Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wenye Kustaajabisha Wadudu

Wenye Kustaajabisha Wadudu

Wenye Kustaajabisha Wadudu

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA HISPANIA

JE, WEWE huwaona wadudu kuwa wasumbufu tu? Je, ungependa wadudu hawa wasumbufu waondolewe ulimwenguni? Je, wewe huwapulizia viuadudu, huwaua, au huwakanyaga uwaonapo? Kabla ya kuazimia kuua kila mdudu unayekutana naye, mbona usijaribu kujifunza jambo fulani kuwahusu? Kwa vyovyote vile, waweza kuwa na hakika kwamba wadudu watakuwepo daima kwa sababu ni wengi sana kwa kadiri ya wadudu 200,000,000 kwa kila mwanadamu!

Unapochunguza kifupi wachache kati ya viumbe hawa wenye kustaajabisha utasadiki kwamba kwa kweli wadudu wanastahili staha.

Mabingwa wa Kuruka Wenye Umbo la Kustaajabisha

Wadudu wengi ni mabingwa wa kuruka. Fikiria mifano kadhaa. Mbu wanaweza kuruka wakiwa wamepinduka. Wengine hata wanaweza kuruka katika mvua pasipo kulowa—ndiyo, wakiepa kihalisi matone ya mvua! Nyigu na nyuki fulani wa tropiki huruka kwa mwendo wa karibu kilometa 72 kwa saa. Kipepeo-maliki mmoja wa Amerika Kaskazini alisafiri umbali wa kilometa 3,010 alipokuwa akihama. Nzi aina ya hover waweza kupigapiga mabawa yao zaidi ya mara 1,000 kwa sekunde—kwa kasi zaidi ya ndege-wavumaji. Kereng’ende wanaweza kuruka kinyumenyume, jambo ambalo limechochea watafiti kufanya uchunguzi wa makini.

Ikiwa umejaribu kumwua nzi, wajua kwamba wadudu hawa wana macho yenye uwezo isivyo kawaida, yenye tendo-lisohiari linalopita la mwanadamu mara kumi kwa wepesi. Kwa kupendeza, nzi ana jicho lenye lenzi nyingi zenye pande sita, kila lenzi huwasilisha habari tofauti. Hivyo basi, yaelekea kwamba nzi huona vitu kwa visehemu-sehemu.

Wadudu fulani waweza kuona nuru ya urujuani, isiyoonwa na binadamu. Hivyo, kipepeo tunayemwona akiwa na rangi nyeupe iliyochakaa haonwi hivyo na yule wa kiume. Kwa kweli, kipepeo wa kike huwa na umaridadi wenye kuvutia yule wa kiume kwenye nuru ya urujuani.

Wadudu wengi hutumia macho yao kama dira. Kwa mfano, nyuki na nyigu wanaweza kutambua bapa ya tanzu ya nuru yenye uelekeo hususa, hilo huwawezesha kujua mahali jua lilipo angani—hata lifunikwapo na mawingu. Kwa msaada wa uwezo huo, wadudu hawa wanaweza kutafuta chakula mbali na viota vyao na kurejea bila kupotea.

Upendo Uko Hewani

Kwa kawaida wadudu hutafuta wenzi kwa kuitikia sauti na harufu—hilo ni muhimu endapo unaishi tu kwa muda wa majuma machache huku wenzi wanaofaa wakiwa haba.

Nondo-maliki wa kike hupata mwenzi kwa kutokeza harufu yenye nguvu sana kiasi cha kumvutia nondo wa kiume aliye umbali wa kilometa 11 hivi. Vipapasio vyake vinavyohisi kwa wepesi vyaweza kutambua molekuli moja ya harufu hiyo.

Chenene, panzi, na nyenje hutoa sauti. Hata sisi wanadamu twaweza kumsikia nyenje mwenye ashiki nyingi anapovumisha mwili wake mzima. Kwani, kikundi kikubwa cha nyenje wanaotafuta wenzi chaweza kutokeza mshindo wa juu kupita keekee inayoendeshwa kwa nguvu! Kinyume chake, nyenje fulani wa kike hawatoi sauti yoyote.

