Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuishi Karibu na Jitu Linalolala

Kuishi Karibu na Jitu Linalolala

Kuishi Karibu na Jitu Linalolala

Tangu zamani watu wametatanishwa sana na milima ya volkano. Inaweza kulala kwa karne nyingi halafu ghafula iamke kwa njia ya ajabu na yenye kutokeza madhara. Kwa dakika chache tu mlipuko wa volkano unaweza kuharibu miji na kuwaua watu.

HAKUNA anayetilia shaka kwamba milima ya volkano ni hatari. Katika karne tatu zilizopita, mamia ya maelfu ya watu wameuawa kutokana na milipuko ya volkano. Ni kweli kwamba wengi wetu huishi mbali na majitu hayo yanayolala, lakini mamilioni ya watu duniani huishi karibu na volkano zilizo hai. Kwa mfano, Quito, mji mkuu wa Ekuado uko karibu na Pichincha, mlima wa volkano ulio kaskazini-magharibi ya jiji hilo. Mlima Popocatepetl, jina ambalo katika lugha ya Waazteki linamaanisha “Mlima Unaotoa Moshi,” uko umbali wa kilomita 60 kutoka Mexico City. Majiji makubwa ya Auckland, New Zealand, na Naples, Italia, yako juu au chini ya milima ya volkano. Vyovyote vile, mamilioni ya watu huishi wakiwa na hofu kwamba siku moja utendaji wa nguvu zilizo chini ya ardhi utasababisha jitu linalolala kuamka kwa mlipuko mkubwa.

Jitu Hatari

Wakazi wa Naples wamekuwa wakiishi karibu na Mlima Vesuvius kwa miaka 3,000 hivi. Mlima huo uko umbali wa kilomita 11 kutoka Naples. Kwa kweli, Vesuvius ni kilima kilicho kwenye mojawapo ya mashimo ya mlima wa kale uitwao Monte Somma. Vesuvius ni mojawapo ya volkano hatari zaidi duniani. Kwa kuwa sehemu ya chini ya mlima huo iko chini ya usawa wa bahari, mlima huo ni mkubwa kuliko unavyoonekana.

Mlima Vesuvius umelipuka mara nyingi sana. Umelipuka zaidi ya mara 50 tangu mwaka wa 79 W.K., ulipoharibu majiji ya Pompeii na Herculaneum. Karibu watu 4,000 waliuawa ulipolipuka mnamo 1631. Kuanzia wakati huo neno “lava” lilianza kutumiwa. Limetokana na neno la Kilatini labi, linalomaanisha “kuteleza.” Neno hilo linafafanua kwa kufaa jinsi lava inavyotiririka kwenye miteremko ya Mlima Vesuvius.

Kwa karne zote Vesuvius umeendelea kuwa hai. Ulilipuka mnamo 1944 wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, na kuyakaribisha majeshi ya Muungano kwa kuyamwagia majivu. Miji ya karibu ya Massa na San Sebastiano ilifunikwa kwa majivu. Pia majivu hayo yalifunika lifti ambayo hutumiwa kupanda mlima kwa kutumia nyaya. Lifti hiyo ilifanywa maarufu kwa wimbo wa kitamaduni wa Italia “Funiculì, Funiculà.”

Leo, wakazi wa Naples huendelea na shughuli zao bila kujali hatari iliyo karibu sana nao. Watalii huvutiwa na vitu vya kihistoria na kisanii. Kuna utendaji mwingi kwenye maduka na mikahawa, huku mashua nyingi zikionekana kwenye Ghuba ya Naples. Mlima Vesuvius unaendelea kuwavutia watu wengi nao huonekana kuwa rafiki badala ya jitu hatari linalolala.

Auckland—Jiji Lenye Volkano

Jiji la bandarini la Auckland, New Zealand, lina vilima vingi vya volkano. Kwa kweli wakazi wake zaidi ya milioni moja huishi kati ya vilima 48 vya volkano. Mabonde ya kale ya volkano hufanyiza bandari mbili, ambapo visiwa vilitokea kwa sababu ya milipuko ya volkano. Kisiwa kinachoonekana vizuri zaidi ni kile kinachoitwa Rangitoto, kilichotokea miaka 600 iliyopita, ambacho kimeinuka juu ya maji kikiwa na kontua kama za Mlima Vesuvius. Kisiwa hicho kilipofanyizwa baada ya mlipuko wa volkano kijiji cha karibu cha Wamaori kilizikwa kwa majivu.

Wakazi wa Auckland wamejifunza kuishi na volkano zao. Volkano inayoitwa Maungakiekie ni bustani ya umma na shamba la kondoo, nayo iko katikati ya jiji la Auckland. Volkano nyingine ni maziwa, bustani za kupumzikia, au viwanja vya michezo. Moja kati ya hizo ni sehemu ya kuzikia. Wakazi wengi hupenda kuishi kwenye miinuko ya volkano ili wafurahie mandhari zenye kuvutia.

