Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tour De France Miaka 100 ya Mashindano Makali ya Baiskeli

Tour De France Miaka 100 ya Mashindano Makali ya Baiskeli

Tour De France Miaka 100 ya Mashindano Makali ya Baiskeli

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA

MNAMO Novemba 1902, mkurugenzi wa gazeti la michezo L’Auto, Henri Desgrange, alikuwa akitafuta njia ya kushinda gazeti la Le Vélo kwa mauzo. Géo Lefèvre, mwandishi chipukizi wa gazeti la L’Auto alitoa pendekezo hili: “Mbona tusipange mashindano ya baiskeli kotekote nchini Ufaransa?” Mwanzoni wazo hilo lilionekana kuwa lisilowezekana. Hata hivyo, punde si punde likaanza kupamba moto. Alasiri ya Julai 1, 1903, saa 9:16 kamili, jijini Paris, waendeshaji 60 stadi na wengine, wakaanza mashindano yanayoitwa Tour de France ya majuma matatu yenye umbali wa kilometa 2,428. *

“Watumwa wa Barabara”

Mara moja mashindano hayo yakawavutia watu wengi. Mashabiki wengi walikuja kutoka sehemu zote za Ufaransa ili kuwatazama na kuwashangilia washindanaji hao ambao Albert Londres, mwandishi wa habari wa Ufaransa, aliwaita “watumwa wa barabara.” Kwa kweli, katika miaka michache ya kwanza mashindano hayo hayakuwa rahisi kwa sababu vifaa vilikuwa duni, barabara zilikuwa na mashimo, mikondo ilikuwa mirefu sana, na mara nyingi mikondo hiyo ilianza usiku.

Kwa kuwa hawakupaswa kupata msaada wowote, isipokuwa kwenye vituo vya ukaguzi, baiskeli zao zilipoharibika, waendeshaji wenyewe walilazimika kurekebisha baiskeli zao zenye uzito wa kilogramu 20. Kwa mfano, mwaka wa 1913 na mwaka wa 1919, mara mbili Eugène Christophe alilazimika kurekebisha chuma kinachoshikilia gurudumu la mbele katika karakana ya vyuma kijijini!

Mabadiliko na Usambazaji wa Habari

Ili kuyafanya mashindano hayo yaendelee kuwa yenye kusisimua, wenye kuyapanga walihitaji kubuni njia mpya kila mwaka. Baadhi ya mabadiliko yalitia ndani kuwa na mikondo mingi zaidi lakini mifupi, kuingia kifupi katika nchi jirani, kuwa na timu za taifa au timu zinazodhaminiwa na mashirika, kupima wakati ambao timu au mwendeshaji mmojammoja alitumia, na kumalizia kwenye Champs-Élysées, jijini Paris. Hatua kubwa ilipigwa kufikia mwaka wa 1919, wakati ambapo mshindi wa jumla wa kila siku alitunukiwa jezi la pekee la rangi ileile ya kurasa za manjano za gazeti la L’Auto, yaani lile jezi la manjano ambalo hupendwa sana. Katika mwaka wa 1931, Desgrange alibuni gari la matangazo ambalo liliwatangulia washindanaji kwa saa moja likiwachochea mashabiki barabarani, ili kulipia gharama za mashindano hayo.

Mauzo ya Gazeti la L’Auto, ambalo sasa linaitwa L’Équipe, yakapanda. Mwaka wa 1903, nakala 130,000 za toleo la pekee lililochapishwa dakika saba baada ya kufika kwa Maurice Garin, mshindi wa mashindano ya kwanza ya baiskeli nchini Ufaransa, zilinunuliwa mara moja kutoka kwenye vibanda vya kuuzia magazeti. Siku hizi, kwa sababu mashindano hayo huonyeshwa kwenye televisheni katika nchi zaidi ya 150, mashindano hayo ya Ufaransa yanashikilia nafasi ya tatu kati ya mashindano ya michezo ambayo husambazwa sana na vyombo vya habari, nafasi za kwanza mbili zikichukuliwa na Michezo ya Olimpiki na Kombe la Dunia la Soka. Mashindano hayo yamewavutia watu wengi sana hivi kwamba mwaka wa 1987 wabunge wa Hispania walikatiza mjadala wao ili kutazama ushindi wa mwananchi mwenzao Pedro Delgado akipiga zile kona kali 21 katika mkondo mgumu wa kupanda milima ya Alpe d’Huez!

Kupanda Milima

Mwanzoni, mashindano hayo yalifanywa katika sehemu tambarare. Kisha, mnamo Juni 1910, mwandishi wa habari wa gazeti la L’Auto, Alphonse Steinès, alimtumia Desgrange telegramu kutoka milima ya Pyrenees akisema kwamba vijia vya milimani vingeweza kutumiwa. Steinès hakusema kweli. Yeye mwenyewe alikuwa amepotea usiku kucha kwenye theluji, akiwa kwenye kimo cha meta 2,200! Hata hivyo, mwezi uliofuata waendeshaji kakawana wakapiga moyo konde. Gustave Garrigou wa Ufaransa, hata ingawa hakuwa wa kwanza kufika, alipanda Kijia cha Tourmalet katika milima ya Pyrenees mpaka mwisho bila kushuka kutoka katika baiskeli yake. Tangu wakati huo, vijia vingine vya milima ya Alps na Pyrenees vimeongezwa kwenye mashindano hayo.

