Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wahasmonia na Hali Waliyoacha

Wahasmonia na Hali Waliyoacha

 Wahasmonia na Hali Waliyoacha

YESU alipokuwa duniani, Dini ya Wayahudi ilikuwa imegawanyika vikundi vikundi, na vyote vilikuwa vinang’ang’ania kuwa na mamlaka juu ya watu. Hali hiyo ndiyo inayosimuliwa katika Injili na vilevile katika maandishi ya Josephus, mwanahistoria Myahudi wa karne ya kwanza.

Mafarisayo na Masadukayo wanatokea kama watu wenye ushawishi mkubwa, wenye uwezo wa kubadili maoni ya watu hata kufikia hatua ya kumkataa Yesu kuwa Mesiya. (Mathayo 15:1, 2; 16:1; Yohana 11:47, 48; 12:42, 43) Hata hivyo, makundi hayo mawili yenye ushawishi hayatajwi popote katika Maandiko ya Kiebrania.

Josephus anawataja Masadukayo na Mafarisayo mara ya kwanza katika karne ya pili K.W.K. Wakati huo Wayahudi wengi walikuwa wanavutiwa na utamaduni na falsafa ya Wagiriki. Uvutano kati ya Utamaduni wa Wagiriki na Dini ya Wayahudi ulifikia kilele wakati watawala wa nasaba ya Seleuko walipochafua hekalu huko Yerusalemu kwa kuliweka wakfu kwa Zeusi. Judah Maccabee (Yuda Makabayo), kiongozi Myahudi mwenye nguvu, wa familia ya Wahasmonia, aliongoza jeshi la waasi lililokomboa hekalu hilo kutoka kwa Wagiriki. *

Miaka kadhaa baada tu ya uasi na ushindi wa Wamakabayo kulikuwa na mwelekeo wa kuanzisha madhehebu kwa kutegemea itikadi zilizotofautiana. Kila madhehebu iling’ang’ania kupata wafuasi wengi zaidi miongoni mwa Wayahudi. Lakini kwa nini kulikuwa na mwelekeo huo? Kwa nini Dini ya Wayahudi iligawanyika hivyo? Ili kujibu maswali hayo, acheni tuchunguze historia ya Wahasmonia.

Uhuru na Migawanyiko Zaidi

Baada ya kutimiza mradi wake wa kidini wa kurudisha ibada ya kweli kwenye hekalu la Yehova, Judah Maccabee aligeuka kuwa mwanasiasa. Hivyo, Wayahudi wengi wakaacha kumfuata. Hata hivyo, aliendelea na mapambano yake na watawala wa nasaba ya Seleuko, akafanya mkataba na Roma, na kujaribu kuanzisha Taifa huru la Wayahudi. Baada ya Judah kufa vitani, ndugu zake Jonathan na Simon waliendelea na mapambano hayo. Mwanzoni watawala wa nasaba ya Seleuko waliwapinga Wamakabayo vikali. Lakini baada ya muda, watawala hao wakakubali kuridhiana mambo fulani ya kisiasa na kuruhusu ndugu hao Wahasmonia wawe na uhuru wa kiasi fulani.

Japo Wahasmonia walikuwa wa ukoo wa kikuhani, hakuna Mhasmonia yeyote aliyepata kutumikia akiwa kuhani wa cheo cha juu. Wayahudi wengi walionelea kwamba cheo hicho kingepasa kuchukuliwa na makuhani wa ukoo wa Zadoki, ambaye Solomoni alikuwa amemweka rasmi kuwa kuhani wa cheo cha juu. (1 Wafalme 2:35; Ezekieli 43:19) Jonathan alitumia  vita na busara ili kuwashawishi watawala wa nasaba ya Seleuko wamweke rasmi kuwa kuhani wa cheo cha juu. Lakini baada ya Jonathan kufa, ndugu yake Simon, alitimiza mengi hata zaidi. Mnamo Septemba 140 K.W.K., agizo muhimu lilitolewa huko Yerusalemu, na kuandikwa kwenye mabamba ya shaba kwa Kigiriki: “Mfalme Demetrio [mtawala Mgiriki wa nasaba ya Seleuko] alimwidhinisha [Simon] kuwa kuhani wa cheo cha juu, akamfanya mmoja wa Rafiki zake, na kumtunukia heshima kubwa. . . . Wayahudi na makuhani wao wameazimia kwamba Simon apasa kuwa kiongozi wao na kuhani wao wa cheo cha juu milele, hadi nabii mwenye kutumainika atokee.”—1 Wamakabayo 14:38-41 (kitabu cha kihistoria kilichopatikana miongoni mwa vitabu vya Biblia visivyothibitishwa).

