Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maisha Katika Kambi ya Wakimbizi

Maisha Katika Kambi ya Wakimbizi

Maisha Katika Kambi ya Wakimbizi

UNAPOSIKIA usemi “kambi ya wakimbizi,” unawazia nini? Je, umewahi kutembelea mojawapo ya kambi hizo? Zikoje?

Mnamo Aprili mwaka wa 2002 kulikuwa na kambi 13 katika sehemu ya magharibi ya Tanzania. Watu 500,000 ambao wamekimbia vita ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi nyingine za Afrika, walikuwa wakisaidiwa na serikali ya Tanzania pamoja na Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi (UNHCR). Maisha kambini yakoje?

Kuwasili Kambini

Msichana kijana anayeitwa Kandida anaeleza jinsi hali ilivyokuwa wakati yeye na familia yao walipowasili miaka michache iliyopita: “Walitupatia kadi ya posho iliyokuwa na namba ya kitambulisho, na tulipelekwa katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu. Huko tulipewa namba ya kiwanja na ya mtaa wetu. Tulionyeshwa mahali pa kukatia miti na kukusanya nyasi ili kujenga nyumba yetu ndogo. Tulitengeneza matofali ya matope. Kisha tukafunika paa kwa plastiki kubwa tuliyopewa na shirika la UNHCR. Ilikuwa kazi ngumu lakini tulifurahi tulipoweza kuhamia nyumba yetu ndogo.”

Chakula hugawanywa siku ya Jumatano kila baada ya majuma mawili. Kandida anaongeza: “Sisi hupanga foleni ili tupewe vyakula vinavyogawanywa na shirika la UNHCR.”

Mtu mmoja hupewa kiasi gani cha chakula kwa siku moja?

“Kila mmoja wetu hupokea vikombe vitatu vya unga wa mahindi, kikombe kimoja cha njegere, gramu 20 za unga wa maharagwe ya soya, vijiko viwili vikubwa vya mafuta ya kupikia, na gramu 10 za chumvi. Mara kwa mara sisi hupokea kipande cha sabuni kinachotakiwa kudumu mwezi mzima.”

Vipi maji safi? Mwanamke mchanga anayeitwa Riziki anasema hivi: “Maji huvutwa kutoka katika mito iliyo karibu na kupelekwa hadi kwenye matangi makubwa kupitia mifereji mikubwa. Maji hutiwa dawa ya klorini, kisha husukumwa na mashine kupitia bomba hadi sehemu mbalimbali za kuchotea maji katika kila kambi. Hata hivyo, ili kuepuka magonjwa sisi hujitahidi kuchemsha maji kabla ya kuyanywa. Mara nyingi sisi huanza mapema asubuhi na kuendelea hadi jioni kuchota maji na kufua nguo zetu kwenye sehemu za kuchotea maji. Sisi huruhusiwa kuchota ndoo moja na nusu tu ya maji kila siku.”

Ukipitia moja ya kambi hizo utaona kwamba kuna shule za watoto wadogo, shule za msingi na shule za upili. Nyakati nyingine kuna masomo ya watu wazima pia. Ili kudumisha usalama kambini kuna kituo cha polisi na ofisi ya serikali nje tu ya kambi. Utaona pia soko kubwa lenye maduka mengi madogo yanayouza mboga, matunda, samaki, kuku na vyakula vinginevyo. Wenyeji wa eneo huja sokoni kuuza bidhaa zao. Lakini wakimbizi wanapata pesa wapi? Baadhi yao hupanda mboga na kuziuza sokoni. Wengine huuza sehemu ya posho lao la unga au njegere na kununua nyama au matunda kwa pesa wanazopata. Kambi nyingine zinaonekana kama vijiji vikubwa wala si kambi za wakimbizi. Ni jambo la kawaida kuwaona watu sokoni wakicheka na kujifurahisha kama tu walivyofanya walipokuwa katika nchi ya kwao.

Ukiingia hospitalini, daktari atakuambia kwamba wagonjwa wenye magonjwa ya kawaida hutibiwa kwenye kliniki, lakini wagonjwa wa dharura na watu walio wagonjwa sana hupelekwa hospitalini. Wodi ya uzazi, na chumba ambacho akina mama hujifungua ni sehemu muhimu za hospitali hiyo, kwani, kuna watu 48,000 kambini na watoto 250 hivi hutazamiwa kuzaliwa kila mwezi.

Wanalishwa Vizuri Kiroho

Mashahidi wa Yehova kotekote duniani wangependa kujua habari za ndugu zao wa kiroho wanaoishi katika kambi hizo nchini Tanzania. Kuna Mashahidi 1,200 hivi wanaoishi katika kambi hizo, na kuna makutaniko 14 na vikundi 3. Wanaendeleaje?

Wakristo hao wenye bidii walipowasili kambini, mara moja waliomba wapewe kiwanja cha kujengea Jumba la Ufalme. Jambo hilo lingewawezesha wakimbizi wengine kuwapata Mashahidi na kuhudhuria mikutano yao ya kila juma. Katika kambi ya Lugufu, kuna makutaniko 7 yaliyo na Mashahidi wa Yehova 659. Watu 1,700 hivi huhudhuria mikutano ya Jumapili katika makutaniko hayo 7.

