Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maisha ya Wachungaji wa Wales

Maisha ya Wachungaji wa Wales

Maisha ya Wachungaji wa Wales

WACHUNGAJI ulimwenguni pote hutunza zaidi ya kondoo bilioni moja. Kila majira huwa na magumu ya pekee. Gerwyn, Ioan, na Rhian wanaeleza kuhusu kazi ya mchungaji katika milima ya Wales, ambako idadi ya kondoo ni mara tatu zaidi ya ile ya wanadamu.

Wana-Kondoo wa Majira ya Kuchipua

Majira ya kuchipua yanapowasili, wachungaji hufanya kazi mchana na usiku ili kuwasaidia kondoo wa kike wanapozaa.

Gerwyn: “Ingawa kipindi cha mwaka wakati kondoo wanapozaliwa ndicho kipindi kigumu zaidi, hicho ndicho kipindi chenye kuridhisha zaidi, na mbwa aliyezoezwa vizuri husaidia sana. Ikiwa kondoo-jike ana matatizo wakati wa kuzaa, mbwa wangu humkamata bila kumwumiza na kumshikilia chini ili niweze kumsaidia anapojifungua.”

Ioan: “Hata niwe nimewasaidia kondoo-jike wangapi kuzaa, kila mara huwa ni jambo la pekee kuwaona wana-kondoo wakizaliwa!”

Kuwanyoa Wakati wa Majira ya Kiangazi

Kazi ya mchungaji wakati wa majira ya kiangazi huwa ni kuwanyoa kondoo manyoya, ambayo yanaweza kuwa na uzito wa kilo 10, ikitegemea aina ya kondoo. Mchungaji anaweza kunyoa hadi kondoo 250 kwa siku.

Rhian: “Ili kumtayarisha kondoo anyolewe, kwanza mimi huondoa manyoya machafu kuzunguka mkia. Wakitumia makasi ya umeme, wanyoaji stadi wanaweza kunyoa manyoya yote kwa dakika mbili tu. Mimi husaidia kusafisha manyoya hayo, na baadaye kuyakunja na kuyatia kwenye magunia tayari kuuzwa.”

Kwenye nyanda za chini, wachungaji hutumaini kwamba kutakuwa na kipindi cha majuma mawili kisichokuwa na mvua ambapo watakata nyasi na kuzikausha. Chakula hicho hutumika kuwalisha kondoo wakati wa majira ya baridi kali. Watu wa familia na marafiki pia husaidia kubeba nyasi hizo.

Ioan: “Mimi hufurahi sana kutembea shambani asubuhi baada ya nyasi zote kukatwa na kuhifadhiwa.”

Kuwakusanya Katika Majira ya Kupukutika

Ili wachungaji waweze kutenganisha kondoo wa kike na wana-kondoo wao walioachishwa kunyonya, kondoo wote hukusanywa na kupelekwa kwenye nyanda za juu.

Ioan: “Hata iwe hakuna ua wala ukuta wa mawe kwenye milima fulani, ni vigumu kwa kondoo kupotea au kuingia kwenye mashamba jirani. Kwenye shamba letu, kondoo-jike hujua mipaka. Kwa kuwa alijifunza kuhusu mipaka hiyo kutoka kwa mama yake au kutoka kwa mchungaji, kondoo-jike huyo huwafundisha kondoo wengine wa kike mambo hayo. Hata hivyo, nyakati nyingine sisi huwatafuta kwa saa nyingi, au hata siku nyingi, kondoo wachache waliopotea.”

Wachungaji pia hukagua, hununua, na kuwatayarisha kondoo-dume kwa ajili ya kondoo-jike. Kondoo-dume anahitajika kwa kondoo-jike 25 hadi 50. Kuwepo kwa kondoo dume huhakikisha kwamba wakati ujao kutakuwa na uzao mpya katika kundi.

Kati ya majuma 10 hadi 12 baada ya kondoo-dume kujamiiana na kondoo-jike, mchungaji hutumia kifaa kinachotumia mawimbi ya sauti ili kujua ni kondoo gani ambao wameshika mimba na watazaa wana-kondoo wangapi katika majira ya kuchipua. Kondoo-jike tasa huuzwa. Wale wanaotarajia kuzaa mwana-kondoo mmoja huwekwa pamoja, na wale wanaotarajia kuzaa mapacha, au wana-kondoo watatu hutunzwa kwa njia ya pekee na kupewa chakula cha ziada.

Kuwalisha Katika Majira ya Baridi Kali

Wakati wa majira ya baridi kali mchungaji hutumia muda mwingi kuwalisha kondoo-jike wenye mimba wakati wa saa chache zenye mwangaza. Hata hali ya hewa iwe mbaya kadiri gani, mchungaji huwa karibu na kondoo wakati wote, akihakikisha kwamba wana chakula cha kutosha theluji inapofunika malisho.

Gerwyn: “Katika majira hayo, kondoo wanamhitaji sana mchungaji nao humtegemea awape chakula na ulinzi.”

Rhian: “Inafurahisha sana kuwatunza kondoo wakati wa majira yote ya mwaka na kuona mabadiliko yanayotokea kwa wanyama na hata mimea—jambo linaloridhisha sana ninapoendelea kufanya kazi niipendayo ya kuwatunza kondoo wangu.”

[Ramani katika ukurasa wa 12]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

IRELAND KASKAZINI

IRELAND

SCOTLAND

WALES

UINGEREZA

[Picha katika ukurasa wa 14]

Ioan akimkagua kondoo-dume

[Picha katika ukurasa wa 14]

Gerwyn akiwa na mbwa mwenye uzoefu wa kuchunga kondoo