Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Fahari ya Okidi

Fahari ya Okidi

Fahari ya Okidi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KOSTA RIKA

“Huonyesha urembo wake kwenye ukuta wenye vigae. Hupepea-pepea kwenye upepo. Na kivuli, na jua, huyafanya yapendeze zaidi, na sasa kuliko wakati mwingine wowote, yana fahari zaidi.”

HUO ulikuwa utangulizi wa makala moja ya gazeti iliyokuwa ikitangaza Maonyesho ya Okidi ya Kitaifa ya Kila Mwaka huko San José, Kosta Rika. Kutajwa tu kwa jina okidi kwaweza kumfanya mtu akumbuke baadhi ya maua maridadi sana ulimwenguni. Mgeni aliyehudhuria maonyesho hayo alisikika akisema: “Baada ya kutazama uzuri huo wa ajabu, ni nani anayeweza kukana kwamba Mungu ndiye aliyeyaumba?” Kwa kweli, okidi humletea sifa Yehova Mungu, ambaye sifa zake zisizoonekana zinaweza kuonekana kupitia vitu alivyoumba!—Waroma 1:20.

Okidi zimethaminiwa kwa maelfu ya miaka. Yaonekana kwamba Wachina walikuwa wakiyapanda maua hayo zaidi ya miaka 4,000 iliyopita. Katika sehemu nyingine ya ulimwengu, inasemekana kwamba Montezuma aliyetawala nchi inayoitwa sasa Mexico kuanzia mwaka wa 1502 hadi 1520, alikuza jamii mbalimbali za okidi. Hata hivyo, ni katika miaka ya 1800 tu ndipo mimea hiyo ilipoanza kutafutwa sana.

Katika mwaka wa 1818, mwanamume aitwaye William Cattley kutoka Uingereza alipokea shehena ya mimea ya kitropiki kutoka Brazili. Katika mfuko uliobeba shehena hiyo, aliona sehemu za mmea zilizofanana na mizizi. Baada ya kuzipanda, alifurahi wakati zilipochanua ua maridadi la zambarau. Aina hii ya okidi siku hizi inaitwa Cattleya.

Katika miaka ya 1800, matajiri walikuwa na desturi ya kukusanya okidi za pekee. Jamii mpya zingeweza kuuzwa kwa bei ghali sana. Hata hivyo, desturi ya kukusanya okidi ilikuwa imefifia kufikia mwishoni mwa karne hiyo. Kisha ikaanza tena miaka mingi baadaye wakati mbinu mpya nafuu za kuzalisha okidi kwa njia isiyo ya asili zilipogunduliwa. Sasa mtu yeyote angeweza kufurahia maua hayo yenye kupendeza!

Aina Nyingi Ajabu

Kukiwa na jamii zipatazo 20,000 za okidi ulimwenguni pote, huenda hiyo ikawa ndiyo jamii kubwa zaidi ya maua. * Hupatikana karibu kila mahali, kutoka Ncha ya Kaskazini hadi kwenye maeneo yaliyo kama jangwa. Huku okidi nyingine zikipatikana juu ya miti kwenye miinuko ya meta 3,000 katika Milima ya Andes, okidi nyingine—kama zile za Australia—hukua ardhini muda wote.

Kuna okidi za ukubwa, rangi, na harufu mbalimbali. Katika Papua New Guinea, okidi fulani huwa na urefu wa meta nyingi na hufikia uzito wa tani mbili. Nyingine, huwa na maua yanayotoshana na kichwa cha sindano, ambazo zaweza kutoshea kwa urahisi ndani ya kastabini. Okidi nyingine hutia mizizi ardhini, huku zilizo nyingi zikikua kwenye miti au mimea mingine. Kuna okidi ambazo huwa na harufu hafifu ya nazi au rasiberi, huku nyingine zikinuka kama nyama inayooza.

Huenda watu wengine wakauliza, ‘Je, maua yote haya yaliyo tofauti yangeweza kutokana na jamii moja?’ Hata kukiwa na aina nyingi hivyo, kuna mambo mawili ambayo hutofautisha okidi na maua mengine. Kwanza, okidi zina mpangilio wa pekee wa petali. Pili, okidi zina sehemu inayounganisha kwa njia ya pekee sehemu za kike na za kiume za ua hilo.

