Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Twakutana na Nyangumi wa Kijivu wa Ajabu

Twakutana na Nyangumi wa Kijivu wa Ajabu

Twakutana na Nyangumi wa Kijivu wa Ajabu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

Mtu yeyote anayemwona nyangumi wa kijivu huvutiwa hasa na ukubwa wake. Ana umbo la kushangaza, na lenye kustaajabisha. Mtu anaweza kumsikia akipumua na kuhisi matone ya maji yakimwangukia kutoka puani mwa nyangumi huyo. Huo ndio wakati ambapo mtu anatambua kwamba amekutana na kiumbe asiyeeleweka; fumbo kubwa, lenye umbo kubwa jeusi.—Jacques-Yves Cousteau, mvumbuzi wa viumbe wa majini.

MANENO hayo yanaeleza vyema jinsi tulivyohisi motaboti yetu ndogo ilipokaribia nyangumi wa kijivu katika maji yenye kung’aa ya ghuba ya Magdalena huko Baja California, Mexico. Kwa muda mrefu tulitamani kuwaona viumbe hao wa ajabu, ambao huhamia kwenye nyangwa za Baja kila mwaka ili kujamiiana na kuzaa.

Kiongozi wetu alizima injini na kuwakaribia polepole. Yaonekana kwamba nyangumi hao hawakutambua kwamba tulikuwa tukiwakaribia. Tuliwatazama wakijamiiana huku wakibingirika, kufoka maji, na kujitumbukiza majini kwa ghafula, wakitikisa mikia yao. Baadhi yao walikuwa wakitokeza vichwa vyao juu ya maji na kuchunguza mazingira yao.

Kiongozi wetu alituambia kwamba ingawa sheria hazituruhusu kuwakaribia nyangumi hao kwa umbali meta 30, mara kwa mara mama nyangumi wadadisi pamoja na watoto wao hukaribia motaboti na kukubali waguswe!

Pambano la Kuendelea Kuishi

Baada ya kuwaona nyangumi hao, tulichochewa kufanya utafiti zaidi. Tulijifunza kwamba katika karne ya 19, wawindaji wenye bidii karibu wamalize nyangumi wote katika mashariki mwa Pasifiki. Baada ya muda, matumizi ya mafuta na mifupa ya nyangumi yalipungua, na idadi ya nyangumi ikaongezeka. Kisha, mapema katika miaka ya 1900, uwindaji ulianza tena wakati mashua zilipokuwa ‘viwanda vinavyoelea’ ambamo wawindaji walitayarishia nyangumi. Kwa mara nyingine tena, nyangumi wa kijivu wa mashariki mwa Pasifiki walikaribia kutoweka.

Mnamo mwaka wa 1947, Tume ya Kimataifa ya Kudhibiti Uwindaji wa Nyangumi iliweka sheria kali za kulinda nyangumi wa kijivu. Katika miaka ya karibuni serikali ya Mexico hata imejenga hifadhi za nyangumi na Hifadhi ya Vizcaíno Biosphere. * Sasa kuna nyangumi wa kijivu wapatao 26,000, kwa hiyo hawamo tena katika hatari ya kutoweka.

Uhamaji Wao Usio na Kifani

Wakati wa kiangazi nyangumi wa kijivu hupata chakula kaskazini ya mbali, katika bahari ya Bering na Chukchi. Nyangumi hao hula wanyama wadogo wenye magamba, na huhifadhi mafuta mwilini kwa ajili ya safari yao ya umbali wa kilometa 16,000 kuelekea kusini kwenye nyangwa za Baja na kurudi. Nyangumi hao husafiri kwa mwendo wa kati ya kilometa 5-10 kwa saa, na hufika huko baada ya miezi miwili au mitatu. Wao hupoteza uzito mwingi wanapohama na kukaa huko Baja California, kwani nyangumi wa kijivu hutegemea hasa mafuta yanayohifadhiwa mwilini mwao.

Nyangumi wenye mimba huwa wa kwanza kufika kwenye nyangwa, ambapo huzaa katika maji matulivu. Watoto wa nyangumi huzaliwa mkia kwanza na lazima watolewe majini haraka iwezekanavyo ili wapumue. Nyangumi husaidiwa kuzaa na nyangumi wengine wawili wa kike, wanaoitwa shangazi, ambao huwa kama wakunga. Mimba huchukua miezi 12 hadi 13, kwa hiyo nyangumi humzaa mtoto mmoja baada ya kila miaka miwili au mitatu. Hebu wazia kuzaa mtoto mwenye wastani wa kilo 680 na mwenye urefu wa meta 5!

Watoto hunyonya kwa miezi minane hivi maziwa yenye asilimia 53 ya mafuta—mara kumi kuliko mafuta yaliyo katika maziwa ya ng’ombe. Nyangumi hao hukaa nyangwani kwa miezi miwili au mitatu, kuanzia Januari hadi katikati ya Machi, muda ambao huruhusu watoto hao kuhifadhi mafuta mengi kwa ajili ya safari ya kuelekea kaskazini na kuhifadhi joto lao la mwili katika maji baridi ya Aktiki.

Mambo yote hayo kuhusu nyangumi wa kijivu yalitushangaza, pia hatutasahau tulivyowaona katika mazingira yao. Viumbe hao walitufanya tukumbuke maneno ya Zaburi 148:7: “Msifuni BWANA kutoka nchi, enyi nyangumi na vilindi vyote.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Tume ya Kimataifa ya Kudhibiti Uwindaji wa Nyangumi huruhusu wenyeji wa Alaska na Siberia wawinde nyangumi ili kujiruzuku tu. Hatua hizo zimewafaidi nyangumi wa kijivu, ambao sasa wanaonwa na wenyeji kuwa rafiki kwa sababu ya tabia zao zilizotajwa na kiongozi wetu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

ULAJI

Badala ya meno, nyangumi wa kijivu ana mifupa ya rangi ya malai (inayoonyeshwa kwenye picha). Mifupa hiyo ina urefu wa sentimeta 5 hadi 25, na inaning’inia pande zote za utaya wa juu. Mifupa hiyo ina keratini sawa na ile ambayo huwa katika kucha zetu. Nyangumi wa kijivu hula vitu vilivyo kwenye sakafu ya bahari, hufyonza masimbi na wanyama wa baharini wenye magamba. Kisha huchuja maji kupitia mifupa hiyo.

[Hisani]

Courtesy Gray whales with Winston

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

MAELEZO MAFUPI KUHUSU NYANGUMI WA KIJIVU

▪ Nyangumi wa kijivu ana madoadoa meupe kwenye ngozi yake kwa sababu ya kombe na vimelea.

▪ Nyangumi wa kiume hukua kufikia meta 14—huwa warefu kuliko mabasi ya jijini—na wa kike ni wakubwa kidogo kuliko wa kiume.

▪ Nyangumi wa kijivu ana makunyanzi mawili hadi matano kwenye shingo ambayo huliwezesha koo lake kupanuka anapokula.

▪ Kwa kawaida uzito wa nyangumi wa kijivu huwa tani 16, lakini wengine wamefikia tani 30 hadi 40.

▪ Nyangumi wa kijivu hutoka nje ya maji kila dakika tatu hadi tano ili kupumua, lakini anaweza kukaa majini kwa dakika 15.

[Hisani]

© Richard Herrmann/Seapics.com

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Kuchunguza mazingira

[Hisani]

© Michael S. Nolan/Seapics.com

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

© Howard Hall/Seapics.com