Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Biashara ya Uhalifu Inayokua Haraka Zaidi

Biashara ya ulanguzi wa binadamu “ndio biashara ya uhalifu inayokua haraka zaidi ulimwenguni,” asema Pino Arlacchi, mkurugenzi mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Kupambana na Uhalifu. Kulingana na Bw. Arlacchi, inakadiriwa kwamba takriban watu milioni 200 wako mikononi mwa walanguzi hao. Ingawa watu milioni 11.5 walihamishwa kutoka Afrika kwa meli hadi Marekani katika ile miaka 400 ya utumwa, zaidi ya wanawake na watoto milioni 30 wamehamishwa nje au ndani ya eneo la Kusini-mashariki mwa Asia katika mwongo mmoja tu uliopita. Wengi wao wanatumikishwa katika biashara zenye kudhulumu au kwa makusudi ya ngono. Bw. Arlacchi anapendekeza kwamba serikali zirejeshe tena sheria za kupinga utumwa.

Mateso na Ukatili Ulaya

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika la Amnesty International, “kifo wakati wa kuhamishwa kinguvu, mateso gerezani, kuteswa na polisi hatua kwa hatua, na kugandamizwa kwa sababu ya kabila na dini,” ni baadhi ya matendo yanayokiuka haki za binadamu katika Ulaya. “Ingawa watu wengi huko Ulaya hufurahia haki za binadamu kwa kadiri fulani, watu fulani, kutia ndani wakimbizi na vikundi vidogo vya kikabila na vya kidini, huendelea kukabili hali inayopingana na maoni ya kuwa Ulaya ni kitovu cha haki za binadamu na uhuru,” yasema ripoti hiyo. “Uthibitisho mkubwa zaidi ni ripoti za kuenea na kuongezeka kwa ukatili wa polisi. Kutoka Uingereza hadi Azerbaijan, watu mmoja-mmoja wametendewa . . . kikatili, kinyama au kudhalilishwa na polisi.” Shirika hilo linadai kwamba wale wanaofanya mambo hayo kwa kawaida hawahukumiwi. Linataja mfano ufuatao: “Mnamo Julai [1999], Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu ilipata Ufaransa ikiwa na hatia ya kukiuka kanuni za kimataifa kuhusu mateso na haki ya kusikilizwa ifaavyo mahakamani” kuhusiana na mhamiaji mmoja aliyetiwa korokoroni na polisi. “Mwishoni mwa mwaka polisi waliohusika bado walikuwa kazini,” ripoti hiyo yazidi kueleza.

Wazeewazee Wastahili Heshima

Uchunguzi wa miezi sita uligundua kwamba maneno ya kitoto yanatumika sana katika makao ya kutunzia wazeewazee. Kijarida cha afya cha Ujerumani Apotheken Umschau charipoti kwamba, kuongea na wazeewazee kwa maneno ya kitoto hakuwanyang’anyi tu adhama yao bali pia hudhuru hali yao njema. Ukosefu huo wa heshima hudhuru afya. Christine Sowinski, wa Shirika la Wenye Kutunza Wazeewazee la Ujerumani asema hivi: “Kadiri wazeewazee wanavyokosa kuheshimiwa ndivyo wanavyodhoofika kimwili na kiakili.” Anapendekeza kwamba maneno hasi na ya kitoto yasitumiwe wakati wa kuwahudumia watu wazeewazee, “kwa kuwa maneno yanayotumiwa yataelekea kuathiri mtazamo wako.”

Watu wa Kidini Huishi Muda Mrefu Zaidi?

“Kulingana na ukaguzi wa takwimu za uchunguzi mbalimbali 42 uliochapishwa juu ya habari hii tangu mwaka wa 1977, kujihusisha kwa ukawaida katika utendaji wa kidini, huenda sawia na hali njema ya afya na maisha marefu,” lasema gazeti la Science News. “Wanasayansi hao walisema takwimu zaonyesha kwamba utendaji wa kidini, hasa wa peupe, hurefusha maisha.” Sababu kadhaa zimetolewa kwa uamuzi huo—kuepuka mazoea yanayohatarisha uhai, ndoa thabiti, kutovunjika moyo kwa sababu ya mambo yasiyoweza kudhibitiwa, rafiki wengi, pamoja na hisia na mielekeo chanya. Ripoti moja ilifikia mkataa huu: “Imegunduliwa kuwa uhudhuriaji wa mikutano ya kidini kwa ukawaida . . . hurefusha maisha, hasa miongoni mwa wanawake. Wanaohudhuria kwa ukawaida mikutano ya kidini . . . walisema wana utegemezo mkubwa wa marafiki, uwezekano mdogo wa kupatwa na mshuko-moyo, na wana mazoea mazuri ya afya.”

Idadi ya Watu India Yapita Bilioni Moja

Ilisemekana kwamba idadi ya watu India ilifikia bilioni moja mnamo Mei 11, 2000. Hata hivyo, shirika la habari la Associated Press lilisema hivi: “Ni vigumu kuamua hususa wakati ambapo India ilifikia idadi ya watu bilioni 1 kwa sababu watoto 42,000 wanazaliwa kila siku na rekodi za hospitali huwa si kamili.” Kwa sababu ya ukuzi wa idadi ya watu, njaa na kutojua kusoma na kuandika huongezeka, licha ya maendeleo makubwa yaliyofanywa katika nyanja ya uzalishaji wa chakula na elimu. Ijapokuwa mamilioni wanaishi katika ufukara, kila mtoto anayezaliwa huonwa kuwa mleta-riziki mpya, ambaye ataweza kufanya kazi na kusaidia kukimu familia.

