Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Kila mwaka, karibu watoto milioni sita, yaani, mtoto mmoja kila sekunde tano, hufa kwa sababu ya kukosa chakula cha kutosha.”—JAMES T. MORRIS, MKURUGENZI MKUU WA SHIRIKA LA CHAKULA ULIMWENGUNI

Idadi rasmi ya watu waliokufa kutokana na Tufani Katrina, iliyokumba eneo la kusini la Marekani mnamo Agosti 2005, ni zaidi ya 1,300.—THE WASHINGTON POST, MAREKANI.

Tetemeko la nchi lililokumba Pakistan kaskazini na India mnamo Oktoba 2005, liliua watu zaidi ya 74,000.—SHIRIKA LA HABARI LA UINGEREZA.

Ripoti moja inasema kwamba “ulimwenguni pote karibu watu milioni 1.2 hufa katika aksidenti za barabarani kila mwaka.” —SOUTH AFRICAN MEDICAL JOURNAL, AFRIKA KUSINI.

Hazina Zilizo Hatarini

Kanisa Katoliki limeshindwa kuamua jinsi ya kulinda sanaa zenye thamani kubwa za wakati wa ukoloni ambazo zimepamba makanisa huko Peru. Katika miaka sita iliyopita, wezi wamepora makanisa 200. Huko Cuzco pekee, sanaa 5,000 hivi, hasa zile zilizochorwa kwa rangi ya mafuta, zimeibwa katika miaka 15 iliyopita. Hakuna ajuaye ni sanaa ngapi hususa ambazo zimeibwa nchini kote. Ili kupambana na waporaji, makanisa fulani yameficha sanaa zao, lakini yameziweka mahali pasipofaa. Sanaa za kanisa moja zililiwa na panya.

Ukosefu wa Wafanyakazi wa Kiufundi Nchini Finland

Sekta ya viwanda na huduma nchini Finland inahitaji sana wafanyakazi wa kiufundi ambao wamemaliza elimu ya kiufundi, kama vile maseremala, mafundi wa mabomba, mafundi wa kuunganisha vyuma, waashi, makanika, watengeneza-mashini, na wauguzi. Kwa nini? Elimu ya juu ndiyo imekaziwa zaidi, linasema gazeti Helsingin Sanomat. “Ni jambo lisilopatana na akili kuzoeza kizazi kizima kuwa madaktari na kupata shahada mbili katika sanaa na sayansi,” anasema Heikki Ropponen wa Shirikisho la Wafanyakazi wa Rejareja la Finland. “Elimu ya kiufundi inapaswa kukaziwa zaidi.”

Uamuzi Mzuri wa Mahakama Nchini Ufaransa

Desemba 1, 2005, Mahakama ya Rufani ya Paris iliamuru waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa awaruhusu Mashahidi wa Yehova waone hati za polisi zilizotumiwa kuwaorodhesha kuwa “madhehebu” mnamo 1996. Watu hawakuruhusiwa kuwepo orodha hiyo ilipokuwa ikitayarishwa, na habari zilizokuwa katika hati hizo ziliwekwa kuwa siri kwa madai ya kwamba zilihusu ‘usalama wa Serikali na wa umma.’ Lakini, mahakama hiyo iligundua kwamba “athari” inayotokezwa na kazi ya Mashahidi kama ilivyotajwa katika hati hizo ilikuwa “ndogo sana” hivi kwamba “haikustahili kuzingatiwa.” Hata hivyo, orodha hiyo imetumiwa mara nyingi kuhalalisha ubaguzi dhidi ya Mashahidi wa Yehova nchini Ufaransa.

“Ukuta Mkubwa wa Kijani Kibichi”

Maeneo mengi nchini China yanageuka kuwa makame kwa sababu ya kulisha mifugo kupita kiasi, ukame, ukataji-miti, na kutumia maji kupita kiasi. Kwa hiyo, serikali ya China imeanzisha “mradi mkubwa zaidi wa kimazingira katika historia ya ulimwengu,” linasema gazeti New Scientist. “Chini ya mradi huo ambao umeitwa ‘ukuta mkubwa wa kijani kibichi,’ miti mingi sana imepandwa ili kuzuia vumbi lisipeperushwe.” Pia nyasi na vichaka vinapandwa ili kuzuia udongo usipeperushwe. Mradi huo ulianza mnamo 1978 na karibu nusu ya eneo lenye ukubwa wa ekari milioni 86, ambalo linakusudiwa kufunikwa kwa miti na mimea inayoweza kuhimili ukame, limekamilishwa.