Kwenye miteremko, waendeshaji hufikia mwendo mkali wa kilometa 100 kwa saa, na wengi wao huanguka. Katika mwaka wa 1951, Wim Van Est wa Uholanzi, akiwa amevaa lile jezi la manjano, alianguka katika genge lenye kina cha meta 50, naye akavutwa kutoka humo kwa mipira ya ndani ya magurudumu ya baiskeli iliyounganishwa. Wengine wamekumbwa na hali mbaya zaidi. Katika Mwaka wa 1935, Mhispania Francisco Cepeda alikufa baada ya kuanguka katika Kijia cha Galibier, katika milima ya Alps. Na katika mwaka wa 1995, Mwitaliano Fabio Casartelli alianguka na kufa katika mteremko huko Portet d’Aspet, kwenye milima ya Pyrenees.

Mashindano Milimani

Katika mwaka wa 1964, Wafaransa wawili, Jacques Anquetil na Raymond Poulidor, walishindana vikali kupanda Puy-de-Dôme, kwenye milima ya Auvergne. Poulidor, ambaye mara nyingi alikuwa akishikilia nafasi ya pili, alimshinda mwenzake lakini hakupata lile jezi la manjano kwa kuwa alichelewa kwa sekunde chache tu katika jumla ya hatua za mkondo huo.

Katika mwaka wa 1971, Mbelgiji Eddy Merckx na Mhispania Luis Ocaña walikuwa waking’ang’ania uongozi. Katika mteremko wa Kijia cha Mente kwenye milima ya Pyrenees mnamo Julai 12, Ocaña akaanguka. Kwa kuwa alikuwa amejeruhiwa, Mhispania huyo hakuweza kuendelea katika mashindano hayo. Kwa heshima ya mpinzani wake, Merckx aliomba asivae lile jezi la manjano wakati wa kuondoka siku iliyofuata.

Katika mikondo ya milimani waendeshaji wameonyesha ungwana katika michezo kwa njia nyingine pia. Kwa mfano, wakati wa kupanda Kijia cha Izoard kwenye milima ya Alps mwaka wa 1949, wapinzani wakuu wawili Waitaliano Gino Bartali na Fausto Coppi walisahau kwa muda uadui wao ili wasaidiane.

Ushirikiano

Ni jambo lenye kuvutia sana kumwona mwendeshaji mmoja akiwaacha wenzake mbali. Mwaka wa 1951 katika mkondo wa Brive-Agen, Mswisi Hugo Koblet aliwaacha wenzake umbali wa kilometa 145. Lakini mara nyingi, ushirikiano unahitajiwa ili kushinda. Kwa kawaida kuna timu 20 zenye waendeshaji tisa stadi kwenye kila timu. Wanatimu humfuata kabisa kiongozi wa timu, wakiwa tayari sikuzote kumsaidia akichoka, baiskeli yake ikiharibika, au akianguka.

Katika mwaka wa 1934, mwendeshaji Mfaransa René Vietto, mwenye umri wa miaka 20, alionyesha vizuri roho hiyo ya ushirikiano. Ingawa alikuwa na nafasi nzuri ya kushinda mkondo huo, hakusita kurudi na kupanda kijia ambacho alikuwa ametoka tu kuteremka ili akampe baiskeli yake Antonin Magne, kiongozi wa timu yake, ambaye baiskeli yake ilikuwa imeharibika.

Mabingwa

Kushinda mashindano hayo zaidi ya mara moja ni mafanikio makubwa. Mpaka leo hii, waendeshaji wanne wameshinda mara tano: Jacques Anquetil (Ufaransa, mwaka wa 1957, 1961 hadi 1964), Eddy Merckx (Ubelgiji, mwaka wa 1969 hadi 1972, 1974), Bernard Hinault (Ufaransa, mwaka wa 1978 hadi 1979, na 1981 hadi 1982, 1985), na Miguel Indurain (Hispania, mwaka wa 1991 hadi 1995). Lakini ni nani anayejua Mbelgiji Philippe Thys (aliyeshinda katika mwaka wa 1913, 1914, 1920) angalishinda mara ngapi ikiwa mashindano hayo hayangalikatizwa na vita ya ulimwengu ya kwanza, ambapo baadhi ya washindi walifia?

Watu wengi huonelea kwamba mwendeshaji bora kuliko wote alikuwa Eddy Merckx, ambaye aliitwa Mla Watu. Alishinda mikondo 34, akafanya vizuri katika sehemu zote, kama vile katika kutumia wakati mfupi zaidi, katika kuendesha kwa kasi sana, na katika mikondo ya miteremko, na sehemu tambarare na ya kupanda milima. Wapinzani wake aliowashinda walilalamika hivi: “Anatuachia makombo tu.” Wengine humwona Fausto Coppi aliyeshinda mara mbili kuwa ndiye mwendeshaji stadi na mwenye fahari kuliko wote.

