Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Uhitaji Unaoongezeka wa Tiba na Upasuaji Bila Damu

Uhitaji Unaoongezeka wa Tiba na Upasuaji Bila Damu

Uhitaji Unaoongezeka wa Tiba na Upasuaji Bila Damu

“Wale wote wanaoshughulika na damu na wagonjwa wanaopasuliwa wahitaji kufikiria upasuaji bila damu.”—Dakt. Joachim Boldt, profesa wa unusukaputi, Ludwigshafen, Ujerumani.

MSIBA wa UKIMWI umewashurutisha wanasayansi na matabibu wachukue hatua zaidi ili kufanya chumba cha upasuaji kiwe mahali salama zaidi. Bila shaka, hilo limemaanisha damu ichunguzwe zaidi. Lakini wataalamu wanasema kwamba hata hatua hizo hazimalizi kabisa hatari zinazoletwa na utiaji-damu mishipani. “Hata wakati ambapo jumuiya inatumia rasilimali nyingi kufanya damu iwe salama zaidi kuliko wakati mwingine wowote,” lasema gazeti Transfusion, “twaamini kwamba bado wagonjwa wataepuka kutiwa damu kwa sababu tu damu haiwezi kamwe kuwa salama kabisa.”

Basi haishangazi kwamba madaktari wengi wanatahadhari kutumia damu. “Kwa msingi utiaji-damu mishipani si jambo jema, na tunajitahidi vilivyo kuuepuka kwa kila mtu,” asema Dakt. Alex Zapolanski, wa San Francisco, California.

Umma pia unazidi kufahamu hatari za kutiwa damu mishipani. Kwa kweli, kura ya 1996 ilifunua kwamba asilimia 89 ya Wakanada wangependelea njia badala kuliko kutiwa damu mishipani. “Si wagonjwa wote watakaokataa damu kutoka kwa mtu mwingine kama wafanyavyo Mashahidi wa Yehova,” lasema jarida Journal of Vascular Surgery. “Hata hivyo, hatari za kupitishwa kwa maradhi na kuvuruga mfumo wa kinga ni uthibitisho dhahiri kwamba lazima tutafute njia badala kwa ajili ya wagonjwa wetu wote.”

Njia Inayopendelewa

Jambo la kutia moyo ni kwamba, kuna njia badala—tiba na upasuaji bila damu. Wagonjwa wengi hawaioni kuwa hatua ya mwisho bali utibabu unaopendelewa, wakiwa na sababu nzuri. Stephen Geoffrey Pollard, daktari-mpasuaji na mshauri wa Uingereza asema kwamba viwango vya kupatwa na maradhi na vya vifo miongoni mwa watu wanaofanyiwa upasuaji bila damu “angalau vyatoshana na viwango vya kupatwa na maradhi na vya vifo miongoni mwa wagonjwa wanaopokea damu, na katika visa vingi wale wanaofanyiwa upasuaji bila damu huepuka maambukizo ya baada ya upasuaji na matatizo ambayo mara nyingi huhusiana na damu.”

Tiba bila damu ilisitawije? Katika maana moja swali hilo hushangaza, kwa kuwa tiba bila damu kwa kweli ni ya kale zaidi kuliko matumizi ya damu. Kwa kweli, ni kufikia mapema katika karne ya 20 kwamba tekinolojia ya utiaji-damu mishipani ilifikia kiwango cha kutumiwa kwa ukawaida. Hata hivyo, katika miongo ya karibuni watu fulani wamefanya upasuaji bila damu upendwe na watu. Kwa mfano, katika miaka ya 1960 daktari-mpasuaji mashuhuri Denton Cooley alifanya upasuaji wa kwanza wa moyo bila kutumia damu.

Kwa kuwa visa vya mchochota wa ini viliongezeka miongoni mwa wagonjwa waliotiwa damu katika miaka ya 1970, madaktari wengi walianza kutafuta njia badala za damu. Kufikia miaka ya 1980 idadi kadhaa ya vikundi vikubwa vya matabibu walikuwa wakifanya upasuaji bila damu. Kisha, ugonjwa wa kuenea wa UKIMWI ulipozuka, vikundi hivyo viliombwa ushauri mara kadhaa na vikundi vingine vilivyokuwa na hamu ya kutumia mbinu hizohizo. Katika miaka ya 1990 hospitali nyingi zilitokeza programu zinazowaruhusu wagonjwa wachague kutibiwa bila damu.