Azuiwa na Wale Alionuia Kuokoa

“Baharia mmoja wa California aliyefunga safari ya kuvuka bahari ya Pasifiki akiwa peke yake, iliyokusudiwa kuokoa nyangumi alilazimika kuvunja safari hiyo . . . baada ya kukumbana na nyangumi wawili,” laripoti gazeti la The New York Times. Baharia huyo, Michael Reppy, alianza safari yake huko San Francisco akielekea Yokohama, Japani. Alikusudia kuvuka kwa wakati mfupi iwezekanavyo akiwa katika merikebu yake ya kasi yenye urefu wa meta 18 iitwayo Thursday’s Child, “ili kutangaza hali yenye kusikitisha ya nyangumi walio utekwani.” Lakini siku ya kwanza tu ya safari yake, nyangumi wawili “walipita karibu kwa kishindo,” na kufanya isiwezekane kudhibiti merikebu. “Aligundua kwamba sehemu ya chini ya usukani ilikuwa haipo, ikiwa imevunjwa na nyangumi hao walipokuwa wakipita,” likasema gazeti Times. Safari yake ya kwanza katika mwaka wa 1997 “iliyokusudiwa kutangaza hali yenye kusikitisha ya viumbe wa bahari” ilikoma merikebu yake ilipopinduka yapata kilometa 500 kutoka Tokyo.

DDT Yatumiwa Kupambana na Malaria

“Dawa ya kuua wadudu, DDT, ambayo imepigwa marufuku kwa miaka isiyozidi 30 katika Ulaya na Marekani, huenda isiharamishwe ulimwenguni pote kwa sababu ya uwezo wake wa kuwaua mbu ambao ni chanzo cha mojawapo ya visababishi vikuu vya kifo ulimwenguni—malaria,” laripoti gazeti BBC Wildlife. “Ingawa DDT ni sumu kali sana yenye kuathiri vibaya wanyama-pori, watetezi wa afya wanasema kwamba DDT ni muhimu sana katika jitihada za kupambana na malaria, ugonjwa unaoua watu milioni 2.7 kila mwaka na kufanya takriban watu 500 wawe na malaria ya kudumu.” Ingawa Shirika la Afya Ulimwenguni launga mkono kupigwa marufuku kwa matumizi ya DDT katika kilimo, lasema kwamba dawa hiyo yapasa kutumiwa tu katika kupambana na malaria hadi dawa salama na yenye uwezo itakapopatikana.

Kasa wa Baharini Waonekana Tena!

Wahifadhi wa wanyama wametiwa moyo watembelee pwani ya mashariki ya India mwaka huu ili kuona idadi kubwa zaidi iliyowahi kuonekana tangu katikati ya miaka ya 1980 ya kasa aina ya Olive Ridley wakitaga mayai. Kwa mujibu wa gazeti la kimazingira Down to Earth, hilo ni jambo la kustaajabisha kwa sababu ufuo wa jimbo la Orissa uliharibiwa vibaya sana na kimbunga katika mwaka wa 1999. Ufuo huo ndio eneo kubwa zaidi ulimwenguni wanakozalia viumbe hao walio katika hatari ya kutoweka. Kati ya Machi 13 na 20, zaidi ya kasa 1,230,000 waliibuka kutoka baharini, na 711,000 kati yao walitaga mayai, hata hivyo 28,000 waliuawa karibu na ufuo na boti kubwa za kuvulia samaki. Adui wa kasa ni wengi—nguruwe-mwitu, mbwa-mwitu wanaokula mayai, wawindaji-haramu wanaouza nyama ya kasa kwa watu wanaopenda mlo huo, na boti kubwa zenye nyavu zisizokuwa na “vifaa vya kuwaondoa kasa.”

Mnururisho wa Chernobyl

Msiba wa nyuklia wa Chernobyl mnamo mwaka 1986 “utatokeza visa vipya 50,000 vya kansa ya kikoromeo miongoni mwa vijana wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa sana,” lasema gazeti The Guardian la London. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni, kufikia sasa zaidi ya watu milioni saba wameshikwa na kansa hiyo ilhali idadi kamili huenda isijulikane kamwe. Watoto milioni tatu wanahitaji matibabu, ilhali wengine watakufa mapema. Inasemekana kwamba watu 73,000 katika Ukrainia wamelemaa kabisa. Asilimia 23 hivi ya watu waliohusika na usafishaji huo walilemazwa, huku sehemu moja kwa tano ya msitu katika Belarus bado imechafuliwa. Kwenye utangulizi wa ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa UM, Kofi Annan alisema hivi: “Sote tunatamani kulifuta neno Chernobyl katika kumbukumbu zetu,” lakini “wanadamu wenzetu wanaozidi milioni 7 hawawezi kusahau. Bado wanateseka kila siku kutokana na yaliyotendeka.”

Kanisa Kwenye Kompyuta

Dayosisi ya askofu mkuu ya Kanisa Katoliki la Winnipeg, Manitoba, Kanada, ina mpango wa “kuanzisha mfumo wa kompyuta ili kuwaandalia waumini fursa ya kutafakari, kuungama dhambi na kutafuta ushauri wa padri kupitia kwa kompyuta,” laripoti gazeti la Calgary Herald. Mkurugenzi wa mawasiliano wa dayosisi hiyo Richard Osicki, anatumaini kwamba mfumo huo utawachochea Wakristo wengi wasiotenda waanze tena kutenda, asilimia 75 hivi kati yao hawaendi kabisa kanisani. “Tunaandaa huduma za kidini nje ya kanisa. Hivyo waweza kuwasiliana na Mungu ukiwa umeketi mbele ya kompyuta yako,” akasema.