Mashahidi katika kambi zote hufaidika pia na makusanyiko makubwa zaidi ya Kikristo. Watu 2,363 walihudhuria kusanyiko la kwanza la wilaya katika kambi ya Lugufu. Mashahidi walichimba kidimbwi cha ubatizo nje tu ya mahali walipokusanyika. Baada ya kuchimba shimo, waliweka plastiki kubwa ndani. Akina ndugu walichota maji katika mto na kuyapeleka kwa baiskeli umbali wa kilometa mbili hivi hadi mahali pa kusanyiko. Waliweza kubeba lita 20 tu safari moja. Kwa hiyo, walihitaji kwenda na kurudi mara nyingi. Wale waliotaka kubatizwa walipanga foleni wakiwa wamevalia nguo zinazofaa. Watu 56 walibatizwa kwa kuzamishwa kabisa majini. Mhudumu mmoja wa wakati wote aliyehojiwa kusanyikoni alieleza kwamba yeye huongoza mafunzo 40 ya Biblia pamoja na watu mbalimbali. Wanne kati ya wanafunzi wake walibatizwa katika kusanyiko hilo.

Ndugu kwenye ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova wamepanga waangalizi wasafirio watembelee makutaniko hayo kwa ukawaida. Mmoja wao anasema hivi: “Ndugu zetu wana bidii katika kazi ya kuhubiri. Kuna watu wengi wa kuhubiria, na katika kutaniko moja kila Shahidi hutumia saa 34 kila mwezi katika kazi ya kuhubiri. Wengi huongoza mafunzo ya Biblia matano au zaidi na watu wanaopendezwa. Painia mmoja [mhubiri wa wakati wote] alisema kwamba hangeweza kuwa na eneo zuri zaidi popote penginepo. Watu wanaoishi kambini wanapenda sana vichapo vyetu.”

Vichapo vya Biblia hupelekwaje hadi kwenye kambi hizo? Ofisi ya tawi huvipeleka kwa gari-moshi hadi Kigoma, mji ulio kwenye ufuo wa mashariki wa Ziwa Tanganyika. Huko ndugu huvipokea na kupanga vipelekwe hadi kwenye makutaniko. Nyakati nyingine wao hukodi lori dogo na wao wenyewe huvisafirisha hadi kambi zote. Safari hiyo inachukua siku tatu au nne kwa sababu barabara ni mbaya sana.

Misaada ya Kimwili

Mashahidi wa Yehova huko Ufaransa, Ubelgiji, na Uswisi wametoa misaada mingi kwa ajili ya wakimbizi katika kambi hizo. Wengine wao wameruhusiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani na shirika la UNHCR kutembelea kambi hizo nchini Tanzania. Mashahidi huko Ulaya wamekusanya kiasi kikubwa sana cha maziwa yaliyotengenezwa kwa maharagwe ya soya, nguo, viatu, vitabu vya shule, na sabuni. Vitu hivyo vimechangwa ili vigawiwe wakimbizi wote kulingana na kanuni hii ya Biblia: “Maadamu tuna wakati wenye kufaa kwa ajili ya hilo, acheni sisi tufanye lililo jema kuelekea wote, lakini hasa kuelekea wale ambao katika imani ni jamaa zetu.”—Wagalatia 6:10.

Misaada hiyo imewafaidi sana wakimbizi wengi. Baraza linaloshughulikia mahitaji ya wakimbizi katika kambi moja lilishukuru kwa kusema hivi: “Kwa niaba ya watu wote kambini, kwa heshima kubwa tunawashukuru kwa misaada ambayo shirika lenu limetoa mara tatu . . . Nguo zimegawiwa watu 12,654 wenye uhitaji—wanaume, wanawake, na watoto . . . Kwa sasa kuna wakazi 37,000 katika kambi ya wakimbizi ya Muyovozi. Watu 12,654 walisaidiwa, yaani, asilimia 34.2 ya wakazi wote kambini.”

Katika kambi moja, watu 12,382 walipewa nguo tatu kila mmoja, na kambi nyingine ilipokea vitabu vya kutumiwa katika shule za upili na za msingi, na katika sehemu za kutunzia watoto. Msimamizi wa ugavi wa UNHCR katika eneo moja alisema: “Tunawashukuru kwa vitu tulivyopokea [vinavyotosheleza] mahitaji makubwa ya watu wanaoishi katika kambi za wakimbizi. Hivi majuzi tulipokea makontena 5 ya vitabu, ambavyo watu wetu wanaohudumia jamii wamewagawia wakimbizi. . . . Asanteni sana.”

Waandishi wa magazeti ya habari ya eneo hilo pia wametaja misaada ambayo ilitolewa. Kichwa kikuu katika gazeti la Sunday News la Mei 20, 2001, kilisema hivi: “Nguo kwa Ajili ya Wakimbizi Nchini Tanzania Zinaletwa.” Katika toleo la Februari 10, 2002, gazeti hilo lilisema: “Wakimbizi wanathamini mchango huo kwa kuwa baadhi ya watoto waliokuwa wameacha kwenda shuleni kwa sababu ya kukosa nguo, sasa wanaenda shuleni kwa ukawaida.”

Wamesongwa Lakini Si Bila Njia ya Kutokea

Kwa kawaida inawachukua wakimbizi mwaka mmoja hivi kuzoea maisha mapya kambini. Wao huishi maisha ya kujinyima. Mashahidi wa Yehova wanaokaa katika kambi hizo hutumia wakati mwingi kuwaeleza majirani wao habari njema zenye kufariji kutoka kwa Neno la Mungu, Biblia. Wao huhubiri kuhusu ulimwengu mpya, ambamo watu wote “watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.” Wakati huo “wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA wa majeshi kimesema hivi.” Bila shaka, kwa baraka ya Mungu hakutakuwa na kambi za wakimbizi duniani wakati huo.—Mika 4:3, 4; Zaburi 46:9.

[Picha katika ukurasa wa 8]

Nyumba katika kambi ya Nduta

[Picha katika ukurasa wa 10]

Jumba la Ufalme huko Lukole (kulia) Ubatizo huko Lugufu (chini)

[Picha katika ukurasa wa 10]

Kusanyiko la Wilaya katika kambi ya Lugufu