Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ganda la Mti Linalofanyiza Kifuniko cha Chupa

Ganda la Mti Linalofanyiza Kifuniko cha Chupa

Ganda la Mti Linalofanyiza Kifuniko cha Chupa

Je, unaweza kuwazia ganda la mti linalotumiwa katika kutengeneza injini, mipira ya kriketi, mipira ya besiboli, na vizibo vya chupa za shampeni —ganda ambalo lilitumiwa maelfu ya miaka iliyopita na wavuvi na wanawake matajiri na ambalo limetumiwa pia katika anga za juu? Jambo la kushangaza hata zaidi ni kwamba ganda hilo la pekee linaweza kutumiwa katika njia hizo zote bila mti kukatwa!

KIZIBO au kifuniko kinachotumiwa hasa kufunika chupa za mvinyo kimetolewa kwenye aina fulani ya mti wa mwaloni. Lakini ganda lake si la kawaida. Ni jepesi, halishiki moto, na linaweza kutanuka.

Kila mwaka, mti huo wa mwaloni huongeza sana ukubwa wa ganda lake. Iwapo ganda lake halitavunwa, linaweza kukua kufikia unene wa sentimita 25—nalo husaidia mti huo usipigwe na jua, baridi, wala na moto wa msitu. Ganda lake linapovunwa, mti huo wa mwaloni utakuza ganda lingine katika muda wa miaka kumi hivi.

Nchi ya Ureno hutokeza asilimia 55 hivi ya vifuniko vyote ulimwenguni vinavyotumiwa katika chupa za mvinyo, Hispania inatokeza asilimia 30 hivi, na nchi nyingine (kutia ndani Algeria, Italia, Morocco, Tunisia, na Ufaransa) hutokeza asilimia 15 inayosalia. *

Matumizi Mengi

Waroma na Wagiriki waligundua kwamba ganda la mti huo lilifaa katika kutengeneza vifaa vya kuelea vinavyotumiwa katika nyavu na pia kutengeneza sehemu ya chini ya sapatu. Inaonekana kwamba pia walitengeneza vifuniko vya mitungi kutokana na ganda hilo. Kwa kuwa ganda hilo halibadili umbo lake hata linapopigwa na joto kali, linafaa sana kutengeneza gasketi za injini. Pia ni sehemu muhimu sana ya vifaa vinavyotumiwa katika vyombo fulani vya kusafiri kwenye anga za juu.

Kwa kuwa watu wengi hupendezwa na sura na uwezo wake wa kuhifadhi joto, vigae vilivyotengenezwa kutokana na ganda la mti huo vimetumiwa sana kurembesha kuta na sakafu. Watengenezaji wa vifaa vya michezo huona kwamba ganda hilo ni muhimu kwa ajili ya kutengeneza sehemu ya ndani ya mpira wa besiboli au kishikio cha ufito wa kuvulia. Bila shaka, ganda hilo linajulikana hasa kwa kufunika chupa za divai na shampeni.—Ona sanduku “Kifuniko Bora.”

Haiharibu Mazingira

Msitu mzuri wa aina hii ya mialoni unaonyesha wazi kwamba mwanadamu anaweza kuishi kwa upatano na mazingira—akifaidika kutokana na mazao yake bila kuharibu utajiri wake. Mialoni hiyo ya kale hurembesha maeneo ya vijijini, huandaa kivuli na chakula kwa ajili ya mifugo inayolisha chini yake, na kupunguza ukali wa majira ya kiangazi.

Ndege kadhaa ambao wanakabili hatari ya kutoweka—kutia ndani tai anayeitwa imperial, tumbusi mweusi, na korongo mweusi—hupendelea hasa kujenga viota vyao juu ya mialoni mikubwa. Pia, simba-mangu wa Iberia ambaye anakabili hatari ya kutoweka anaishi katika misitu hiyo ya mialoni. Hivi karibuni, Hazina ya Wanyama wa Pori Ulimwenguni ilisema kwamba kuokoka kwa mnyama huyo kunategemea biashara ya ganda hilo la mwaloni nchini Hispania na Ureno.

