Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ya Kwanza Miaka 100 iliyopita

Ya Kwanza Miaka 100 iliyopita

Ya Kwanza Miaka 100 iliyopita

Hati ya kisheria ya Watch Tower Bible and Tract Society ilisajiliwa rasmi huko Pennsylvania, Marekani, mnamo Desemba 15, 1884. * Makao makuu ya sosaiti hiyo yalianzishwa huko. Baadaye, mnamo Aprili 23, 1900, majengo ya ofisi ya tawi ya kwanza yalinunuliwa huko London, Uingereza. Majengo hayo yalikuwa kwenye barabara ya 131 Gipsy Lane, Forest Gate, huko East London, kama inavyoonyeshwa hapa.

OFISI ya tawi hiyo ya kwanza ilipoanzishwa miaka mia moja iliyopita, Uingereza ilikuwa na Wanafunzi wa Biblia 138, kama Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo. Miaka miwili baadaye, katika mwaka wa 1902, ofisi ya tawi ya pili ilifunguliwa, huko Ujerumani; na kufikia mwaka wa 1904, ofisi nyingine za tawi zilikuwa zimeanzishwa huko Australia na Uswisi.

Katika mwaka wa 1918, Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ilipomalizika, kulikuwa na Wanafunzi wa Biblia 3,868 walioripoti utendaji wa kuhubiri ulimwenguni pote. Ofisi ya tawi ya tano ya Watch Tower Society ilianzishwa mwaka uliofuata—huko Kanada. Kisha, utendaji wa kuhubiri ujumbe wa Biblia ulipozidi kupamba moto, ofisi mpya za tawi zilianzishwa katika nchi nyinginezo nyingi, sita katika mwaka wa 1921 pekee.

Kufikia mwaka wa 1931, Wanafunzi wa Biblia walipokubali jina la Kibiblia Mashahidi wa Yehova, kulikuwa na ofisi za tawi 40 ulimwenguni pote. (Isaya 43:10-12) Katika miaka mitatu iliyofuata ofisi ziliongezeka hadi 49! Kufikia mwaka wa 1938 kulikuwa na kilele cha Mashahidi 59,047 wakihubiri katika nchi 52, lakini wakati huo utendaji wao wa Kikristo ulikuwa umeanza kugandamizwa na upinzani mkali katika sehemu mbalimbali.

Tawala za kiimla na za kimabavu zilipokuwa zikiibuka katika nchi moja hadi nyingine na kufyatuka kwa Vita ya Ulimwengu ya Pili mnamo Septemba 1939, ofisi za tawi za Mashahidi wa Yehova zilifungwa katika nyingi. Ni ofisi 25 tu zilizokuwa zikifanya kazi kufikia mwaka wa 1942. Kwa kushangaza, wakati wa hiyo vita mbaya zaidi katika historia ya wanadamu, ulimwenguni pote Mashahidi wa Yehova waliendelea na utendaji wao na kufurahia mojawapo ya ukuzi mkubwa zaidi katika historia yao ya kisasa.

Hata Vita ya Ulimwengu ya Pili ilipokuwa ikifikia kikomo katika mwaka wa 1945—na sehemu nyingi za ulimwengu zikiwa magofu—ofisi za tawi za Mashahidi zilifunguliwa upya na nyingine mpya kuanzishwa. Kufikia mwaka wa 1946 kulikuwa na ofisi za tawi 57 kote ulimwenguni. Na kulikuwako na Mashahidi wangapi watendaji? Kilele cha Mashahidi 176,456! Hicho kilikuwa mara tatu zaidi ya idadi ya mwaka wa 1938!

Ofisi za Tawi za Kwanza Zilivyopanuka

Katika mwaka wa 1911 ofisi ya tawi ya kwanza ya Watch Tower Society, huko London, Uingereza, ilihamia 34 Craven Terrace, ambako kulikuwa na nafasi tele ya ofisi na makao. Kisha mnamo Aprili 26, 1959, majengo mapya ya ofisi ya tawi yaliwekwa wakfu huko Mill Hill, London. Baadaye jengo la makao lilipanuliwa, na hatimaye (katika mwaka wa 1993) jengo la matbaa na maofisi lenye ukubwa wa meta 18,500 za mraba liliwekwa wakfu karibu na mahali hapo. Matbaa hiyo huchapa zaidi ya nakala milioni 90 za Mnara wa Mlinzi na Amkeni! katika lugha 23 kila mwaka.

