Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Watoto Wanene Wanaongezeka Ulimwenguni

“Watoto wanene wanaongezeka ulimwenguni na tatizo hilo linapasa kutatuliwa kuanzia chanzo chake, yaani, ulaji wa chakula kisichojenga afya,” laripoti gazeti The New York Times. “Kulingana na kikundi cha kimataifa kinachopambana na unene, zaidi ya robo ya watoto wenye umri wa miaka 10 katika nchi fulani katika sehemu zote za ulimwengu ni wanene kupita kiasi.” Nchi zinazoongoza ni Malta (asilimia 33), Italia (asilimia 29), na Marekani (asilimia 27). Robo ya watoto wenye umri kati ya miaka minne hadi kumi huko Chile, Mexico, na Peru ni wanene. Katika sehemu fulani za Afrika, watoto wanene ni wengi kuliko wale wenye uzito wa chini sana. Kwa nini watoto wengi ni wanene? Gazeti la The Washington Post linajibu hivi: “Mtoto Mmarekani hutazama wastani wa matangazo 10,000 ya chakula kila mwaka, asilimia 95 ya matangazo hayo yanahusu vitafunio na soda, peremende, na vyakula vya nafaka vilivyotiwa sukari. Hivyo vyote ni vyakula ambavyo hugharimu pesa nyingi na havina lishe. Vitafunio na soda huhusianishwa na vitu vya watoto vya kuchezea, michezo, bidhaa za kukusanywa, sinema na watu mashuhuri. . . . Basi haishangazi kwamba watoto hupata asilimia 15 ya nishati yao kutokana na vitafunio, asilimia 10 kutokana na soda, na nusu tu kutoka kwa matunda na mboga zinazopendekezwa.”

Tembo Huwaogopa Nyuki

Idadi ya tembo nchini Kenya imeongezeka, lakini jambo hilo limesababisha matatizo. Tembo huharibu miti na mimea, na kwa wastani huua mtu mmoja kila majuma mawili. Hata hivyo, mwanabiolojia wa Chuo Kikuu cha Oxford, Fritz Vollrath, amevumbua suluhisho la tatizo hilo. Anasema kwamba tembo wanapowachokoza nyuki “wao hushtuka na kukimbia na nyuki huwafuata hadi mbali sana.” Nyuki hushambulia sehemu nyeti za tembo kama vile macho, nyuma ya masikio, chini ya mkono, na tumboni. Vollrath aliweka mizinga ya Kiafrika yenye nyuki na ile isiyokuwa na nyuki juu ya miti kwenye kichaka kinachopendwa na tembo. Gazeti New Scientist laripoti kwamba tembo hao hawakuikaribia miti yoyote yenye mizinga iliyokuwa na nyuki wala thuluthi moja ya miti iliyokuwa na mizinga mitupu. Lakini tembo waliishambulia miti 9 kati ya 10 ambayo haikuwa na mizinga. Vollrath pia aligundua kwamba tembo waliogopa sauti ya nyuki wenye hasira hata kama ilichezwa kwenye kikuza-sauti.

Wajapochelewa Kupata Habari, Walitenda Haraka

“Katika sehemu hii ya Kenya [Enoosaen], Wamasai hawajawahi kuona majengo yoyote marefu, na vitu virefu zaidi ambavyo wameviona ni miti ya migunga na twiga wanaoitafuna vichakani,” gazeti The New York Times lasema. “Hivyo, Kimeli Naiyomah aliporudi katika kijiji hiki kidogo kutoka masomoni nchini Marekani hivi majuzi, alikuta kwamba Wamasai wenzake hawakuwa na habari kabisa kuhusu kilichotokea mbali sana huko New York mnamo Sept. 11. Baadhi ya watu wa jamii hiyo ya wahamaji hawakuwa na habari yoyote kuhusu tukio hilo.” Naiyomah alikuwa anatembelea eneo la Manhattan katika Septemba 11, na alipowaambia wanakijiji wenzake kwamba aliona tukio hilo mwenyewe miezi minane mapema, huzuni ilitanda kijijini na walitaka kusaidia. Kwa kuwa ng’ombe ni wenye thamani sana kwa Wamasai, walitoa ng’ombe 14 ili kuwasaidia wale walioathiriwa na msiba huo. Kwa sababu ya ugumu wa kuwasafirisha ng’ombe hao, afisa wa ubalozi wa Marekani aliyewapokea alisema kwamba “labda angewauza ng’ombe hao na kununua vito vya Wamasai ili kuvipeleka Marekani,” gazeti Times lilisema.

Wasichana Wachokozi

“Wavulana huwachokoza wengine kwa kuwapiga,” lasema gazeti Toronto Star, lakini “wasichana hutumia njia za kiakili na kihisia.” Inadhaniwa kwamba wasichana wanapobalehe, wao huwa waoga na wenye wasiwasi, na huhangaikia jinsi wavulana au wanaume wanavyowaona. Wataalamu wanaochunguza tabia wanaamini kwamba “wasichana hutaka kuwavutia wavulana au wanaume wengi kwa urembo wao, kwa sababu vyombo vya habari huonyesha picha za mahaba.” Aliyekuwa msimamizi wa Kamati ya Kitaifa Kuhusu Hadhi ya Wanawake, Denise Andrea Campbell, anasema hivi: “Wasichana wengi hawajui jinsi ya kushughulikia hisia zao za hasira na wivu kwa njia ya moja kwa moja.” Kwa hiyo, wao ‘huwaelekezea wengine hisia hizo kwa njia isiyo ya moja kwa moja,’ kama vile kuwapuuza, kuwakunjia uso, kuwachongea, na kueneza uvumi.

