Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuzuru Yerusalemu Mjini Quebec

Kuzuru Yerusalemu Mjini Quebec

Kuzuru Yerusalemu Mjini Quebec

WATU wanaozuru Yerusalemu leo huwazia jinsi jiji hilo lilivyokuwa katika nyakati za Biblia. Hata hivyo, unaweza kuona mandhari ya pekee ya jiji hilo la kale kilometa 8,500 hivi magharibi ya Yerusalemu katika mji mdogo ulio karibu na Mto wa St. Lawrence huko Kanada. Huko, wageni wanaweza kutazama mandhari yenye kuvutia ya Yerusalemu na viunga vyake. Jinsi gani? Inafaa tueleze.

Picha Kubwa ya Yerusalemu ambayo ni mojawapo ya picha kubwa zaidi ulimwenguni za mandhari iko katika jengo la duara katika mji wa Sainte Anne de Beaupré, Quebec. Picha hiyo kubwa ina urefu wa meta 14 na mzingo wa meta 110. Ingawa picha hiyo si sahihi kabisa, inawapendeza wanafunzi wa Biblia kwa kuwa inaonyesha kihalisi kabisa jinsi maisha yalivyokuwa Yerusalemu katika nyakati za Biblia.

Wageni wanapoitazama picha hiyo wakiwa kwenye jukwaa katikati ya jengo hilo, wanaweza kuona jinsi eneo la mashambani la Yerusalemu lilivyokuwa katika karne ya kwanza. Wanaweza pia kuona picha kamili ya kuta kubwa, hekalu tukufu, na majumba ya kifalme ya fahari ya jiji hilo mashuhuri. Upande wa pili, kuna picha inayoonyesha matukio ya mwisho ya maisha ya Yesu duniani. Picha hiyo ni halisi sana hivi kwamba watazamaji huwazia wakichangamana na umati katika barabara za Yerusalemu.

Jambo la kushangaza ni kwamba picha hiyo halisi ilichorwa zamani za kale. Ama kwa hakika, msanii maarufu wa Paris, Paul Philippoteaux, aliichora kuanzia mwaka wa 1878 hadi 1882. Wasanii wengine watano—wawili kutoka Marekani, wawili kutoka Ufaransa na mmoja kutoka Uingereza—walimsaidia kuchora picha hiyo isiyo na kifani. Hata hivyo, inasemekana kwamba msanii Mjerumani, Bruno Piglhein, ambaye alikuwa ameazimia kuwaelimisha watu kuhusu maisha ya kila siku katika nyakati za Biblia, ndiye aliyebuni picha hiyo. Baada ya picha hiyo kukamilishwa huko Munich, Ujerumani, ilionyeshwa katika majiji makuu ya Ulaya. Tangu mwaka wa 1895, imehifadhiwa huko Kanada.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]

All photos: Cyclorama de Jérusalem inc.