Kwa hiyo, wakati ujao unapotoa kizibo au kifuniko cha chupa ya divai kilichotengenezwa kwa ganda hilo, tua na ukithamini. Mkononi mwako umeshika kitu cha kiasili, kisichoharibu mazingira, kilichotokana na ganda linaloweza kukua tena. Na matumizi yake yanasaidia kulinda mazingira yetu. Mti huo unafaa kabisa kwa matumizi ya mwanadamu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Aina hii ya mti wa mwaloni unapatikana katika sehemu nyingine za ulimwengu, lakini eneo la Mediterania ndilo hutokeza vifuniko au vizibo vyake kwa ajili ya biashara, kwa kuwa mti huo hukua kwa njia ya asili katika eneo hilo.

[Sanduku/​Picha katika ukurasa wa 20]

“Kifuniko Bora”

Miguel Elena, msimamizi wa Taasisi ya Ganda la Mwaloni, Mbao na Makaa, huko Extremadura, Hispania, anaeleza mengi zaidi kuhusu kutumia ganda hilo kama kifuniko.

Linafaa kadiri gani kuwa kifuniko?

Nimeona chupa fulani zikifunuliwa baada ya miaka zaidi ya mia moja, na divai iliyomo ilikuwa imehifadhiwa vizuri sana! Ganda hilo ni kifuniko bora.

Mwaloni unapaswa kuwa na umri gani kabla ya ganda lake kuvunwa ili kutengeneza vifuniko?

Ili kutokeza kifuniko cha hali ya juu, mwaloni unapaswa kuwa na umri wa miaka 50 hivi, ingawa ganda lake linaweza kuvunwa kwa mara ya kwanza miaka 25 baada ya mbegu yake kupandwa. Bila shaka, ni watu wachache sana walio tayari kupanda mmea ambao utawaletea pesa baada ya miaka 50. Kwa kweli, siwezi hata kufikiria kuhusu biashara inayoweza kusubiri muda mrefu kadiri hiyo kabla ya kujipatia faida.

Mwaloni huo unaweza kuishi kwa miaka mingapi?

Mwaloni unaweza kuishi miaka 200 hivi, na aina fulani zinaweza kuishi kwa miaka mingi zaidi. Mwaloni huvunwa baada ya kila miaka tisa.

Ni mambo gani yanayofanywa ili kudumisha kutokezwa kwa ganda hilo?

Muungano wa Ulaya na serikali ya eneo letu hutenga pesa fulani ili kuwatia watu moyo kupanda mialoni. Kwa hiyo, katika miaka ya karibuni tumepanda misitu mipya ya mialoni katika mashamba ya ekari nyingi na tumejitahidi kudumisha misitu iliyopo.

Ni maendeleo gani ya karibuni ambayo yamefanywa katika kutokeza vifuniko bora?

Katika miaka 20 ambayo imepita, tumefanya utafiti mwingi ili kutambua mbegu za mwaloni zinazofaa zaidi. Na tunafanya kazi kwa ukaribu pamoja na nchi nyingine zinazotokeza vifuniko hivyo ili kuboresha kazi hiyo. Tuliwafundisha watu kutumia msumeno fulani mdogo unaowawezesha watu wavune ganda la mti huo kwa ustadi zaidi, kwani kwa karne nyingi kazi ya kuvuna imefanywa kwa kutumia shoka.

[Picha katika ukurasa wa 19]

Kila mara ganda linapovunwa, linakua tena

[Picha katika ukurasa wa 19]

Wafanyakazi stadi wanavuna ganda kwa uangalifu

[Picha katika ukurasa wa 19]

Maganda yaliyovunwa, yakisubiri hatua inayofuata

[Picha katika ukurasa wa 19]

Vizibo vya hali ya juu bado vinatengenezwa kwa mikono

[Picha katika ukurasa wa 18, 19]

Mabaki ya maganda hukusanywa na kutengeneza vifuniko na vifaa vingine