Upanuzi wa ofisi ya tawi ya pili ya Sosaiti ulikuwa wenye kutokeza hata zaidi. Katika mwaka wa 1923 ofisi ya tawi ya Ujerumani ilihamia Magdeburg. Gazeti la Mnara wa Mlinzi la Julai 15, 1923, lilikuwa la kwanza kuchapwa katika matbaa hiyo ya Sosaiti. Katika miaka michache iliyofuata, uwanja uliokuwa karibu ulinunuliwa, majengo zaidi yakajengwa, na vifaa vya kujalidi na matbaa nyingine zilinunuliwa. Katika mwaka wa 1933, ofisi hiyo ya tawi ilitwaliwa na Wanazi, Mashahidi wakapigwa marufuku, na hatimaye Mashahidi elfu mbili kati yao wakapelekwa kwenye kambi za mateso.

Vita ya Ulimwengu ya Pili ilipomalizika katika mwaka wa 1945, majengo katika Magdeburg, iliyokuwa sasa sehemu ya Ujerumani Mashariki, yalirudishwa na ofisi ya tawi ikafunguliwa upya. Lakini mnamo Agosti 30, 1950, polisi wa Kikomunisti waliingia kwa kishindo katika majengo hayo na kuwakamata wafanyakazi, na Mashahidi katika Ujerumani Mashariki wakapigwa marufuku. Wakati huohuo, katika mwaka wa 1947 uwanja ulinunuliwa katika Wiesbaden, Ujerumani Magharibi. Katika miongo iliyofuata, majengo ya ofisi ya tawi yaliyokuwa yamejengwa mahali hapo yalipanuliwa mara kwa mara ili kukabiliana na uhitaji wa vichapo.

Kwa sababu ya uwanja kuwa mdogo katika Wiesbaden, eneo la ekari 75 lilinunuliwa karibu na Selters mwaka wa 1979. Baada ya ujenzi wa miaka mitano, ofisi ya tawi kubwa iliwekwa wakfu mnamo Aprili 21, 1984. Tangu wakati huo imepanuliwa ili kutoshea wafanyakazi wanaozidi elfu moja. Kila mwezi zaidi ya nakala milioni 16 za magazeti katika zaidi ya lugha 30 huchapishwa katika matbaa kubwa huko Selters; na katika mwaka wa hivi karibuni, zaidi ya vitabu milioni 18, kutia ndani Biblia zilitayarishwa katika kiwanda cha kujalidi cha mahali hapo.

Ofisi Nyingine Kubwa za Uchapishaji

Ofisi ya tawi ilianzishwa kwa mara ya kwanza huko Kobe, Japani, katika mwaka wa 1927, lakini mnyanyaso mkali dhidi ya Mashahidi wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili ulizuia utendaji wao. Punde tu, baada ya vita, ofisi ya tawi ilianzishwa upya huko Tokyo. Nafasi ilipozidi kuwa ndogo, ofisi mpya ya tawi ilijengwa huko Numazu. Iliwekwa wakfu mwaka wa 1973. Majengo hayo yaliposongamana kwa sababu ya ukuzi, majengo makubwa mapya yalijengwa huko Ebina, na kuwekwa wakfu mwaka wa 1982. Upanuzi wa majengo hayo yawezayo kukaa wafanyakazi 900, ulikamilika hivi karibuni. Zaidi ya nakala milioni 94 za magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! pamoja na mamilioni ya vitabu vilichapishwa mwaka wa 1999 katika lugha ya Kijapani pekee.