Kushinda kwa Vyovyote

Kudanganya katika mashindano hayo kumekuwa kishawishi sikuzote. Waendeshaji wa kwanza wanne katika mwaka wa 1904 waliondolewa kwenye mashindano kwa sababu walifanya mambo kama vile kutumia njia za mkato au kusafiri kwa gari.

Udanganyifu mbaya zaidi katika mashindano ya baiskeli ni matumizi ya dawa ili kupata nguvu zaidi. Miaka ya mwanzoni, baadhi ya washindanaji walipewa dawa isiyojulikana. Katika mwaka wa 1920, gazeti la L’Auto lilichapisha makala iliyoshutumu matumizi ya dawa kwa msaada wa madaktari. Katika mwaka wa 1924, ndugu wawili wa familia ya Pélissier walikubali kwamba wakati wa mashindano hayo walitumia “baruti,” yaani, dawa hatari. Kwa makumi ya miaka, yasemekana kwamba mikasa kadhaa imesababishwa na matumizi ya dawa, kama vile kifo cha mwendeshaji Mwingereza Tom Simpson, alipokuwa akipanda Mont Ventoux katika mwaka wa 1967.

Katika mwaka wa 1998, vyombo vya habari viliripoti kisa cha matumizi ya dawa kwa msaada wa madaktari. Vidonge 400 vya dawa zinazoongeza nguvu mwilini, kutia ndani erythropoietin, vilipatikana katika gari la mkandaji wa misuli wa timu fulani. Timu moja iliondolewa kwenye mashindano, na ya pili ikajiondoa. Mwaka uliopita sifa ya yule aliyeshikilia nafasi ya tatu iliharibiwa na kashfa. Mkurugenzi wa Mashindano ya Baiskeli Nchini Ufaransa, Jean-Marie Leblanc, aliandika hivi kwenye dibaji ya chapisho lenye kichwa 100 ans de Tour de France (Miaka 100 ya Mashindano ya Baiskeli Nchini Ufaransa), lililochapishwa na gazeti la L’Équipe, “matumizi ya dawa, kuyafanya mashindano hayo yawe marefu kupita kiasi, na fedha” ni mambo yanayoweza kukomesha mashindano hayo.

Licha ya matatizo hayo, wanariadha hao bado hawajapoteza tamaa na bidii yao kwa mashindano hayo. Lance Armstrong wa Texas, ambaye ameshinda mashindano hayo mara nne na ambaye pia anatarajiwa kushinda mashindano ya mwaka wa 2003, huu ukiwa mwaka wa 100 tangu mashindano hayo yalipoanza, mashindano ambayo yatafuata ule mzunguko wa mwaka wa 1903, alisema hivi: mashindano hayo “ni maarufu, yana historia ndefu, na ni ya namna ambayo haina kifani. Hayatapata kamwe kuwa mashindano ya kawaida, hata iweje.” Kila mwendeshaji stadi hutamani sana kushinda Mashindano ya Baiskeli Nchini Ufaransa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Leo, mashindano hayo yana umbali wa kilometa 3,600 na mikondo 20, kila mkondo ukichukua siku moja.

[Mchoro/Ramani katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mzunguko wa mashindano ya mwaka wa 100 Julai 5-27, 2003

–– Kupima wakati

—— Usafiri kati ya mikondo

• Mahali pa kuanza

○ Mahali pa kumaliza

• PARIS

-- ——

○ Sedan

-- ——

○ Saint-Dizier

-- ——

○• Nevers

--

○• Lyons

--

○ L’Alpe d’Huez

--

○ Marseilles

——

• Narbonne

--

○• Toulouse

-- ——

○ Cap’ Découverte

-- ——

○ Bayonne

-- ——

○• Bordeaux

-- ——

○ Nantes

——

• Ville d’Avray

--

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 22]

1903 Maurice Garin, mshindi wa kwanza wa Mashindano ya Baiskeli Nchini Ufaransa

1927 Wafanyakazi viwandani wakatiza kazi zao ili kutazama

[Hisani]

100 ans de Tour de France, L’Équipe, 2002 © L’Équipe/Presse Sports

[Picha katika ukurasa wa 23]

1910 Octave Lapize, anasukuma baiskeli yake akipanda milima ya Pyrenees, akiwa na mipira ya ndani ya ziada shingoni

[Hisani]

100 ans de Tour de France, L’Équipe, 2002 © L’Équipe/Presse Sports

[Picha katika ukurasa wa 24]

1951 Mwitaliano Fausto Coppi, ambaye ameshinda mara mbili

1964 Anquetil na Poulidor wakiwa katika mashindano makali

[Hisani]

100 ans de Tour de France, L’Équipe, 2002 © L’Équipe/Presse Sports

[Picha katika kurasa za 24, 25]

1991 hadi 1995 Jezi la manjano Miguel Indurain (Hispania) alishinda Mashindano ya Baiskeli Nchini Ufaransa mara tano

1999 Lance Armstrong akijitahidi kutumia wakati mfupi zaidi

[Hisani]

100 ans de Tour de France, L’Équipe, 2002 © L’Équipe/Presse Sports