Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Karibu nusu ya wenzi wote wa ndoa wanakubali wamedanganya kuhusu pesa, yaani, wamewadanganya wenzi wao jinsi walivyotumia pesa.”—THE WALL STREET JOURNAL, MAREKANI.

“Asilimia 84 ya nchi ya Ugiriki inakabili hatari ya kugeuka kuwa jangwa na asilimia 8 tayari ni jangwa.”—KATHIMERINI (ENGLISH EDITION), UGIRIKI.

Lateu, katika kisiwa cha Tegua huko Vanuatu, kwenye Bahari ya Pasifiki, kinaweza kuwa kijiji cha kwanza kuachwa, yaani, kuhamishwa kwa sababu ya hali ya hewa kubadilika. Nyumba zilikuwa “zimefurika [mara nyingi] wakati wa dhoruba na mawimbi makali.”—VANUATU NEWS, VANUATU.

Watu Wenye Umri wa Miaka 100 Waongezeka

Kuishi kufikia umri wa miaka 100 ni jambo la kawaida siku hizi, linasema gazeti New Scientist. Sasa kuna watu 200,000 ulimwenguni pote wenye umri huo. Kulingana na gazeti hilo, kati yao 66 wamefikia umri wa miaka 110. Gazeti New Scientist linatambua kuwa kuthibitisha madai kuhusu kuishi muda mrefu ni vigumu, lakini linasema “ukosefu wa rekodi za kuthibitisha pia kunamaanisha kwamba idadi ya watu walio na zaidi ya miaka 110 inaweza kuwa kubwa kufikia watu 450.”

Muuaji Atambuliwa

“DNA iliyopatikana kwenye meno katika kaburi la kale la Athene imesaidia kutambulisha” muuaji wa kale, linasema gazeti la Kanada Maclean’s. Katika kitabu History of the Peloponnesian War, mwandishi Mgiriki Thucydides alitaja kuhusu pigo la kufisha huko Athene mnamo 430 K.W.K. ambalo lilifanya maadui wao kutoka Sparta kuwashinda katika vita dhidi ya majiji hayo mawili. Ufafanuzi wa Thucydides kuhusu ugonjwa huo haukutosha kuutambulisha. Lakini sasa, uchunguzi wa sehemu ya katikati ya meno ambayo inaweza kuhifadhi virusi kwa karne kadhaa, umewawezesha watafiti kutambulisha muuaji huyo kuwa homa ya matumbo.

Roboti Zinazoweza Kupanda Ngamia

Mchezo wa mashindano ya ngamia, unaopendwa katika nchi za Ghuba ya Uajemi, ulikumbwa na matatizo mashirika ya haki za kibinadamu yalipolalamika kuhusu watoto kutumiwa kupanda ngamia. Hata hivyo, ili kuwawezesha ngamia hao wakimbie mbio zaidi, wapandaji hawapaswi kuwa na zaidi ya kilo 27, kwa hiyo hata vijana walio na umri usiozidi miaka 19 hawafai kutumiwa kwa kuwa ni wazito sana. Wangesuluhishaje jambo hilo? Roboti zinazoweza kupanda ngamia. Wabuni Waswisi, wameunda roboti yenye uzito wa kilo 26 inayoweza kuongozwa kutoka mbali ambayo inaweza kufungwa juu ya tandiko fulani la pekee la ngamia. Ili isimwogopeshe ngamia, roboti hiyo ina umbo na sauti ya mwanadamu. Pia inaweza kuinama, kujisawazisha, kutumia fimbo na kumwelekeza ngamia. Wenye ngamia wamefurahia sana ubuni huo.

Mbegu Yaota Baada ya Miaka 2,000

Mitende iliyokuzwa katika Yudea ya kale, ambayo ilithaminiwa sana kwa sababu ya uzuri, kivuli, na manufaa ya afya, iliharibiwa na wapiganaji wa Vita Takatifu katika Enzi za Kati. Lakini sasa, “wataalamu na wanasayansi wa Israeli wamefaulu kukuza mbegu ya tende ambayo imekuwapo kwa miaka 2,000 hivi,” linaripoti gazeti The New York Times. “Mbegu hiyo, ambayo imebandikwa jina Methusela, ilifukuliwa kule Masada,” ile ngome iliyokuwa juu ya mwamba ambayo ilitekwa na Waroma mnamo 73 W.K. Dakt. Elaine Solowey, mtaalamu wa kilimo katika maeneo makame ambaye aliotesha mbegu hiyo, anasema kwamba itachukua miaka mingi kwa mti huo mdogo kuzaa matunda yoyote, nao utazaa tu ikiwa ni mti wa kike. Anasema kwamba “ikiwa mti huo ni wa kiume, utakuwa tu mti wa kustaajabisha.”