Cheo cha Simon akiwa mtawala na pia kuhani wa cheo cha juu—kwa ajili yake na wazao wake—kiliidhinishwa na mamlaka ya kigeni ya ukoo wa Seleuko na pia “Kusanyiko Kubwa” la watu wake mwenyewe. Huo ulikuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa. Kama mwanahistoria Emil Schürer alivyoandika, mara tu nasaba ya kisiasa ilipoanzishwa na Wahasmonia, “hangaiko lao kubwa lilikuwa kuhifadhi na kupanua uwezo wao wa kisiasa wala si kutimiza Torati [Sheria ya Kiyahudi].” Hata hivyo, Simon alikuwa mwangalifu asiwaudhi Wayahudi hivyo akajiita “ethnarch,” yaani, “kiongozi wa watu,” badala ya kujiita “mfalme.”

Si watu wote waliopendezwa na jinsi Wahasmonia walivyonyakua mamlaka ya kidini na kisiasa. Kulingana na wasomi wengi, wakati huo ndipo jumuiya ya watu waitwao Qumran ilipoanzishwa. Kuhani wa ukoo wa Zadoki, anayeaminika kuwa ndiye anayeitwa “Mwalimu wa Uadilifu” katika maandishi ya Qumran, aliondoka Yerusalemu na kuongoza kikundi cha wapinzani kwenye Jangwa la Yudea kando ya Bahari ya Chumvi. Mojawapo ya Hati Kunjo za Bahari ya Chumvi, ambayo inafafanua kitabu cha Habakuki, yashutumu “Kuhani Mwovu aliyetumainiwa mwanzoni, lakini akawa mwenye kiburi alipotawala Israeli.” Wasomi wengi wanaamini kwamba madhehebu hiyo ilikuwa inazungumzia Jonathan au Simon ilipotaja “Kuhani Mwovu” mwenye kutawala.

Simon aliendelea na vita vyake vya kupanua eneo alilotawala. Hata hivyo, utawala wake ulikoma ghafula wakati mkwe wake wa kiume, Ptolemy, alipomwua pamoja na wanaye wawili walipokuwa wakifurahia karamu karibu na Yeriko. Jaribio hilo la kutaka kutawala halikufua dafu. John Hyrcanus, mwana aliyesalia wa Simon alionywa juu ya jaribio la kumwua. Aliwakamata watu ambao wangemwua na kuchukua uongozi na ukuhani mkuu, vyeo vilivyokuwa vya babake.

Upanuzi Zaidi na Ukandamizaji

Mwanzoni, John Hyrcanus alikabili vitisho vikali kutoka kwa majeshi ya Siria, lakini katika mwaka wa 129 K.W.K., ufalme wa nasaba ya Seleuko ukashindwa kwenye vita muhimu walivyopigana na Waparthia. Kuhusiana na matokeo ya vita hivyo vya Waparthia na ufalme wa nasaba ya Seleuko, msomi mmoja Myahudi Menahem Stern aliandika: “Mpangilio wote wa ufalme uliporomoka.” Hivyo Hyrcanus “akaweza kuliweka huru kisiasa eneo lote la Yudea na kuanza kulipanua kuelekea pande mbalimbali.” Na alilipanua kwelikweli.

Sasa kukiwa hakuna tisho lolote lenye kumzuia kutoka Siria, Hyrcanus alianza kuvamia maeneo yaliyokuwa nje ya Yudea, na kuyatawala. Walilazimisha wakazi wa maeneo hayo kugeuza imani yao na kufuata Dini ya Wayahudi la sivyo majiji yao yangeharibiwa kabisa. Walifanya hivyo na Waedomu. Kuhusu jambo hilo Stern alisema: “Kugeuzwa imani kwa Waedomu kulikuwa kwa pekee, kwa kuwa si watu wachache tu waliogeuzwa imani bali jamii nzima.” Mojawapo ya maeneo yaliyovamiwa ni Samaria, ambako Hyrcanus aliharibu kabisa hekalu la Samaria kwenye Mlima Gerizimu. Akionyesha jambo lililo kinyume cha sera hiyo ya wafalme wa nasaba ya Wahasmonia ya kuwalazimisha watu kubadili imani yao, mwanahistoria Solomon Grayzel aliandika hivi: “Mjukuu wa Mattathias [baba ya Judah Maccabee] alikuwa anavunja kanuni, yaani, uhuru wa ibada ambao kizazi kilichopita kilikuwa kimeuhifadhi vizuri.”