Okidi za Kosta Rika

Kosta Rika ni nchi ndogo lakini ina mojawapo ya idadi kubwa zaidi ya okidi ulimwenguni. Ama kweli, nchi hiyo ina jamii zipatazo 1,400 tofauti-tofauti, na nyingine bado hazijagunduliwa. Kosta Rika ni eneo lenye hali zinazobadilika-badilika za unyevu na hivyo linafaa kwa ukuzi wa okidi mbalimbali kwa sababu ya hali nzuri ya hewa inayosababishwa na Bahari ya Karibea upande wa Mashariki na Bahari ya Pasifiki upande wa Magharibi. Pia katika nchi hiyo kuna misitu mingi ya mvua ambamo okidi nyingi husitawi. Mti wenye aina 47 za okidi ulipatikana katika msitu mmoja wa mvua!

Jitihada zaendelea kufanywa ili kuokoa jamii nyingi za okidi ambazo ziko hatarini. Ingawa hivyo, inafurahisha kwamba jamii nyingine bado husitawi katika misitu ya Kosta Rika. Leo, watu wa aina zote wanapenda kukuza okidi. Si vigumu kukuza okidi, lakini kuna tatizo moja. Si rahisi kuacha kukuza okidi ukisha zoea. Mwandishi mmoja aliandika hivi: “Kuwa na okidi moja ni kama kujaribu kula njugu moja tu!”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Pia kuna okidi mchanganyiko karibu 100,000 zilizopatikana.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Maonyesho ya Okidi ya Kitaifa ya Kila Mwaka

Chama cha Wakuzaji wa Okidi nchini Kosta Rika kilipanga maonyesho ya kitaifa ya kwanza katika mwaka wa 1971 ili kuwajulisha watu wengi zaidi uhitaji wa kuhifadhi mazingira ya asili ya okidi. Maonyesho ya kwanza yalikuwa madogo yakiwa na mimea 147 kwenye meza chache. Hata hivyo, mwaka mmoja hivi karibuni mimea zaidi ya 1,600 ilionyeshwa. Wanapofika kwenye maonyesho hayo, wageni huona rangi mbalimbali wanapotazama okidi za ukubwa na maumbo mbalimbali.

[Hisani]

Jardín Botánico Lankester

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

Bustani ya Lankester

Bustani hii tulivu iliyoanzishwa mwaka wa 1917 na mtaalamu wa viumbe Charles Lankester Wells kutoka Uingereza, huonwa kuwa mojawapo ya bustani zenye thamani zaidi huko Amerika. Bustani ya Lankester ina jamii 800 za okidi za kienyeji na za kutoka nchi nyingine zinazokua katika eneo la ekari 26 lenye msitu na mbuga. Pia hutumiwa kama hifadhi ya kitaifa. Nyakati nyingine okidi-mwitu—hasa zile zilizo adimu—huuzwa kimagendo. Wenye mamlaka wanapozipata okidi hizo, wanazileta kwenye Bustani ya Lankester ili kuzihifadhi.

[Hisani]

Photos above: Jardín Botánico Lankester de la Universidad de Costa Rica

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]

Kukuza Okidi Nyumbani

▪ Okidi nyingi zinaweza kukua katika mitungi au vikapu vyenye mawe au maganda ya miti.

▪ Ingawa okidi nyingi hazihitaji mchanga, zahitaji mbolea kwa ukawaida—hasa zinapochanua maua.

▪ Mwangaza unaohitajiwa hutegemea aina ya okidi. Nuru nyangavu kutoka dirishani upande wa kusini hufaa okidi aina ya Vanda, huku nuru nyangavu kutoka magharibi au iliyotiwa kivuli upande wa kusini hufaa Cattleya. Nayo Phalaenopsis husitawi inapopata nuru kutoka magharibi au nuru iliyotiwa kivuli katika dirisha linaloelekea kusini.

▪ Okidi zinapaswa kutiwa maji mengi mpaka yaanze kutiririka kupitia mashimo yaliyo chini ya mtungi. Mmea wapaswa kuachwa mpaka maji yakauke kiasi kabla ya kutiwa maji tena.

▪ Okidi husitawi katika hali ya unyevu. Kwa hiyo ikiwa unaishi katika makao makavu, weka mimea yako kwenye sinia yenye mawe na uongeze maji kiasi cha kutofunika mawe hayo.

[Picha]

“Phalaenopsis”

“Vanda”

“Cattleya”

[Hisani]

Jardinería Juan Bourguignon

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Okidi ya “tiger” inaweza kukua kufikia urefu wa meta sita na uzito wake tani mbili

[Hisani]

Noemi Figueroa/Brooklyn Botanical Garden

[Picha katika ukurasa wa 25]

Okidi ndogo zaidi ulimwenguni ina upana wa milimeta moja