Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Mauaji Yanazidi Kuwa ya Kijeuri?

Kwa Nini Mauaji Yanazidi Kuwa ya Kijeuri?

Kwa Nini Mauaji Yanazidi Kuwa ya Kijeuri?

ASUBUHI moja, Frank na Gabriella walikuwa wakitembea kwenye ufuo wa Oregon, Marekani, huku wakitazama jua likichomoza. Hawakutarajia kamwe jambo ambalo lilitukia punde baadaye. Dakika chache baadaye, wote wawili walipigwa risasi kichwani, wakafa. Je, aliyewaua alikuwa akilipiza kisasi? Je, aliwaonea wivu? La hasha. Muuaji huyo hakuwajua hata kidogo, bali alitaka kutimiza ndoto yake. Alitaka kujua jinsi mtu anavyohisi anapomuua mwenzake.

“Mnamo Jumapili Aprili 28, 1996, Martin Bryant aliushangaza ulimwengu wa Magharibi kwa matendo yake ya kujifurahisha. Alisisimuka sana na kujiona kuwa shujaa alipowafyatua risasi watu wote aliokutana nao alipokuwa akizurura-zurura katika mji wa Port Arthur, Tasmania.” (A Study of Our Decline, cha Philip Atkinson) Pia, aliwaua watu 35!

Huko Kanada, mzee mmoja aliyestaafu, mwenye umri wa miaka 65, alikuwa akiendesha baiskeli yake asubuhi moja. Ghafula bin vuu, akagongwa na gari kutoka nyuma, na dereva akatoroka akimwacha katika hali mahututi. Baiskeli yake iliburutwa meta 700 hivi kutoka ilipokuwa. Mwanzoni, ilidhaniwa kwamba dereva huyo alimgonga bila kukusudia na ndiyo sababu aliamua kutoroka, lakini uchunguzi zaidi ulionyesha kwamba dereva huyo alikuwa ameiba gari hilo, na alikuwa akiliendesha ovyoovyo ili kujifurahisha. Inaonekana alimgonga mzee huyo ili “kujifurahisha” pia.

Je, Hii Ni Aina Mpya ya Uhalifu?

Japo uhalifu umekuwepo kwa karne nyingi, watu wanaposikia kuhusu visa vya uhalifu vilivyotajwa hapo juu, wao hujiuliza hivi: “Kwa nini watu hufanya mambo hayo? Mtu anawezaje kufanya kitu kama hicho?” Ingawa huenda uhalifu wa kawaida, kama vile wizi au upunjaji, usiwashtue watu wengi, kuna visa fulani vinavyoripotiwa sana katika vyombo vya habari ambavyo vimewafanya watu waseme hivi, ‘Hiki ni kichaa! Ulimwengu unaelekea wapi?’

Visa hivyo vya uhalifu ni tofauti. Vingi hushtua na huwa vya ukatili. Kama mifano iliyo juu inavyoonyesha, vitendo hivyo hufanywa dhidi ya watu wasio na hatia ambao hawawajui wauaji hao. Isitoshe, mara nyingi mauaji hayo ya kijeuri hufanywa bila sababu hususa. Kuna visa vingi vya aina hiyo.

Mnamo Aprili 1999, wanafunzi 2 huko Colorado, Marekani, walifyatua risasi na kuwaua wanafunzi 12 na mwalimu mmoja halafu wakajiua. Mnamo mwaka wa 1982, mwanamume mmoja huko California alikufa baada ya kununua na kumeza dawa ambayo mtu fulani alikuwa ameitia sumu ya strychnine. Katika mwaka wa 1993, wavulana wawili wenye umri wa miaka kumi walimshawishi mtoto wa miaka miwili anayeitwa James Bulger atoke dukani huko Bootle, Merseyside, Uingereza, ambako mamake alikuwa ameenda kwenye bucha. Walimpeleka kwenye reli, wakampiga hadi akafa.

Matendo mengine huwa ya kigaidi, kama kile kisa cha sumu kilichotukia huko Tokyo katika njia ya chini kwa chini mnamo mwaka wa 1995. Wenyeji wa Japan walishtuka wakati gesi yenye sumu ilipopulizwa na wafuasi wa madhehebu fulani katika njia ya chini kwa chini ya Tokyo na kuwaua watu 12 na kuwajeruhi maelfu ya watu. Haiwezekani kusahau mashambulizi ya majengo ya World Trade Center huko New York na jengo la Pentagon, huko Washington, D.C., ambayo yalisababisha vifo 3,000 hivi. Pia, watu 200 hivi walikufa mwaka jana wakati mabomu yalipolipuliwa huko Bali, Indonesia.

Ni wazi kwamba mauaji ya kijeuri yameenea sana. Tatizo hilo lipo ulimwenguni pote kwani linaathiri mataifa mengi na watu wa matabaka mbalimbali.

Nyakati nyingine, ni kana kwamba watu wanaoyasababisha huwa wanashindana, wakijaribu kuona ni nani atakayefanya tendo la kushtua zaidi. Isitoshe, visa vya uhalifu vinavyosababishwa na chuki vinaongezeka sana. Visa hivyo huwa vikatili sana, navyo hufanywa dhidi ya watu wasio na hatia eti kwa sababu tu wao ni wa jamii, dini, au kabila lingine. Kisa kimoja kama hicho kilitukia mwaka wa 1994 wakati Watutsi 800,000 hivi walipouawa huko Rwanda.

Mambo hayo yote huwafanya watu wajiulize hivi: ‘Kuna nini? Je, mambo yalikuwa hivi zamani? Ni nini kinachosababisha visa hivyo vya ujeuri? Je, inawezekana kupunguza au kukomesha mauaji hayo ya kikatili?’ Makala zinazofuata zitazungumzia maswali hayo na mengineyo.

[Blabu katika ukurasa wa 4]

Mara nyingi watu wanaoua kijeuri humuua mtu yeyote bila sababu hususa