Sasa madaktari wamefanikiwa kutumia mbinu zisizohusisha damu wakati wa upasuaji na wa hatua za dharura ambazo kwa kawaida zilihitaji damu. “Upasuaji hatari wa moyo, mishipa, uzazi, mifupa, na mfumo wa mkojo unaweza kufanywa kwa mafanikio bila kutumia damu au vitu vyenye damu,” asema D. H. W. Wong, katika jarida la Canadian Journal of Anaesthesia.

Faida moja ya upasuaji bila damu ni kwamba huendeleza utunzaji bora. “Ustadi wa daktari-mpasuaji ni wa maana zaidi ili kuzuia kupoteza damu,” asema Dakt. Benjamin J. Reichstein, mkurugenzi wa upasuaji huko Cleveland, Ohio. Jarida la kisheria la Afrika Kusini lasema kwamba katika visa fulani upasuaji bila damu unaweza kuwa “wa haraka zaidi, safi zaidi na wa gharama ya chini zaidi.” Laongezea hivi: “Kwa hakika tiba ya utunzaji wa baadaye katika visa vingi imekuwa ya gharama ya chini zaidi na isiyochukua muda mwingi.” Hizi ni sababu chache zinazofanya kuwe na hospitali zipatazo 180 sasa ulimwenguni pote zenye programu mahususi za tiba na upasuaji bila damu.

Mashahidi wa Yehova na Damu

Mashahidi wa Yehova hukataa kutiwa damu mishipani kwa sababu zinazotegemea Biblia. * Lakini wao hukubali—na hufuatia kwa dhati—tiba iliyo badala ya damu. “Mashahidi wa Yehova hutafuta kwa bidii tiba iliyo bora zaidi,” akasema Dakt. Richard K. Spence, alipokuwa mkurugenzi wa upasuaji kwenye hospitali moja ya New York. “Wakiwa kikundi, ndio wateja walioelimika zaidi ambao daktari-mpasuaji atapata kukutana nao.”

Madaktari wamefaulu kutumia mbinu nyingi za upasuaji bila damu kwa Mashahidi wa Yehova. Fikiria aliyojionea daktari-mpasuaji wa moyo Denton Cooley. Kwa miaka 27, kikundi chake kilifanya upasuaji wa moyo bila kutumia damu kwa Mashahidi wa Yehova 663. Matokeo hudhihirisha kwamba upasuaji wa moyo unaweza kufanywa kwa mafanikio bila kutumia damu.

Ni kweli kwamba wengi wamewachambua Mashahidi wa Yehova kwa kukataa damu. Lakini kitabu cha mwongozo kilichochapishwa na Shirika la Madaktari-Nusukaputi wa Uingereza na Ireland chaita msimamo wa Mashahidi wa Yehova “ishara ya kuheshimu uhai.” Kwa kweli, msimamo thabiti wa Mashahidi umechangia sehemu kubwa katika kutokeza tiba iliyo salama zaidi inayopatikana kwa wote. “Mashahidi wa Yehova waliohitaji kufanyiwa upasuaji wameonyesha njia na kutilia mkazo kufanywa kwa maendeleo katika sekta muhimu ya Norway ya huduma za afya,” aandika Profesa Stein A. Evensen, wa Hospitali ya Taifa ya Norway.

Ili kusaidia madaktari watibu bila kutumia damu, Mashahidi wa Yehova wamebuni huduma za uhusiano zenye kusaidia. Kwa sasa, zaidi ya Halmashauri za Uhusiano na Hospitali 1,400 ulimwenguni pote zimetayarishwa kuandalia madaktari na watafiti vichapo vya kitiba kutoka habari iliyohifadhiwa kwenye kompyuta yenye makala zaidi ya 3,000 zinazohusu tiba na upasuaji bila damu. “Si Mashahidi wa Yehova tu, bali pia wagonjwa wote kwa ujumla, leo hawatatiwa damu isivyo lazima kwa sababu ya kazi ya Halmashauri za Mashahidi za Upatanisho na Hospitali,” asema Dakt. Charles Baron, profesa katika Boston College Law School. *

Habari inayohusu tiba na upasuaji bila damu ambayo imekusanywa na Mashahidi wa Yehova imefaidi wengi katika uwanja wa kitiba. Kwa mfano, walipokuwa wakitayarisha habari ya kitabu chenye kichwa Autotransfusion: Therapeutic Principles and Trends, waandishi waliwaomba Mashahidi wa Yehova wawape habari kuhusu njia zilizo badala ya kutiwa damu mishipani. Mashahidi walikubali ombi lao kwa furaha. Waandishi hao walishukuru na baadaye wakasema: “Katika kusoma habari hiyo yote, hatujapata kuona orodha iliyo sahihi, na kamili ya mbinu za kuzuia kutiwa damu ya mtu mwingine kwenye mishipa.”

