Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kumbukumbu ya Milki Kuu ya Roma

Kumbukumbu ya Milki Kuu ya Roma

Kumbukumbu ya Milki Kuu ya Roma

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UJERUMANI

Ni nini kilicho na miaka zaidi ya 1,900, urefu wa zaidi ya kilometa 500, na ni mojawapo ya majengo ya ukumbusho yenye kustaajabisha zaidi ya Milki ya Roma huko Ulaya ya Kati? Jibu ni: “limes.”

LIMES ni jina la ujumla la ngome zilizojengwa na Waroma ili kulinda mpaka wao wa kaskazini dhidi ya makabila ya Ujerumani. Leo ngome hizo zinaonyesha jinsi Milki ya kale ya Roma ilivyokuwa na nguvu.

Maana ya awali ya neno la Kilatini limes ni ‘kijia kilichotengenezwa na wanadamu, kinachopita katikati ya eneo fulani na kuligawanya mara mbili.’ Limes zilijengwa kama kijia au barabara. Mwanzoni hazikukusudiwa kufanyiza mpaka. Hata hivyo, baada ya ngome hizo kujengwa zilifanyiza mpaka. Ujenzi wa ngome hizo ulibadili sana historia ya Milki ya Roma.

Kwa Nini Ngome Hizo Zilijengwa?

Makabila ya Ujerumani yaliyokuwa upande mwingine wa mpaka wa kaskazini wa Milki ya Roma ambao wakati mwingine uliitwa barbaricum yalichukia Roma. Katika eneo hilo, makabila kama vile Wachati yalifanya mashambulio mara nyingi kwenye eneo la mpakani. Wachati walikuwa wapiganaji wakali, hivyo kupigana nao kungesababisha hasara kubwa.

Badala ya kushambulia eneo la barbaricum, jeshi la Roma lilijenga ngome katikati yake na kufanyiza sehemu nyembamba iliyopita kati ya Mto Rhine na Mto Danube, kwenye eneo lisilomilikiwa. Katika sehemu fulani, ngome hizo zilijengwa kwa kukata misitu. Eneo hilo lililindwa na askari-jeshi, hivyo wasafiri walikuwa salama kwa kadiri fulani walipopita hapo.

Mwanzoni, Waroma walitengeneza njia pana tu. Baada ya muda, minara ya mbao ilijengwa kando ya barabara ili ikaliwe na askari-jeshi. Kila mnara ulijengwa karibu na mwingine. Kando ya barabara, ngome yenye kimo cha meta 2.7 ilijengwa kwa vipande vya mbao vilivyochongoka. Kisha mtaro ukachimbwa na ukuta ukajengwa kando yake. Katika sehemu fulani, ukuta wa mawe na minara ya mawe ilijengwa pia.

Katika maeneo ya mbali, ngome zaidi zilijengwa ili zikaliwe na askari-jeshi. Hatimaye, kufikia karne ya tatu W.K., mpaka wa ngome hizo huko Ujerumani ulikuwa na urefu wa zaidi ya kilometa 500. Mpaka huo ulitia ndani ngome nyingine kubwa 60 na nyingine nyingi ndogo. Isitoshe, askari-jeshi wengine walishika doria wakiwa kwenye angalau minara 900. Watu fulani wanasema kwamba minara hiyo ilikuwa na orofa tatu zenye urefu wa meta 10 hivi.

Mpaka Uliofanyizwa na Wanadamu

Kwa hiyo, njia iliyotengenezwa kwenye eneo la adui ikawa mpaka uliofanyizwa na wanadamu. Mpaka uliofanyizwa na ngome hizo ulipita Ujerumani hadi eneo ambalo leo linaitwa Uholanzi na kufika pwani ya Bahari ya Kaskazini. Na huko Uingereza wakati wa Milki ya Roma, Ukuta wa Hadrian na Ukuta wa Antonine zilijengwa kulinda mpaka kutokana na makabila ya Caledonia yaliyoishi katika eneo linaloitwa Scotland leo.

Ngome hizo hazikukusudiwa kufunga mpaka kabisa. Malango yalijengwa ili kuruhusu wakaaji wa eneo la barbaricum kupita ngome hizo na kuingia mikoa ya Roma ya Rhaetia na Germania Superior. Hilo liliwawezesha watu kufanya biashara.

Ngome hizo zinaonyesha wazi badiliko kubwa katika sera ya Waroma. T. W. Potter anaandika hivi: “Kwa karne nyingi Waroma waliona kwamba haikufaa milki hiyo iwe na mipaka hususa.” Basi mpaka huo ukawa “mwanzo wa badiliko kubwa katika sera, yaani, kuacha kupanua mipaka na badala yake kuweka mipaka.”

Je, Kuna Ngome Zilizosalia?

Kufikia karne ya tatu, milki hiyo ilianza kuanguka hatua kwa hatua. Hatimaye askari-jeshi wakaondoka mpakani. Ngome hizo zikaharibika kwa sababu hazikutunzwa, na mawe na mbao zake zikachukuliwa ili zitumiwe kwa makusudi mengine. Mpaka wa mojawapo ya milki zenye nguvu zaidi ulimwenguni ukafunikwa na mimea, ukaachwa, na hatimaye kusahauliwa.