Mafarisayo na Masadukayo Watokea

Anapoandika juu ya utawala wa Hyrcanus, ndipo Josephus kwanza anaandika juu ya uvutano  unaozidi wa Mafarisayo na Masadukayo. (Josephus alikuwa ametaja Mafarisayo walioishi wakati wa utawala wa Jonathan.) Yeye hataji kama walikuwa na chanzo kimoja. Wasomi wengi wanaonelea kwamba walikuwa kikundi kilichotokana na Wasidim, madhehebu yenye kujitoa kwa Mungu iliyomwunga mkono Judah Maccabee katika kutimiza malengo yake ya kidini lakini wakamwacha wakati alipoanza kutamani mambo ya kisiasa.

Kwa kawaida jina Mafarisayo linahusianishwa na neno la Kiebrania linalomaanisha “waliojitenga,” japo wengine huona kuwa linahusiana na neno “wafasiri.” Mafarisayo walikuwa wasomi walioishi miongoni mwa watu wa kawaida wasiokuwa na ukoo maalum. Walijitenga wasichafuliwe kidini, hivyo wakafuata falsafa ya utakatifu wa pekee na kutumia sheria za hekalu, ambazo zinahusiana na utakatifu wa kikuhani, katika hali za kawaida za maisha yao ya kila siku. Mafarisayo walitokeza njia mpya ya kufasiri Maandiko na dhana ambayo baadaye iliitwa sheria ya mdomo. Wakati wa utawala wa Simon walipata kuwa na uvutano mkubwa zaidi wakati baadhi yao walipoteuliwa kuwa washiriki wa Gerousia (baraza la wanaume wazee), ambalo baadaye liliitwa Sanhedrini.

Josephus asimulia kwamba mwanzoni John Hyrcanus alikuwa mwanafunzi wa Mafarisayo na aliwaunga mkono. Hata hivyo, baadaye Mafarisayo walimkemea kwa kutoacha ukuhani wa cheo cha juu, jambo lililofanya afarakane nao kabisa. Hyrcanus alipiga marufuku sheria za kidini za Mafarisayo. Ili kuwaadhibu zaidi Mafarisayo, aliwaunga mkono Masadukayo waliokuwa wapinzani wao wa kidini.

Yaelekea jina Masadukayo linahusiana na Zadoki, Kuhani wa Cheo cha Juu, ambaye wazao wake waliendelea kuwa makuhani tangu wakati wa Solomoni. Hata hivyo, si Masadukayo wote waliotokana na uzao huo. Josephus asema kwamba Masadukayo walikuwa matajiri, watu wa tabaka ya juu katika taifa, lakini hawakuungwa mkono na umma. Profesa Schiffman aeleza hivi: “Yaonekana wengi wao . . . walikuwa makuhani au watu waliooana na familia za makuhani wa cheo cha juu.” Hivyo, kwa muda mrefu walikuwa na uhusiano na wale waliokuwa mamlakani. Kwa hiyo, yale ambayo Mafarisayo walitimiza miongoni mwa watu na pia dhana yao ya kueneza utakatifu wa kidini kwa watu wote, ilionekana kuwa tisho ambalo lingedhoofisha mamlaka ya iasili ya Masadukayo. Sasa, katika miaka ya mwishomwisho ya utawala wa Hyrcanus, Masadukayo walipata mamlaka tena.

Siasa Zazidi, Utakatifu Wapungua

Aristobulus, mwana wa kwanza wa Hyrcanus, alikufa baada ya kutawala kwa mwaka mmoja. Aliendelea na ile sera ya kulazimisha watu kubadili imani yao, akawalazimisha Waiturea wafanye hivyo na sehemu ya juu ya Galilaya ikawa chini ya utawala wa Wahasmonia. Lakini wakati wa utawala wa ndugu yake Alexander Jannaeus, aliyetawala kuanzia 103-76 K.W.K., nasaba ya wafalme Wahasmonia ilifikia upeo wa utawala wake.

