Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

 Je, Wajua?

Je, ni kweli kwamba chungu hutayarisha chakula chao wakati wa kiangazi na kukusanya akiba wakati wa mavuno?

Methali 6:6-8 inasema: “Mwendee chungu, ewe mvivu; zitazame njia zake upate kuwa na hekima. Ijapokuwa hana kiongozi, ofisa wala mtawala, yeye hutayarisha chakula chake wakati wa kiangazi; amekusanya akiba ya chakula chake wakati wa mavuno.”

Jamii kadhaa za chungu huhifadhi chakula. Huenda Sulemani alikuwa akirejelea jamii ya chungu mvunaji (Messor semirufus) ambao wanajulikana sana nchini Israel leo.

Kulingana na kitabu kimoja, “chungu wavunaji hutoka katika kichuguu chao wakati wa kiangazi ili kutafuta chakula . . . [nao] hukusanya mbegu wakati wa miezi yenye joto.” Wao hukusanya mbegu kutoka kwenye mimea au wanakusanya zilizoanguka ardhini. Wadudu hao hujenga vichuguu chini ya ardhi karibu na mashamba, maghala, au mahali pa kupuria ambapo nafaka zinaweza kupatikana.

Ndani ya kichuguu chao, chungu huhifadhi chakula katika vyumba vidogo vilivyounganishwa na vijia vingi. Maghala hayo yanaweza kuwa na ukubwa wa kipenyo cha sentimita 12 na kimo cha sentimita 1. Imesemekana kuwa chungu wavunaji walio na chakula cha kutosha wanaweza kuendelea kuishi “kwa zaidi ya miezi 4 bila kutoka nje kutafuta chakula au maji.”

Kazi ya mnyweshaji wa mfalme ilihusisha nini?

Nehemia alikuwa mnyweshaji wa Mfalme Artashasta wa Uajemi. (Nehemia 1:11) Katika makao ya mfalme huko Mashariki ya Kati ya kale, cheo cha mnyweshaji wa mfalme hakikuwa cheo duni. Badala yake, alikuwa ofisa wa cheo cha juu. Vitabu na michongo mingi ya zamani ya wanyweshaji inatusaidia kufikia mikataa fulani kuhusu cheo cha Nehemia katika makao ya mfalme wa Uajemi.

Mnyweshaji angeonja divai ya mfalme ili kumlinda asipewe sumu. Kwa hiyo, mnyweshaji aliaminiwa kabisa na mfalme. “Uhitaji wa kuwa na wanyweshaji waaminifu unaonyeshwa wazi ukifikiria njama zilizokuwa za kawaida katika makao ya kifalme ya Waajemi,” anasema msomi Edwin M. Yamauchi. Mnyweshaji pia alipendwa sana na mfalme na hivyo alikuwa na uvutano mkubwa juu ya mfalme. Kwa kuwa kila siku alifanya kazi kwa ukaribu na mfalme, yeye ndiye aliyeamua ni nani angeingia kumwona mfalme.

Huenda cheo hicho ndicho kilichowezesha ombi la Nehemia la kurudi kujenga upya kuta za Yerusalemu likubaliwe. Lazima mfalme awe alimthamini sana Nehemia. Kamusi moja ya Biblia (The Anchor Bible Dictionary) inasema hivi: “Mfalme alimwuliza swali moja tu, ‘Utarudi wakati gani?’”—Nehemia 2:1-6.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 9]

Mchongo kutoka jumba la mfalme la Waajemi huko Persepoli

[Mchoro]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mnyweshaji

Shasta Mwana-mrithi wa Ufalme

Dario Mkuu

[Hisani]

© The Bridgeman Art Library International