Hata hivyo, mwishoni mwa karne ya 19, watu nchini Ujerumani walipendezwa tena na historia na utamaduni wa Waroma. Tangu wakati huo, sehemu ndogo za mtaro, ukuta wa mtaro, na ukuta wa ngome hizo zimerekebishwa, na vilevile ngome na minara kadhaa. Bado, kuna sehemu kubwa ambazo hazijarekebishwa na hazitambuliki kwa urahisi.

Mojawapo ya ngome iliyorekebishwa vizuri ni ile ya Saalburg katika eneo la Taunus, iliyo kilometa 40 hivi kutoka kwenye ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Ujerumani. Ngome hiyo ina upana wa meta 147 na urefu wa meta 221 na imezungukwa na handaki na ukuta wa mawe wenye minara. Hapo awali ilitumiwa na vikosi 500 hivi vya askari-jeshi. Jengo muhimu la ngome hiyo, yaani makao makuu, liko katikati yake.

Nyuma ya jengo hilo kuna sehemu takatifu ambapo nembo iliwekwa. Kijitabu Limeskastell Saalburg (Ngome ya Limes, Saalburg) kinasema: “Sehemu hiyo takatifu yenye nembo ilitengwa kwa ajili ya miungu ya Milki ya Roma na ibada ya maliki. Mlinzi alisimama mbele yake wakati wa mchana.” Basi, marekebisho yaliyofanywa kwenye ngome hizo yanaonyesha kwamba askari-jeshi waliona dini kuwa muhimu.

Tangu marekebisho hayo yalipofanywa, mpaka wa ngome hizo umewavutia watalii wengi. Katika sehemu nyingi, mahali ambapo ngome hizo zilikuwa, pana njia inayotumiwa na watu wanaotembea kwa miguu. Ukitembelea Ujerumani, mbona usijionee mambo hayo? Utaona kumbukumbu zenye kustaajabisha zitakazokukumbusha kwamba hatimaye hata milki za wanadamu zenye nguvu zaidi huanguka na kutokomea.

[Maelezo ya chini]

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

MAISHA YA ASKARI-JESHI MROMA

Jeshi la Roma lilikuwa na askari-jeshi waliokuwa raia wa Roma na vikosi vingine vya kusaidia vilivyokuwa na askari-jeshi kutoka miongoni mwa watu waliokuwa wameshindwa vitani na milki hiyo. Kikundi kidogo zaidi katika jeshi hilo kiliitwa contubernium, ambacho kilikuwa na askari-jeshi kumi walioishi pamoja. Kila contubernium kumi zilikuwa zikiongozwa na afisa anayeitwa centurion, na maafisa 60 wenye cheo cha centurion walifanyiza kikosi kimoja kilichokuwa na jumla ya askari-jeshi wapatao 4,500 hadi 7,000.

Napoléon Bonaparte alisema kwamba “askari-jeshi wanahitaji kulishwa vizuri.” Milki ya Roma ilijua hilo muda mrefu kabla ya Napoléon, nayo iliwalisha askari-jeshi wake vizuri. Gazeti Archäologie in Deutschland linasema kwamba “hakukuwa kamwe na maasi katika jeshi la Roma kwa sababu ya chakula kisichofaa.” Kwa kweli, “katika sehemu fulani za ulimwengu wa Roma, chakula cha askari-jeshi kilikuwa bora kuliko cha raia.”

Posho la kila siku lilitia ndani nyama, matunda, mboga, mkate wa ngano, na mafuta. Hata hivyo, askari-jeshi hawakuendekezwa. Gazeti hilo linaeleza kwamba “jeshi la Roma halikuwa na mkahawa.” Kila contubernium ilipaswa kujitayarishia chakula.

Baada ya kutumikia katika jeshi kwa miaka 25, kila askari-jeshi Mroma alistaafu kwa heshima, na alipewa kiasi fulani cha pesa au shamba ili kumshukuru kwa utumishi wake. Askari-jeshi ambaye hakuwa raia wa Roma, alipewa uraia pamoja na watoto wake. Kulingana na kitabu Der Limes zwischen Rhein und Main (Ngome Zilizo Katikati ya Rhine na Main), “kwa wanaume wengi, kutumikia katika jeshi la Roma kulikuwa njia rahisi zaidi ya kuwa raia wa Roma.”

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 16, 17]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

NGOME ZILIZOREKEBISHWA HUKO UJERUMANI

-- Ngome za mpakani

1 Wiesbaden

Ngome na mnara wa mawe

2 Butzbach

Mnara wa mbao wenye kuta za udongo

3 Weissenburg

Lango la kaskazini la ngome ya mawe

4 Saalburg

Mojawapo ya ngome zilizorekebishwa vizuri

5 Rainau

Mnara wa mbao na ngome

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.