Kuamka na Kujipasha Joto

Kujipasha joto ni muhimu kwa wanadamu wanaoishi sehemu zenye baridi. Ndivyo ilivyo na wadudu wenye damu baridi wanaojikuta wameganda kabisa kila asubuhi. Jua huwanufaisha, nao huliota kikamili.

Nzi na mbawakavu hupenda kuota jua kwenye maua au matawi mapema asubuhi. Mbawakavu fulani hupenda sana yungiyungi wa Australia unaotenda kama kipasha-joto cha mimea, hupasha maua yake joto kufikia nyuzi Selsiasi 20 zaidi ya joto la mazingira. Vipepeo huwa na mfumo wa kujipasha joto mwilini tofauti na mbawakavu. Wanapotaka kujipasha joto, wao hutandaza mabawa yao, yanayotenda kama paneli bora za kunasa jua, wakiyaelekeza juani.

Wadudu Hutekeleza Kazi Nyingi!

Kila jamii ya wadudu hutekeleza kazi tofauti, hata kazi za ajabu. Kwa mfano, nondo fulani hupata chumvi na unyevu ulio muhimu kwa uhai kwa kufyonza machozi ya nyati. Wadudu wengine, wenye kishusha-gando bora, huishi katika vilele vya milima vyenye barafu nao hujikimu kwa kula wadudu waliokufa kwa baridi.

Sawa na alivyosema Mfalme Solomoni mwenye hekima maelfu ya miaka mapema, chungu hasa hufanya kazi kwa bidii. Solomoni aliandika: “Ewe mvivu, mwendee chungu, zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, wala msimamizi, wala mkuu, lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.” (Mithali 6:6-8) Kutokuwapo kwa msimamizi ni jambo la kustaajabisha sana ufikiriapo kwamba makundi fulani ya chungu yaweza kuwa na chungu zaidi ya milioni 20! Na bado, “jiji” hilo la wadudu huendeshwa sawasawa, kila chungu akitekeleza kazi yake hususa, hivi kwamba kundi zima linapata chakula, ulinzi, na makao.

Huenda vilima vya mchwa ndio makao ya wadudu yenye kuvutia zaidi. Vingine huwa na urefu wa meta 7.5. * Majengo haya yenye kustaajabisha huwa na mfumo tata wa kusafisha hewa na bustani za kuvu ardhini. Jambo lenye kustaajabisha hata zaidi ni kwamba mchwa wanaojenga piramidi hizi ndefu ni vipofu!

Sababu Tunahitaji Wadudu

Wadudu ni muhimu kwa maisha yetu ya kila siku. Kwa kweli, takriban asilimia 30 ya vyakula tunavyokula hutegemea uchavushaji wa nyuki, hasa nyuki mwitu. Lakini uchavushaji ni mojawapo tu ya kazi muhimu zinazofanywa na wadudu. Wadudu husafisha dunia kwa njia bora sana, kwa kutayarisha mbolea kwa mimea na wanyama waliokufa. Hivyo, udongo hupokea rutuba inayowezesha mimea kukua. “Pasipo wadudu,” aandika mtaalamu wa elimu ya wadudu Christopher O’Toole katika kitabu chake Alien Empire, “tungefunikwa na mbolea ya mimea na wanyama waliokufa.”

Wadudu wasipofanya kazi yao watu huteseka sana. Fikiria jambo lililotukia Australia, nchi yenye mamilioni ya ng’ombe. Ng’ombe husambaza kinyesi chao kila mahali. Mbali na kwamba samadi hiyo ilichukiza, iliandaa mahali pa bush fly kutaga mayai—pigo kwa wanadamu na ng’ombe. Kwa hiyo viviringamavi wakaletwa kutoka Ulaya na Afrika. Tatizo hilo likatatuliwa!

Ni Rafiki au Adui?