Maendeleo katika uwanja wa kitiba yamefanya wengi wafikirie tiba bila damu. Twaweza kutarajia maendeleo gani wakati ujao? Profesa Luc Montagnier, aliyegundua virusi vya UKIMWI, asema: “Badiliko bora la uelewevu wetu katika uwanja huu laonyesha kwamba siku moja utiaji-damu mishipani utakoma.” Kwa wakati uliopo, tayari njia badala ya damu zinaokoa uhai wa wengi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 16 Zinapoalikwa, Halmashauri za Uhusiano na Hospitali hutolea wafanyakazi wa hospitali mihadhara. Kwa kuongezea, msaada wao ukihitajika kihususa, wanasaidia wagonjwa wawe na mawasiliano ya mapema, ya wazi na yenye kuendelea pamoja na tabibu anayehusika.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Wanavyosema Madaktari Fulani

‘Upasuaji bila damu si kwa ajili ya Mashahidi wa Yehova peke yao bali ni kwa ajili ya wagonjwa wote. Nafikiri kwamba kila daktari apaswa kuutumia.’—Dakt. Joachim Boldt, profesa wa unusukaputi, Ludwigshafen, Ujerumani.

“Ingawa kutiwa damu mishipani ni salama zaidi ya wakati uliopita, bado kwahusisha hatari, zinazotia ndani maitikio ya kinga na kupatwa na mchochota wa ini au maradhi yanayopitishwa kingono.” —Dakt. Terrence J. Sacchi, tabibu aliye naibu wa profesa wa tiba.

“Kuhusu utiaji-damu mishipani, matabibu wengi hutenda mara moja kwa kuwatia watu damu kwa wingi bila kubagua. Mimi sifanyi hivyo.” —Dakt. Alex Zapolanski, mkurugenzi wa upasuaji wa moyo kwenye Taasisi ya Moyo ya San Francisco.

“Sioni upasuaji wowote wa tumbo ulio wa kawaida kwa mgonjwa wa kawaida ukihitaji utiaji-damu mishipani.” —Dakt. Johannes Scheele, profesa wa upasuaji, Jena, Ujerumani.

[Picha]

Dakt. Joachim Boldt

Dakt. Terrence J. Sacchi

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Tiba na Upasuaji Bila Damu

Baadhi ya Mbinu

Umajimaji: Mchanganyiko wa chumvi wa ringer, dextran, wanga wa hydroxyethyl, na mingineyo hutumiwa kudumisha kiasi cha damu, na kuzuia mshtuko unaosababishwa na kupungua kwa damu inayozunguka mishipa ni. Baadhi ya umajimaji unaofanyiwa majaribio sasa unaweza kusafirisha oksijeni.

Dawa: Kubadilishwa jeni kwa protini fulani kwaweza kuchochea kutokezwa kwa chembe nyekundu za damu (erythropoietin), vigandisha-damu (interleukin-11), na chembe nyeupe za damu za namna mbalimbali (GM-CSF, G-CSF). Dawa nyingine hupunguza sana kuvuja damu wakati wa upasuaji (aprotinin, antifibrinolytic) au husaidia kupunguza kuvuja damu sana (desmopressin).

Gundi ya vitu hai: Pedi zilizofumwa za collagen na selulosi hutumiwa ili kukomesha kuvuja damu zinapotumiwa moja kwa moja. Gundi ya fibrin na vizibo vinaweza kuziba vidonda au kufunika sehemu kubwa za tishu zinazovuja damu.

Kuokoa damu: Mashine za kuokoa huzuia uvujaji wa damu wakati wa upasuaji au vurugu. Damu hiyo husafishwa na inaweza kurudishwa kwa mgonjwa katika mzunguko usiokatishwa. Katika visa visivyo vya kawaida, lita nyingi za damu zinaweza kuokolewa kwa kutumia mfumo huo.

Vifaa vya upasuaji: Vifaa fulani hukata na kuziba mishipa ya damu wakati uleule. Vifaa vingine vinaweza kuziba kuvuja damu kwenye sehemu kubwa za tishu. Kifaa kinachoitwa laparoscope pamoja na vifaa vingine vyenye ncha kali sana huwezesha upasuaji ufanywe bila kuvuja damu kutoka katika sehemu kubwa iliyokatwa.

