Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kitabu Kinachopinga Vitabu Vingine

Kitabu Kinachopinga Vitabu Vingine

 Kitabu Kinachopinga Vitabu Vingine

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

KWA nini watu wengi wana maoni mabaya kuhusu Biblia? Katika nchi fulani huenda jibu likahusiana na kitu fulani kilichobuniwa na wanadamu ili kudhibiti “uasi wa kidini”—kitabu Index of Forbidden Books (Orodha ya Vitabu Vilivyopigwa Marufuku). Hilo lingewezekanaje?

Kanisa Katoliki lilifurahi sana wakati uchapishaji wa vitabu ulipobuniwa. Hata mapapa fulani walisifu kile kilichoitwa na makasisi fulani “ustadi kutoka kwa Mungu.” Ingawa hivyo, muda si muda, makasisi waligundua kwamba vitabu vilivyochapishwa vilikuwa vikitumiwa kueneza mawazo yanayopingana na Ukatoliki. Kwa hiyo, vikwazo vikawekwa katika dayosisi kadhaa za Ulaya mwishoni mwa karne ya 15. Leseni ya kuchapisha ilianzishwa na katika mwaka wa 1515, Baraza Kuu la Tano la Kanisa likatoa maagizo ya kudhibiti uchapishaji. Wale waliokiuka maagizo hayo wangeweza kutengwa na kanisa. Lakini, hilo halikuwazuia watu kusambaza vitabu ambavyo kanisa iliviona kuwa hatari kwa imani na maadili hasa baada ya kuanza kwa Marekebisho Makubwa ya Kidini. Kwa hiyo, kufikia mwishoni mwa karne ya 16, makundi ya Vatikani yalitaka “uchapishaji usifanywe tena kwa miaka mingi.”

 Ili kuzuia “kuongezeka kasi kwa vitabu visivyofaa na vyenye kudhuru”—kama Myesuiti mmoja Mwitaliano alivyosema mwaka wa 1951—kanisa lilitaka orodha ya vitabu vilivyopigwa marufuku ichapishwe kwa ajili ya Wakatoliki wote. Katika mwaka wa 1542 Baraza la Roma la Kukomesha Uasi lilianzishwa. Baraza hilo lilianza kazi kwa kutunga sheria iliyopinga uhuru wa kuandika vitabu vya kidini. Mdadisi mkuu wa awali, Gian Pietro Carafa, alipowekwa kuwa Papa Paulo wa Nne mwaka wa 1555, mara moja aliamuru tume ya kuorodhesha vitabu vilivyopigwa marufuku ianzishwe. Kitabu cha kwanza cha Index of Forbidden Books kilichapishwa mwaka wa 1559 kwa ajili ya Wakatoliki wote.

Ni Vitabu vya Aina Gani Vilivyopigwa Marufuku?

Kitabu Index kiligawanywa katika “sehemu” tatu. Sehemu ya kwanza iliorodhesha waandishi wote ambao vitabu vyao vilipigwa marufuku bila kujali vilikuwa na habari gani. Sehemu ya pili iliorodhesha vitabu vilivyopigwa marufuku vya waandishi waliokubaliwa. Na sehemu ya tatu ilikuwa na orodha ndefu ya vitabu vya waandishi wasiojulikana. Kitabu Index kilikuwa na orodha ya vitabu 1,107 vilivyopigwa marufuku, iliyoathiri waandishi wa vitabu vya kidini na pia vitabu vinginevyo. Nyongeza ya kitabu hicho iliorodhesha tafsiri za Biblia zilizopigwa marufuku, na ilitaja waziwazi kwamba tafsiri zote za lugha za kienyeji zilikuwa zimepigwa marufuku.

Ingawa tayari vitabu fulani vilikuwa vimepigwa marufuku, “kupitia maagizo hayo yaliyowaathiri Wakatoliki wote, kanisa lilitoa tangazo rasmi la kwanza lililopinga kuchapisha, kusoma, na kuwa na Biblia Takatifu katika lugha ya kienyeji,” asema Gigliola Fragnito, mwalimu wa historia ya kisasa kwenye Chuo Kikuu cha Parma, Italia. Kitabu Index kilipingwa vikali na wauzaji na waandishi wa vitabu hali kadhalika na serikali ambazo zilifaidika kutokana na uchapishaji. Kwa sababu hiyo na nyinginezo, chapa nyingine iliagizwa nayo ilichapishwa katika mwaka wa 1564 baada ya Baraza la Trent.

Baraza la Index lilianzishwa kwa madhumuni hasa ya kukirekebisha mwaka wa 1571. Vikundi vitatu ndivyo vilivyoamua ni vitabu gani vitakavyopigwa marufuku—Baraza la Ofisi Takatifu, Baraza la Index, na bwana wa jumba takatifu, mtu maarufu aliyeteuliwa na papa. Baadhi ya sababu zilizochelewesha kuchapishwa kwa orodha ya tatu ya vitabu vilivyopigwa marufuku zilikuwa kwamba watu kadhaa walikuwa na majukumu yanayofanana na maoni yaliyotofautiana kuhusu ikiwa maaskofu au wadadisi ndio waliopaswa kupewa mamlaka zaidi. Orodha hiyo iliyokuwa imetayarishwa na baraza la Index na kutolewa rasmi na Clement wa Nane mnamo Machi 1596, ilizuiliwa kufuatia ombi la Ofisi Takatifu hadi wakati ambapo ingekuwa na nguvu zaidi za kupiga marufuku usomaji wote wa Biblia katika lugha za watu wa kawaida.