Upanuzi wa majengo ya ofisi ya tawi umekuwa ukiendelea katika nchi moja hadi nyingine. Ofisi ya tawi ilianzishwa huko Mexico City, Mexico, mwaka wa 1929. Kisha, idadi ya Mashahidi ilipofikia 60,000, majengo makubwa mapya yalijengwa nje ya mji. Yaliwekwa wakfu mwaka wa 1974, na upanuzi wake ulikamilika mwaka wa 1985 na 1989. Kwa sasa jengo jipya kubwa la matbaa na sehemu ya makao lakaribia kukamilika na kwa hiyo, karibuni ofisi ya tawi ya Mexico itaweza kukaa wafanyakazi 1,200. Tayari ofisi hiyo ya tawi inachapisha magazeti na vitabu kwa Mashahidi zaidi ya 500,000 na mamilioni ya watu wengine katika Mexico kutia ndani wale wanaoishi katika nchi jirani.

Katika mwaka wa 1923 ofisi ya tawi ilianzishwa Rio de Janeiro, Brazili, na baadaye majengo mapya yenye kuvutia yalijengwa huko. Lakini kwa kuwa mji wa São Paulo ndio kitovu cha biashara na uchukuzi katika Brazili, ofisi mpya ya tawi ilijengwa huko mwaka wa 1968. Kufikia katikati ya miaka ya 1970, Brazili ilikuwa na takriban Mashahidi 100,000. Hata hivyo, nafasi zaidi ya upanuzi haikupatikana katika São Paulo, hivyo uwanja wa ekari 285 ulinunuliwa huko Cesário Lange, yapata kilometa 150 nje ya São Paulo. Mnamo Machi 21, 1981, majengo ya ofisi ya tawi katika eneo hilo jipya yaliwekwa wakfu. Kwa sababu ya kupanuliwa kwa majengo katika eneo hilo jipya, ofisi hiyo ya tawi inaweza kukaa watu 1,200. Magazeti na vitabu huchapishwa Brazili kwa ajili ya nchi nyingi za Amerika Kusini na sehemu nyingine za ulimwengu.

Ofisi nyingine kubwa ya tawi ya uchapishaji ilikamilishwa mapema katika miaka ya 1990, karibu na Bogotá, Colombia. Magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! yanayogawanywa kotekote kaskazini-magharibi mwa Amerika Kusini huchapwa huko.

Ofisi nyingine za tawi zinazochapisha mamilioni ya magazeti kila mwaka ziko Afrika Kusini, Argentina, Australia, Finland, Hispania, Italia, Kanada, Korea, Nigeria, na Filipino. Ofisi ya tawi huko Italia huchapisha pia mamilioni ya vitabu, na Biblia katika lugha nyingi kila mwaka. Uchapishaji mkubwa wa kila mwaka unaofikia vitabu milioni 40 na magazeti zaidi ya bilioni moja, ungali unafanyiwa katika makao makuu ya Watch Tower Bible and Tract Society huko Brooklyn, New York, na katika matbaa iliyo kaskazini ya jimbo la New York.

Kwa kweli, ni jambo lisilo na kifani kwamba ofisi za tawi zimeongezeka kutoka moja miaka mia moja iliyopita hadi ofisi 109 leo na zinahudumia mahitaji ya Mashahidi wa Yehova katika nchi 234. Na wazia kwamba Wakristo waliojiweka wakfu takriban 13,000 wamejitolea kufanya kazi humo! Bila shaka, kazi yao na vilevile ile ya wale wajitoleaji 5,500 hivi walioko katika makao makuu ya Sosaiti imekuwa na sehemu muhimu katika kutimiza unabii wa Yesu Kristo kwamba ‘habari njema hii ya Ufalme wa Mungu itahubiriwa katika dunia yote inayokaliwa kwa ajili ya kuwa ushahidi kwa mataifa yote; kabla ya mwisho kuja.’—Mathayo 24:14.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Wakati huo iliitwa Zion’s Watch Tower Tract Society.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Tom Hart, inadhaniwa ndiye aliyekuwa Mwanafunzi wa Biblia wa kwanza Uingereza

[Picha katika ukurasa wa 18]

Ofisi ya tawi ya London huko 34 Craven Terrace (picha ya kulia)

[Picha katika ukurasa wa 18]

Majengo yanayotumika sasa huko London