Kwa wazi, wadudu fulani hula mazao na kusambaza magonjwa. Lakini ni takriban asilimia 1 tu ya wadudu ulimwenguni wanaoonwa kuwa waharibifu, na wengi wao huharibu kwa sababu ya jinsi ambavyo mwanadamu mwenyewe amevuruga mazingira. Kwa mfano, mbu anayesababisha malaria hatatizi sana wenyeji wa msitu ulio karibu na ikweta. Hata hivyo, yeye huwa hatari katika miji iliyo karibu na msitu huo, ambako kuna maji mengi yaliyotuama.

Mara nyingi, mwanadamu anaweza kudhibiti kwa urahisi wadudu wanaoharibu mazao, ama kwa kubadilisha mazao ama kwa kuleta au kuhifadhi maadui wa wadudu hawa. Wadudu wapole wanaoitwa ladybug na lacewing huzuia kwa mafanikio shambulio la wadudu wanyonyaji. Na huko Kusini-mashariki ya Asia, wafanyakazi wa afya ya umma waligundua kwamba mabuu kadhaa ya kereng’ende yanaweza kuondoa viluwiluwi vya mbu kutoka katika tangi la maji.

Hivyo basi, wadudu wajapoleta hasara fulani wao ni sehemu muhimu ya ulimwengu wa asili tunaotegemea. Kama Christopher O’Toole anavyosema, ingawa wadudu wanaweza kuishi pasipo wanadamu, “hatuwezi kuishi bila wadudu.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 20 Kwa wanadamu, kazi sawa na hiyo ingekuwa jengo lenye urefu wa zaidi ya kilometa tisa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16, 17]

BADILIKO LA UMBO—Umbo Jipya, na Mtindo Mpya wa Maisha

Wadudu fulani hubadili kabisa umbo lao kupitia kwa hatua inayoitwa badiliko la umbo. Umbo laweza kubadilika kabisa. Viluwiluwi hugeuka na kuwa nzi, viwavi huwa vipepeo, na mabuu ya majini huwa kereng’ende wanaoruka hewani. Mamia ya maelfu ya wadudu hubadilika umbo.

Ili kuwepo na badiliko hilo la umbo—linalolingana na kubadili treni iwe ndege—ni lazima mabadiliko makubwa yatukie ndani ya mwili wa mdudu. Kwa kielelezo, fikiria kipepeo. Ijapokuwa buu la kiwavi huwa bwete, nyingi za tishu na sehemu zilizokuwa mwilini huharibika na sehemu nyingine mpya zilizokomaa—kama vile mabawa, macho, na vipapasio—hutokea.

Kwa kawaida, badiliko hilo la umbo huhusisha kuanza mtindo mpya wa maisha. Kwa mfano, kereng’ende huwinda samaki wadogo au viluwiluwi anapokuwa buu; lakini anapokomaa na kuruka, yeye huanza kula wadudu. Hilo ni sawa na mtu kuogelea baharini miaka 20 ya kwanza ya maisha yake kisha kuruka hewani kama ndege miaka inayosalia.

Je, mabadiliko haya ya umbo yenye kustaajabisha yalitokana na mageuzi? Kiwavi angeweza kuibukaje tu, akiwa tayari kujibadili umbo awe kipepeo? Hivyo basi, ni yupi aliyetokea kwanza—ni kiwavi au ni kipepeo? Mmoja wao hawezi kuwapo bila mwingine, kwa kuwa ni kipepeo tu anayetaga mayai.

Kwa hakika, kubadilika umbo hutoa ushahidi wenye kusadikisha wa kuwapo kwa Mbuni Mkuu, anayetajwa na Biblia kuwa Muumba wa vitu vyote, Mungu Mweza Yote.—Zaburi 104:24; Ufunuo 4:11.

[Picha]

“Swallowtail” aliyetoka tu kwenye pupa, anyoosha mabawa yake

[Picha katika ukurasa wa 18]

Juu: Mbawakavu ambaye hula chavua

Juu kulia: Mbawakavu wa jani aliyefunikwa na umande ajipasha joto

Kulia mwisho: Mbawakavu aina ya “rhinoceros”

[Picha katika ukurasa wa 18]

Panzi wa Afrika mwenye pembe fupi

[Picha katika ukurasa wa 18]

“Horsefly”