Chapa hiyo ya Index of Forbidden Books haikubadilika sana licha ya marekebisho yaliyofanywa katika karne kadhaa. Waprotestanti wengi ambao waliona vitabu vyao katika orodha hiyo, waliiita Index hiyo “mwongozo bora zaidi wa kutambua vitabu bora.” Hata hivyo, kumbuka kwamba wakati huo, mawazo ya Waprotestanti yalikuwa sawa na ya Ukatoliki kuhusiana na kupigwa marufuku kwa vitabu.

Kitabu Index kilikuwa na matokeo mabaya kwa utamaduni, ambao katika nchi kama Italia “ulikandamizwa,” asema mwanahistoria Antonio Rotondò. Mwanahistoria mwingine Guido Dall’Olio asema kwamba kitabu Index “kilikuwa mojawapo ya vitu vilivyochangia sana kukandamizwa kwa utamaduni nchini Italia, kwa kulinganishwa na sehemu nyingine nyingi barani Ulaya.” Jambo la ajabu ni kwamba vitabu fulani viliokoka kwa sababu viliwekwa mahali pa pekee, palipoitwa motoni, mahali maalum katika maktaba nyingi za kanisa ambapo vitabu vilivyopigwa marufuku vilifungiwa.

 Hata hivyo, hatua kwa hatua uhuru wa kutoa maoni katika enzi ya elimu ulichangia sana kutoweka kwa “kifaa chenye kuonea zaidi cha kupinga uhuru wa uandishi.” Katika mwaka wa 1766, mhariri Mwitaliano aliandika hivi: “Ubora wa vitabu hauamuliwi na marufuku ya Roma. Ni umma ndio huamua.” Kitabu Index kilikuwa kikipoteza umuhimu wake, na katika mwaka wa 1917 Baraza la Index, ambalo lilikuwa likikirekebisha, likavunjwa. Tangu mwaka wa 1966 kitabu Index “hakijawa tena na nguvu za kutekeleza sheria za kanisa pamoja na marufuku yake.”

Biblia Katika Lugha za Kawaida

Historia ya kitabu Index yaonyesha kwamba kati ya “vitabu vyote vyenye kudhuru,” kimoja hasa ndicho kilichowatia hofu makasisi—Biblia katika lugha za kawaida. Katika karne ya 16, “tafsiri zipatazo 210 za Biblia nzima au Agano Jipya” ziliorodheshwa katika vitabu Index, aeleza mtaalamu Jesús Martinez de Bujanda. Katika karne ya 16, Waitaliano walijulikana kuwa wasomaji wenye bidii wa Biblia. Hata hivyo, kitabu Index, pamoja na sheria zake kali zilizopiga marufuku Maandiko katika lugha za kienyeji, ziliathiri sana maoni ya taifa hili kuelekea Neno la Mungu. “Yakiwa yamepigwa marufuku na kufutiliwa mbali eti kwa kuwa yanasababisha uasi, hatimaye Waitaliano waliyaona Maandiko matakatifu kimakosa kuwa maandishi ya waasi wa kidini,” asema Fragnito, kisha aongezea: “Wakatoliki wa kusini mwa Ulaya wangeweza tu kupata wokovu kupitia ukatekisimu,” na “watu wasiokomaa ndio waliotakikana zaidi kuliko watu waliokomaa kidini.”

Ni katika mwaka 1757 tu ndipo Papa Benedict wa 14 alipoidhinisha usomaji wa ‘tafsiri za Biblia za lugha za kienyeji ambazo ziliidhinishwa na Dayosisi ya Papa.’ Kwa hiyo, tafsiri mpya ya Kiitaliano, iliyotegemea Biblia ya Kilatini ya Vulgate, hatimaye ingeweza kutayarishwa. Ama kweli, Wakatoliki Waitaliano walingojea hadi 1958 ili kupokea tafsiri ya kwanza ya Biblia nzima iliyotafsiriwa moja kwa moja kutokana na lugha za awali.

Leo, asema Fragnito, watu wasio Wakatoliki wana bidii ya “kusambaza Maandiko kila mahali.” Bila shaka kati ya watu wenye bidii zaidi ni Mashahidi wa Yehova, ambao wamesambaza zaidi ya Biblia milioni nne za Tafsiri ya Ulimwengu Mpya katika Kiitaliano. Kwa hiyo, wamewafanya mamia ya maelfu ya watu waanze tena kupendezwa na Neno la Mungu. (Zaburi 119:97) Kwa nini usijifunze kitabu hicho kisicho na kifani?

[Picha katika ukurasa wa 20, 21]

Kurasa kutoka katika “Index of Forbidden Books”

[Hisani]

Su concessione del Ministero per i Beni e le Attività Culturali

[Picha katika ukurasa wa 22]

Biblia ya Kiitaliano ya karne ya 16 iliyopigwa marufuku na kanisa

[Picha katika ukurasa wa 22]

“Tafsiri ya Ulimwengu Mpya” imewafanya watu wengi waanze tena kupendezwa na Neno la Mungu