kisasa zinazotokana na lugha hiyo.

Kazi ya waeneza-injili hao inatukumbusha maneno haya yaliyoongozwa na roho ya Mungu: “Jinsi inavyopendeza juu ya milima miguu ya yeye anayeleta habari njema, yeye anayetangaza amani, yeye anayeleta habari njema za jambo bora.”—Isaya 52:7.