Alexander Jannaeus alikataa sera ya hapo awali na kujitangaza waziwazi kuwa mfalme na kuhani wa cheo cha juu.  Mapambano kati ya Wahasmonia na Mafarisayo yakaongezeka, na hata kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo Wayahudi 50,000 walikufa. Baada ya uasi huo kukomeshwa, Jannaeus alitenda kama wafalme wapagani kwa kuwatundika mtini waasi 800. Walipokuwa wanakaribia kufa, wake zao na watoto wao waliuawa mbele yao, huku Jannaeus akifurahia karamu hadharani pamoja na masuria wake. *

Licha ya kuwachukia Mafarisayo, Jannaeus alikuwa mwanasiasa mwenye busara. Aliona kwamba Mafarisayo walizidi kuungwa mkono na watu wengi. Alipokuwa anakaribia kufa alimwagiza mke wake, Salome Alexandra, awahusishe Mafarisayo katika utawala. Jannaeus alichagua mke wake badala ya wanaye kuwa mrithi wa ufalme wake. Mke huyo alidhihirisha kwamba alikuwa mtawala mwenye uwezo na utawala wake ndio uliokuwa wenye amani zaidi kati ya tawala za Wahasmonia (76-67 K.W.K.). Mafarisayo walirudishwa kwenye vyeo vya mamlaka, na sheria zilizopinga sheria zao za kidini zikaondolewa.

Salome alipokufa, wanaye Hyrcanus wa Pili, aliyetumikia akiwa kuhani wa cheo cha juu, na Aristobulus wa Pili, wakaanza kung’ang’ania mamlaka. Wote wawili walikosa ufahamu wa kisiasa na wa kijeshi wa babu zao, na inaonekana kwamba hawakuelewa vizuri kwa nini Waroma waliendelea kuongezeka katika eneo hilo baada ya ufalme wa nasaba ya Seleuko kuanguka kabisa. Katika mwaka wa 63 K.W.K., ndugu hao wawili walimwendea Pompey, mtawala wa Roma, alipokuwa Damasko na kumwomba awasaidie kupatana. Mwaka huohuo, Pompey na majeshi yake walivamia Yerusalemu na kuliteka. Huo ndio uliokuwa mwisho wa ufalme wa Wahasmonia. Katika mwaka wa 37 K.W.K., Yerusalemu lilitekwa na Mfalme Herode Mkuu aliyekuwa Mwedomu, ambaye Baraza la Roma lilimwidhinisha kuwa “Mfalme wa Yudea,” “mshirika na rafiki wa Waroma.” Ufalme wa Wahasmonia ukatokomea.

Hali Iliyoachwa na Wahasmonia

Kipindi cha Wahasmonia, kuanzia Judah Maccabee hadi Aristobulus wa Pili, kilisababisha migawanyiko ya kidini iliyokuwako wakati Yesu alipokuwa duniani. Mwanzoni Wahasmonia walikuwa na bidii kwa ajili ya ibada ya Mungu, lakini wakaacha bidii hiyo na kuzingatia mambo ya ubinafsi. Makasisi wao ambao walikuwa na fursa ya kuunganisha watu ili kufuata Sheria ya Mungu, walisababisha mapambano ya kisiasa miongoni mwa watu wa taifa hilo. Katika hali hiyo, maoni tofauti ya kidini yalienea. Wahasmonia walikuwa wametoweka, lakini mapambano ya kupata mamlaka ya kidini kati ya Masadukayo, Mafarisayo, na wengineo yakaendelea katika taifa hilo lililokuwa chini ya Herode na Roma.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Soma makala “Wamakabayo Walikuwa Akina Nani?” katika gazeti Mnara wa Mlinzi la Novemba 15, 1998.

^ fu. 22 “Ufafanuzi Juu ya Kitabu cha Nahumu” (“Commentary on Nahum”) wa Hati Kunjo ya Bahari ya Chumvi unataja “Simba Mwenye Ghadhabu” ambaye “alinyonga watu,” semi ambazo huenda zarejezea tukio lililotajwa hapo juu.

[Chati katika ukurasa wa 30]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Nasaba ya Wafalme Wahasmonia

Judah Maccabee

Jonathan Maccabee

Simon Maccabee

John Hyrcanus

↓ ↓

Aristobulus

Salome Alexandra — aliyekuwa ameolewa — Alexander Jannaeus

↓ ↓

Hyrcanus wa pili

Aristobulus wa pili

[Picha katika ukurasa wa 27]

Judah Maccabee alitaka Wayahudi wawe huru

[Hisani]

The Doré Bible Illustrations/Dover Publications, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 29]

Wahasmonia wakipigania kudhibiti majiji zaidi yasiyo ya Wayahudi

[Hisani]

The Doré Bible Illustrations/Dover Publications, Inc.