Mfadhaiko Kazini

“Karibu asilimia 20 ya Wakanada hupata mfadhaiko mwingi sana hivi kwamba wamewahi kujaribu kujiua ili waondoe mfadhaiko,” laripoti gazeti The Globe and Mail. Mfadhaiko huo unaletwa na nini? Kati ya watu 1,002 waliochunguzwa, asilimia 43 walisema kwamba unaletwa na kazi. “Watu hutarajiwa kufanya kazi nyingi kupita uwezo wao wa kimwili na kiakili siku hizi,” asema Shimon Dolan, profesa wa Chuo Kikuu cha Montreal, anayechunguza tabia za watu katika mashirika. “Matokeo hukaziwa sana, lakini wakati huohuo, wafanyakazi hawana hakika na kazi yao, kwani kesho huenda wakafutwa.” Wakanada hushughulikaje na mfadhaiko? Jambo la kwanza ni kufanya mazoezi, lasema gazeti Globe, “halafu kusoma vitabu, kufanya mambo ambayo mtu anapenda, kucheza, kufanya marafiki, na kuwa pamoja na familia.”

Watoto Hutulia Wanaposoma Pamoja na Wazazi

“Kusoma pamoja na wazazi hupunguza utukutu wa watoto ambao wanapenda kupigana, kuiba, na kusema uwongo,” lasema gazeti The Times la London. Katika uchunguzi wa majuma kumi uliofanywa na Taasisi ya Magonjwa ya Akili, uliohusisha watoto 100 wenye umri wa miaka mitano au sita wanaoishi katikati ya London, wazazi waliambiwa hivi: “Kabla ya kuketi ili kusoma pamoja na watoto, zima simu za mkononi, taja mambo makuu ya hadithi, na utumie wakati fulani kutazama picha kabla ya kufungua kurasa.” Matokeo ya uchunguzi huo “yalithibitisha wazi kwamba mbinu nzuri zilizo rahisi za ulezi, zinaweza kufaulu sana katika kuboresha tabia za watoto tangu wakiwa na umri mdogo sana,” lasema gazeti hilo. “Jambo ambalo watoto wanahitaji hasa ni uangalifu,” anasema kiongozi wa utafiti huo Dakt. Stephen Scott. “Wanaweza kupata uangalifu huo iwapo wazazi watasoma pamoja nao.”

Wanaojitolea Wana Furaha

“Watu wanaofanya kazi ya kujitolea husema kwamba wanafurahia kazi yao, muda wa kazi, ushirika wa kijamii, na wana hali nzuri ya kiroho kuliko watu wengine,” laripoti gazeti The Sydney Morning Herald. Uchunguzi uliofanywa na kundi la watafiti nchini Australia ulionyesha kwamba wafanyakazi wa kujitolea “huridhika sana na afya yao, wakati wao wa kupumzika, na jinsi wanavyoutumia,” yasema ripoti hiyo. Profesa Bob Cummins wa Chuo Kikuu cha Deakin alisema kwamba kuna wafanyakazi wengi sana wa kujitolea nchini Australia—asilimia 32 ya wafanyakazi wote. Gazeti Herald pia liliripoti kwamba wale wanaofanya kazi ya kujitolea kwa zaidi ya saa 60 kila juma—wengi wakiwa wanawake wanaotoa utunzaji—“waliridhishwa na afya na kazi yao kuliko wale waliojitolea kwa saa chache.”

Kutoka Bahari ya Kaskazini Hadi Bahari ya Pasifiki

Baada ya kushindwa mara tatu, kundi la wavumbuzi Wajerumani lilifaulu kuabiri kutoka Bahari ya Kaskazini hadi Bahari ya Pasifiki likitumia meli yenye urefu wa meta 18, laripoti gazeti The Independent la London. Njia ya bahari waliyotumia iko karibu na pwani yenye barafu ya kaskazini ya Urusi. Mvumbuzi kutoka Sweden, Adolf Nordenskjöld, ndiye aliyepitia njia hiyo kwa mara ya kwanza mwaka wa 1879, akitumia meli iliyoendeshwa kwa mvuke na tanga. “Sijawahi kuona njia hiyo ikiwa imekosa barafu kama msimu huu wa kiangazi,” alisema kiongozi wa kundi hilo Arved Fuchs. “Tunadhani hali hiyo ilitokana na ongezeko la joto duniani na pepo zisizo za kawaida. Hivyo, barafu haikujikusanya katika eneo la pwani na tuliweza kusafiri hadi mwisho wa njia hiyo.” Wakitumia ndege inayoweza kutua baharini na picha za barafu zilizopigwa kutoka angani, waliweza kusafiri kilometa 15,000 kutoka Hamburg, Ujerumani hadi Provideniya, Urusi, katika Bahari ya Bering. Walisafiri kwa muda wa siku 127 bila kutumia meli ya kuvunja barafu. Wakati wa safari hiyo, wanaume hao walikula chakula ambacho hutumiwa na marubani wa anga za juu. Hata hivyo, mmoja wao alisema hivi: “Ugumu pekee tuliopata ni kuishi kwa muda wa miezi minne katika nafasi ndogo tukiwa na watu wengine 11.”