Mbinu za upasuaji: Mipango kamili ya upasuaji, kutia ndani kushauriana na matabibu wenye uzoefu, husaidia kikundi cha upasuaji kuepuka hali zenye kutatanisha. Hatua ya haraka ya kukomesha kuvuja damu ni muhimu. Kuchelewa kwa muda unaozidi saa 24 kwaweza kuchangia sana kifo cha mgonjwa. Kugawanya upasuaji mkuu kuwa upasuaji mdogo-mdogo zaidi hupunguza kabisa kuvuja damu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

Tiba Bila Damu—Je, Ni “Kiwango [Kipya] cha Utunzaji?”

AMKENI! lilizungumzia manufaa za tiba na upasuaji bila damu na wataalamu wanne katika uwanja huo.

Mbali na wagonjwa wanaokataa kutiwa damu mishipani kwa sababu za kidini, ni nani wengine ambao huenda wakapendezwa na tiba bila damu?

Dakt. Spahn: Katika kituo chetu wale wanaoomba kutibiwa bila damu kwa kawaida huwa ni wagonjwa wanaojua mambo sana.

Dakt. Shander: Mnamo mwaka wa 1998 idadi ya wagonjwa waliokataa damu kwa sababu za kibinafsi ilizidi idadi ya wagonjwa waliokataa damu kwa sababu za kidini.

Dakt. Boyd: Kwa mfano, kuna wagonjwa walio na kansa. Imeonekana mara nyingi kwamba wasipopokea damu, wanapata nafuu na hawapatwi sana na maradhi yaleyale.

Dakt. Spahn: Mara nyingi tunatibu maprofesa wa chuo kikuu pamoja na familia zao bila kutumia damu. Hata madaktari-wapasuaji hutuomba tuepuke utiaji-damu mishipani! Kwa mfano, daktari-mpasuaji mmoja alitujia kuhusu mke wake, aliyehitaji kupasuliwa. Alisema: “Mhakikishe tu jambo moja—kwamba hammtii damu mishipani!”

Dakt. Shander: Washiriki wa idara yangu ya unusukaputi walisema: ‘Wagonjwa hawa ambao hawatiwi damu wanaendelea vizuri na labda vizuri hata zaidi. Kwa nini tuwe na viwango viwili vya utunzaji? Ikiwa huu ndio utunzaji bora, twapaswa kuutumia kwa kila mtu.’ Kwa hiyo sasa tunatarajia kuwa na tiba bila damu ikiwa ndicho kiwango cha utunzaji.

Bw. Earnshaw: Ni kweli kwamba upasuaji bila damu unahusu hasa Mashahidi wa Yehova. Hata hivyo, hivyo ndivyo tunavyotaka kutibu kila mtu.

Je, tiba bila damu ni ghali zaidi au ni ya gharama nafuu zaidi?

Bw. Earnshaw: Hupunguza gharama.

Dakt. Shander: Tiba bila damu hupunguza gharama kwa asilimia 25.

Dakt. Boyd: Hata ikiwa hiyo ndiyo ingekuwa sababu pekee, twapaswa kuitumia.

Tumepiga hatua kufikia wapi katika kutumia tiba bila damu?

Dakt. Boyd: Nafikiri tumefanya maendeleo makubwa sana. Hatujafikia mwisho bado. Kila mara tunapata sababu mpya iliyo halali ya kutotumia damu.

[Picha]

Dakt. Donat R. Spahn profesa wa unusukaputi,

Zurich, Uswisi

Dakt. Aryeh Shander naibu wa tabibu profesa wa unusukaputi, Marekani

Bw. Peter Earnshaw, FRCS, daktari-mpasuaji na mshauri wa kasoro na magonjwa ya mifupa, London, Uingereza

Dakt. Mark E. Boyd profesa wa uzazi na elimu-uzazi, Kanada

[Sanduku katika ukurasa wa 11]

Daraka la Mgonjwa

▪ Zungumza na daktari wako kuhusu vibadala visivyo vya damu kabla uhitaji wa kutibiwa haujazuka. Hilo ni la maana hasa kwa wanawake wajawazito, wazazi wenye watoto wadogo, na wazee-wazee.

▪ Andika mambo unayotaka ufanyiwe, hasa ikiwa hati ya kisheria inapatikana kwa ajili ya kusudi hilo.

▪ Ikiwa tabibu wako hataki kukutibu bila damu, tafuta tabibu atakayekubaliana na yale unayotaka.

▪ Kwa kuwa vibadala fulani vya damu huhitaji wakati ili viwe na matokeo, usiahirishe kutibiwa ikiwa wajua kwamba unahitaji upasuaji.