Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Kumwamini Mungu Ni Jambo Lisilopatana na Sayansi?

Je, Kumwamini Mungu Ni Jambo Lisilopatana na Sayansi?

Je, Kumwamini Mungu Ni Jambo Lisilopatana na Sayansi?

UNAPOSOMA mambo ya kisayansi, si ajabu kuona maneno mbalimbali ya kidini. Kwa mfano, nyakati nyingine wanasayansi huitwa “makuhani wakuu wa utamaduni mpya wa kiteknolojia,” nazo maabara zao huitwa “mahekalu” au “madhabahu.” Bila shaka maneno hayo hutumiwa kama mifano tu. Hata hivyo, yanaweza kutokeza swali hili muhimu: Je, kweli kuna pengo linalotenganisha sayansi na dini?

Huenda watu fulani wakahisi kwamba kadiri wanasayansi wanavyozidi kujifunza mambo mapya, ndivyo wanavyozidi kupoteza imani katika Mungu. Ni kweli kwamba kuna wanasayansi wengi ambao hudhihaki imani ya kidini. Lakini wengine wengi wanavutiwa sana na uthibitisho unaoonyesha kwamba ulimwengu umebuniwa kwa ustadi. Wanasayansi wengine hawavutiwi tu na ubuni wenyewe; bali wangependa pia kujua kuhusu Mbuni mwenyewe.

Mabadiliko

Nadharia ya mageuzi ya Charles Darwin imekuwapo kwa karne moja u nusu. Huenda watu fulani wenye elimu walidhani kwamba kufikia sasa, watu wasiojua kitu, wanaodanganyika kwa urahisi na washamba ndio tu wangekuwa wakiamini kwamba kuna Mungu. Sivyo ilivyo. Wanasayansi wengi hukubali waziwazi kwamba wanaamini kuwapo kwa Muumba. Ni kweli kwamba huenda wasiamini kwamba kuna Mungu mwenye utu au huenda wasiiamini Biblia. Hata hivyo, wanasadiki kwamba ubuni uliopo ulitokana na Mbuni mwenye akili.

Je, wanasayansi hao wanaweza kuitwa washamba? Ikieleza kuhusu wanasayansi wanaoamini kwamba ulimwengu wetu na viumbe vilivyopo vilibuniwa kwa akili, makala moja katika gazeti The New York Times inasema hivi: “Wana shahada za juu zaidi na vyeo maarufu katika baadhi ya vyuo vikuu vinavyoheshimiwa sana. Dhana zao zinazopinga nadharia ya Darwin hazitegemei Maandiko; badala yake zinategemea kanuni za sayansi.”

Makala hiyohiyo pia inataja kwamba wale wanaounga mkono dhana ya kwamba ulimwengu umebuniwa kwa akili “hawatoi madai ya kipuuzi. . . . Wanachopinga ni kwamba nadharia ya Darwin, au nadharia nyingine yoyote inayodai kwamba uhai ulitokea wenyewe hatua kwa hatua inatosha kueleza chanzo cha uhai. Wanadai kuwa vitu vyenye uhai vinathibitisha wazi kwamba vimebuniwa kwa ustadi, jambo linalothibitisha kwa kadiri kubwa kuwapo kwa Mbuni Mwenye Akili.” *

Inashangaza kwamba kuna wanasayansi wengi wanaoamini hivyo. Kwa mfano, matokeo ya uchunguzi yaliyotolewa mwaka wa 1997 yalionyesha kwamba asilimia 40 ya wanasayansi wa Marekani wanaamini kuna Mungu mwenye utu. Idadi hiyo haikuwa imebadilika tangu mwaka wa 1914, wakati ambapo uchunguzi kama huo ulifanywa.

Katika nchi zisizo na wafuasi wengi wa dini kama vile nchi za Ulaya, idadi hiyo ni ndogo kwa kulinganishwa. Hata hivyo, gazeti la Uingereza, The Guardian liliripoti kwamba “wataalamu wa sayansi ngumu, kama vile fizikia na jiolojia, wanaoamini kuwapo kwa Mungu ni wengi kuliko wataalamu wa sayansi rahisi kama vile anthropolojia.” Gazeti hilo liliongezea hivi: “Huko Uingereza kuna mashirika kama vile shirika la Wakristo Katika Ulimwengu wa Sayansi.” Gazeti hilo lilisema pia kwamba huko Uingereza “idadi kubwa zaidi ya wanafunzi wa sayansi huenda kanisani kuliko idadi ya wanafunzi wa sanaa.”

Hata hivyo, inaonekana kwamba wanasayansi wengi hudharau maoni ya kwamba kuna Muumba. Maoni yao yanawaathiri sana wanasayansi wenzao. Mtaalamu wa anga Allan Sandage anasema kwamba “mtu husita kujitambulisha kuwa muumini.” Kwa nini? Anasema kwamba “kuna shutuma kali na dhihaka nyingi kutoka kwa wanasayansi wengine.”

Kwa hiyo, wanasayansi wanaojaribu kudokeza kwamba sayansi haipingi kuwapo kwa Muumba, huzimwa na wale wanaotilia shaka jambo hilo. Makala zinazofuata zitazungumzia kauli za wanasayansi hao wanaozimwa mara nyingi na sababu za maoni yao. Hata hivyo, wewe mwenyewe unahusikaje? Je, sayansi inaweza kukusaidia kumpata Mungu? Tafadhali endelea kusoma.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Wasomi na wanasayansi maarufu ambao wameunga mkono hadharani wazo la kuwapo kwa Mbuni Mwenye Akili ni pamoja na Phillip E. Johnson, mwalimu wa sheria katika Chuo Kikuu cha California huko Berkeley; mtaalamu wa biokemia Michael J. Behe, mwandishi wa kitabu Darwin’s Black Box—The Biochemical Challenge to Evolution; mwanahisabati William A. Dembski; mwanafalsafa wa mantiki Alvin Plantinga; wanafizikia John Polkinghorne na Freeman Dyson; mtaalamu wa anga Allan Sandage; na wengine wengi.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

Stars: Courtesy of ROE/Anglo-Australian Observatory, photograph by David Malin