Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Njia ya 1—Kula Vizuri

Njia ya 1—Kula Vizuri

Njia ya 1—Kula Vizuri

“Kula chakula. Usile kingi. Kula hasa mboga.” Kwa maneno hayo machache, mwandishi Michael Pollan anaeleza kwa ufupi mazoea ya kula yanayofaa ambayo yametumiwa kwa muda mrefu. Anamaanisha nini?

◯ Kula vyakula ambavyo havijatengenezwa viwandani. Kula vyakula “halisi”—vyakula vinavyotolewa moja kwa moja kutoka shambani ambavyo watu wamekuwa wakila kwa miaka mingi—badala ya vyakula vya kisasa vilivyotengenezwa viwandani. Kwa kawaida, vyakula vilivyotengenezwa viwandani na vyakula vyepesi vya mikahawa vina sukari, chumvi, na mafuta mengi, na inadhaniwa kwamba vitu hivyo husababisha magonjwa ya moyo, kiharusi, kansa, na magonjwa mengine hatari. Unapopika, jaribu kuchemsha, kuoka, na kuchoma badala ya kukaanga chakula. Jaribu kutumia vikolezo na viungo ili usitumie chumvi nyingi. Hakikisha kwamba nyama imeiva vizuri, na usile kamwe chakula kilichoharibika.

◯ Usile chakula kingi. Shirika la Afya Ulimwenguni linaripoti ongezeko la watu wanene kupita kiasi, tatizo ambalo mara nyingi husababishwa na kula kupita kiasi. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba katika sehemu fulani za Afrika, “idadi ya watoto walionenepa kupita kiasi ni kubwa kuliko ya wale walio na utapiamlo.” Watoto walionenepa kupita kiasi wamo katika hatari ya kupatwa na matatizo ya afya sasa na wakati ujao, kutia ndani kisukari. Wazazi, wawekeeni watoto wenu mfano mzuri kwa kula kwa kiasi.

◯ Kula hasa mboga. Chakula chenye lishe kinatia ndani matunda mbalimbali, mboga, na nafaka isiyokobolewa maganda badala ya nyama na vyakula vyenye wanga. Mara moja au mbili kwa juma, jaribu kula samaki badala ya nyama. Punguza vyakula vilivyotolewa virutubisho kama vile tambi, mkate mweupe, na mchele mweupe. Lakini epuka mazoea hatari ya kula yanayofuatwa na watu ili kupunguza uzito. Wazazi, lindeni afya ya watoto wenu kwa kuwasaidia wawe na mazoea ya kula vyakula vyenye lishe. Kwa mfano, wapeni kokwa na matunda na mboga zilizosafishwa vizuri badala ya viazi vilivyokaangwa au peremende.

◯ Kunywa vinywaji vingi. Watu wazima na watoto wanapaswa kunywa maji mengi na vinywaji vingine visivyo na sukari kila siku. Kunywa vinywaji vingi hasa wakati kuna joto jingi na unapofanya kazi ngumu na mazoezi. Vinywaji hivyo husaidia kumeng’enya chakula, kuondoa sumu mwilini, kufanya ngozi iwe laini, na kupunguza uzito. Vinakusaidia kuhisi na kuonekana mwenye afya. Epuka kunywa kileo kupita kiasi na vinywaji vingi vyenye sukari. Soda moja kwa siku inaweza kumfanya mtu aongeze kilo 6.8 kwa mwaka.

Katika nchi fulani, jitihada kubwa sana inahitajika ili kupata maji safi na ni bei ghali sana. Hata hivyo, ni muhimu kunywa maji. Yanahitaji kuchemshwa au kutiwa dawa. Inasemekana kwamba watu wengi zaidi hufa kwa kunywa maji yaliyo na viini kuliko wale wanaokufa kutokana na vita au matetemeko ya nchi; inaripotiwa kwamba kila siku, watoto 4,000 hufa kutokana na maji machafu. Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza kwamba watoto wachanga wanyonye maziwa ya mama peke yake kwa miezi sita ya kwanza, kisha wanyonye maziwa ya mama pamoja na vyakula vingine hadi watakapofikia umri wa miaka miwili hivi.