Haielekei kwamba watu walifikiri kuhusu milipuko ya volkano walipoanza kuishi huko Auckland. Watu wa kwanza kuishi hapo ni Wamaori na kisha wakafuatiwa na Wazungu miaka 180 iliyopita. Jambo lililowavutia zaidi ni kwamba eneo hilo lilikuwa karibu na bahari na udongo wake ulikuwa na rutuba. Kwa kawaida, udongo wa volkano huwa na rutuba hata katika sehemu nyingine za dunia. Kwa mfano, huko Indonesia, mashamba bora zaidi ya mpunga yako karibu na volkano hai. Udongo wa maeneo mazuri zaidi ya kilimo huko magharibi mwa Marekani umetokana hasa na volkano. Chini ya hali zinazofaa, ardhi iliyofunikwa na lava inaweza kutokeza mimea katika muda unaopungua mwaka mmoja baada ya mlipuko.

Mifumo ya Kutoa Maonyo Mapema

Huenda wengi wakajiuliza, ‘Je, si hatari kuishi karibu na volkano?’ Bila shaka, jibu ni ndiyo. Lakini wanasayansi wanaweza kupima matetemeko ya nchi na utendaji wa volkano. Kwa mfano, Shirika la Marekani la Uchunguzi wa Jiolojia linachunguza volkano zote hai kutia ndani zile za Naples na Auckland, ambako kuna mipango ya kushughulika na hali za dharura mlipuko wa volkano unapotokea. Kwa saa 24, wanasayansi hutumia Mfumo wa Kupokea Habari Kutoka Katika Setilaiti (GPS) na mitandao ya kupima miendo ya ardhi na hivyo wanaweza kugundua miendo ya miamba iliyoyeyuka na utendaji chini ya ardhi.

Mlima Vesuvius huchunguzwa kila wakati. Serikali ya Italia imefanya mipango ya kushughulikia hali ya dharura ili kuepuka madhara kama yale yaliyotokea mwaka wa 1631. Wataalamu wanadai kwamba wale wanaoishi katika eneo la hatari zaidi wanaweza kuonywa na kuhamishwa kabla ya mlipuko kutokea.

Wanasayansi wanasema kwamba chini ya hali fulani badala ya mlipuko kutokea katika mlima wa volkano, mlipuko huo unaweza kutokea katika eneo tofauti. Na wanadai kwamba Auckland ni moja kati ya maeneo hayo. Wataalamu wanasema kwamba jambo kama hilo linaweza kutokea tu baada ya matetemeko ya nchi yanayodumu kwa siku kadhaa au majuma kadhaa. Ishara kama hizo zinazotokezwa na matetemeko zinaweza kuwapa watu nafasi ya kukimbilia maeneo salama.

Kuzingatia Maonyo

Ingawa kuchunguza volkano ni muhimu, kufanya hivyo ni kazi bure ikiwa maonyo yatapuuzwa. Mnamo 1985 wenye mamlaka huko Armero, Kolombia walionywa kuhusu mlipuko wa Mlima Nevado del Ruiz uliokuwa karibu kutukia. Mlima huo ulipokuwa ukitetemeka kilomita 50 kutoka jijini, wakazi waliambiwa watulie tu. Watu zaidi ya 21,000 walikufa matope yenye moto yalipofunika jiji.

Ingawa majanga kama haya hayatokei mara nyingi, kipindi kati ya milipuko miwili kimetumiwa kufanya utafiti na kujitayarisha. Hivyo, kuendelea kuchunguza, kujitayarisha vya kutosha, na kuwaelimisha watu, kunaweza kupunguza hatari zinazowakabili wale wanaoishi karibu na jitu linalolala.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]

JITAYARISHENI!

Je, mko tayari kwa ajili ya msiba wa asili? Chunguzeni hatari zilizo katika eneo lenu. Pangeni mapema mahali ambapo mtakutana iwapo washiriki wa familia yenu watatenganishwa, na ni nani mtakayejulisha kuhusu mahali mlipo. Wekeni karibu vitu mnavyopaswa kuwa navyo kwa ajili ya dharura, ambavyo vinapaswa kutia ndani chakula, maji, vifaa vya huduma ya kwanza, mavazi, redio, tochi zinazoweza kustahimili maji, na betri za ziada. Hakikisheni mna vitu vya kutosha mnavyoweza kutumia kwa siku kadhaa.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Watalii wakitembea karibu na bonde la Vesuvius

[Hisani]

©Danilo Donadoni/Marka/age fotostock

[Picha katika ukurasa wa 15]

Naples, Italia, mbele ya Mlima Vesuvius

[Hisani]

© Tom Pfeiffer

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mchoro wa msanii wa mlipuko mkubwa wa mwaka wa 79 W.K., ambao uliharibu majiji ya Pompeii na Herculaneum

[Hisani]

© North Wind Picture Archives

[Picha katika ukurasa wa 16]

Rangitoto, mojawapo ya visiwa vingi vya volkano ya Auckland

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Juu na kulia: Mlima Popocatepetl, Mexico

[Hisani]

AFP/Getty Images

Jorge Silva/AFP/Getty Images

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]

USGS, Cascades Volcano Observatory