Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kupima Dunia kwa Kijiti

Kupima Dunia kwa Kijiti

Kupima Dunia kwa Kijiti

JE, UMEWAHI kusikia kuhusu mwanahisabati na mtaalamu wa nyota Mgiriki, anayeitwa Eratosthenes? Yamkini jina lake linajulikana sana miongoni mwa wataalamu wa anga. Unafikiri ni kwa nini wanamheshimu sana hivyo?

Eratosthenes alizaliwa wapata mwaka wa 276 K.W.K., na kuelimishwa kwa muda huko Athene, Ugiriki. Hata hivyo, kwa muda mrefu aliishi Aleksandria, huko Misri, iliyokuwa ikitawaliwa na Ugiriki wakati huo. Mwaka wa 200 hivi K.W.K., Eratosthenes alianza kupima dunia kwa kijiti. Huenda ukasema, ‘Haiwezekani!’ Alifanyaje hivyo?

Katika jiji la Sewene (ambalo leo linaitwa Aswân), Eratosthenes aliona kwamba jua lilikuwa katikati kabisa saa sita mchana katika siku ya kwanza ya kiangazi. Alijua hivyo kwa kuwa hakukuwa na kivuli nuru ya jua ilipofika kwenye sakafu ya mashimo marefu. Hata hivyo, saa sita mchana siku hiyohiyo katika jiji la Aleksandria, lililokuwa umbali wa stadia * 5,000 kaskazini mwa Sewene, kivuli kingeweza kuonekana. Basi, Eratosthenes akapata wazo jipya.

Eratosthenes alisimamisha kijiti. Jua lilipokuwa juu ya kichwa saa sita mchana, alipima pembe ya kivuli cha kijiti hicho huko Aleksandria. Akagundua kwamba pembe hiyo ilikuwa digrii 7.2 kutoka kwenye kijiti.

Eratosthenes aliamini kwamba dunia ni mviringo, na alijua kwamba mviringo una digrii 360. Kwa hiyo akagawa digrii 360 kwa kipimo alichokuwa amepata, yaani digrii 7.2. Matokeo yalikuwa nini? Kipimo alichokuwa amepata kilikuwa sehemu moja ya 50 ya mviringo. Kisha akakata kauli kwamba umbali kutoka Sewene mpaka Aleksandria, yaani stadia 5,000, ni sawa na sehemu moja ya 50 ya mzingo wa dunia. Kwa kuzidisha 50 kwa 5,000, Eratosthenes alipata kwamba mzingo wa dunia ni stadia 250,000.

Matokeo yake ni sahihi kadiri gani yanapolinganishwa na hesabu za leo? Tukitumia vipimo vya leo, stadia 250,000 ni kati ya kilometa 45,000 na kilometa 47,000. Kwa kutumia chombo cha angani, wataalamu wa nyota walipima mzingo wa dunia kuanzia ncha ya kaskazini hadi ya kusini na kupata kilometa 40,008. Hivyo, makadirio ambayo Eratosthenes alifanya zaidi ya miaka 2,000 iliyopita, yanakaribiana sana na hesabu za leo. Huo ni usahihi wenye kustaajabisha hasa ukizingatia kwamba mwanamume huyo alitumia kijiti tu na jiometria! Leo wataalamu wa anga hutumia mbinu hiyo ya jiometria kupima umbali nje ya mfumo wetu wa jua.

Wengine wanaweza kuona ni ajabu kuwa Eratosthenes alijua kwamba dunia ni mviringo kwani miaka kadhaa iliyopita hata watu fulani wenye hekima walio na ujuzi wa sayansi waliamini kwamba dunia ni tambarare. Wagiriki wa kale walikuwa wamekata kauli kuhusu umbo la dunia kutokana na uchunguzi wao wa kisayansi. Hata hivyo, yapata miaka 500 kabla ya wakati wa Eratosthenes, nabii mmoja Mwebrania aliongozwa na roho ya Mungu kuandika: “Kuna Yeye [Mungu] anayekaa juu ya mviringo wa dunia.” (Isaya 40:22) Isaya hakuwa mwanasayansi. Alijuaje kwamba dunia ni mviringo? Alifunuliwa ukweli huo na Mungu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Stadia ni kipimo kilichotumiwa na Wagiriki kupima urefu. Ijapokuwa kipimo hicho kilikuwa tofauti katika sehemu mbalimbali, inaaminiwa kwamba stadia moja ilikuwa kati ya meta 160 hivi hadi meta 185.

[Mchoro katika ukurasa wa 13]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mwale wa jua

Sewene

7.2°

Aleksandria

7.2°